Kikosi cha Simba kipo mkoani Kagera kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu
Bara dhidi ya Kagera Sugar, lakini habari ni kuwa straika wa timu hiyo, Amissi
Tambwe na beki, Joseph Owino wamebaki jijini Dar es Salaam.
Awali iliripotiwa kuwa, Tambwe anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha
mguu (enka) lakini kwa sasa ni mzima na yeye mwenyewe amethibitisha hilo na
kusema kuwa wamempumzisha tu.
Simba ipo mkoani humo kwa ajili ya mechi hiyo inayotarajiwa kuchezwa
kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Kaitaba ambapo Tambwe alikuwa amelala nyumbani
wakati akizungumza na Championi Ijumaa, jana majira ya mchana.
“Mimi siumwi ni mzima tu lakini wameamua kutupumzisha tu. Tutaendelea
kuwa hapa Dar mpaka pale timu itakaporejea,” alisema Tambwe.
Wakati Tambwe akisema hayo, imefahamika uongozi wa Simba umebaini
ujanja unaotumiwa na straika wao huyo kuhusu kutaka kuihama timu hiyo ili
aongezewe maslahi.
Chanzo kutoka ndani ya Simba kimesema kuwa uongozi umemshtukia Tambwe
kuwa hakuna timu inayomhitaji na kudai kuwa taarifa za kuondoka na kuwaniwa na
wapinzani zinatengenezwa ili mchezaji huyo aongezewe maslahi klabuni hapo.
Alipoulizwa Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga juu ya suala hilo
alisema: “Huu ni mchezo tu ambao unafanyika hivi sasa lakini tumeshaugundua,
jambo la msingi Tambwe anatakiwa kutulia na kufanya kazi yake.”
0 COMMENTS:
Post a Comment