Klabu ya Simba SC, imesema inasubiria
mamilioni ya fedha kutoka kwa Klabu ya AS Cannes ya Ufaransa kutokana na mauzo
ya Shomari Kapombe kwa Azam FC.
Simba ilimpeleka nyota huyo Ufaransa
mwaka jana, kwa makubaliano maalum, kuwa iwapo timu hiyo itafanikiwa kumuuza
nyota huyo ndani ya miaka mitatu, basi wataambulia asilimia 40 za mauzo hayo
huku 40 nyingine zikiliwa na Cannes wakati 20 zitakwenda kwa wakala.
Azam kupitia kwa Katibu Mkuu, Idrissa
Nassor, imekuwa wazi kwa vyombo vya habari kwa kusema imemalizana na Cannes na
kuongeza kuwa, Kapombe atavaa uzi wa Azam msimu ujao.
Hata hivyo, Azam wamekuwa wagumu kuweka
bayana kiasi cha fedha walichomchukua, lakini mazungumzo yaliyokuwepo pande
mbili, ni Azam kutoa kitita cha euro 70,000, sawa na Sh milioni 147 za Tanzania
kama wanataka saini yake. Kwa mantiki hiyo, Simba itachukua kitita cha Sh
milioni 58.8 sawa na AS Cannes.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga,
amesema mchakato wa mauzo ya Kapombe ambapo aliweka
bayana kuwa, si mali ya Simba tena kutokana na makubaliano yao, zaidi
wanasubiria fedha kutoka kwa ‘madalali’ wao.
“Kapombe siyo mali ya Simba na kama
inavyosemekana kuwa Azam wamemalizana na Cannes basi sisi tunasubiria chetu.
Unajua Kapombe tulimpeleka kwa makubaliano maalum kwamba iwapo Cannes watapata
timu ya kumnunua, Simba itapata asilimia fulani kwenye mauzo hayo.
“Kwa hiyo kama ameenda Azam nafikiri ni
wakati wa kudai chetu kule Ufaransa,” alifafanua Kamwaga.
Kapombe amekuwa akijifua na Azam na
kupewa jezi namba 30 huku ikidaiwa kuwa uongozi wa Azam umepanga kumpatia gari
lenye thamani ya Sh milioni 30.
Wasiwasi ni kwamba, huenda hadithi ikawa
kama ile ya Emmanuel Okwi ambaye tangu alipouzwa na Simba kwenda Etoile du
Sahel ya Tunisia, bado Wekundu wa Msimbazi hawajapata fedha yoyote hadi leo.
0 COMMENTS:
Post a Comment