Na Saleh Ally
UMESIKIA mara ngapi wanachama au
mashabiki wa Yanga wanathubutu kusema mchezaji au kiongozi fulani aondoke tu
kwa kuwa klabu yao ni kubwa na waliikuta, hivyo hakutakuwa na tatizo!
Mashabiki na wanachama wana ile hali
ya kujidai kwa ajili ya timu zao, mapenzi ambayo huenda wakati mwingine
yanasababisha wajisahau na kuzungumza maneno ambayo yanaonyesha kujaa haraka au
kutokuwa na uchunguzi wa kina na tafakuri jadid kabla ya kuyazungumza.
Najua ningeuliza, huu ni wakati wa
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Mehboob Manji kuondoka Yanga? Wapo ambao wangesema
hapana, lakini rundo wanaweza kusema aende tu kwani yeye ni nani na Yanga
ameikuta!
Ndani ya mwezi mmoja Yanga itakuwa
imekamilisha marekebisho ya katiba yake ambayo ikipitishwa itaanza mchakato wa
uchaguzi na ndiyo utakuwa mwisho wa uongozi wa Yanga chini ya Manji.
Kila kitabu kina muhula wake, lakini
kuna mambo mengi sana kabla ya kusema maneno rahisi kwenye kitu makini au
muhimu.
Msisitizo, lazima ujipime kabla ya kuzungumza ili uonekane tu.
Kwa kuwa wakati wa Manji umekwisha,
Yanga hawapaswi kuona aibu kufanya mambo kadhaa na mawili ndiyo yanaweza kuwa
muhimu kwa ajili ya kuendelea kuisaidia klabu hiyo kupambana.
Hakuna anayeweza kubisha kwamba Manji
amekuwa ni chachu kubwa ya mafanikio katika Klabu ya Yanga na hata wachezaji
lukuki wa klabu nyingine sasa wanatamani kujiunga nayo.
Amefanya mabadiliko lukuki kwa
kushirikiana na timu aliyonayo madarakani na ukiangalia katika kipindi hiki, si
rahisi kusikia kuna upotevu wa fedha katika mzunguko wa mapato ya Yanga au
vinginevyo.
Taarifa zinaeleza kuna udhibiti mkubwa
katika fedha za Yanga na si rahisi tena kuchukua fedha kiujanja kama ilivyokuwa
hapo awali. Hili linawezekana linawaudhi baadhi, lakini ukweli halisi ndiyo
huo, Manji amefanya mabadiliko.
Wachezaji wa Yanga ni kati ya wale
wanaolipwa fedha nyingi zaidi kwa msimu ukilinganisha na kwingine. Ndiyo maana
kwa mwezi, klabu hiyo inatumia zaidi ya Sh milioni 50 kuwalipa mshahara
wachezaji, benchi la ufundi na watendaji.
Katika vitu wanavyotakiwa kufanya,
Manji bado anaweza kuwa kiongozi, kuna uwezekano wa kumshawishi kuendelea
kugombea kwa mara nyingine ikiwezekana aendelee kupambana kuiimarisha mifumo
ambayo ameianzisha.
Kama ataondoka kipindi hiki, viongozi
wapya watakaoingia, lazima wawe ni wale wasiokuwa na njaa, wale wanaotaka
kuiendeleza klabu na timu na si matumbo yao. Lakini njaa ikitangulia, basi kila
alichokianzisha mwenyekiti huyo wa sasa, kitavurugika na Yanga itaendelea
kubaki ilipo.
Akiendelea, mifumo yake itazidi kuwa
imara na hakuna ubishi, kwa miaka yake zaidi ya kumi ndani ya Yanga akiwa
katika vyeo tofauti, ataendelea kusaidia kuiimarisha klabu hiyo.
Umeona namna ambavyo klabu kubwa za
Ulaya zinavyowahifadhi viongozi wake ambao zinaamini wana msaada! Zimekuwa
zikiendelea kuwatumia hata zaidi ya miaka kumi baada ya kuondoka kwao
madarakani.
Manji anajua nini cha kufanya, nini na
nani msaada kwa Yanga. Lakini kuiimarisha Yanga, Simba pia wakapata kiongozi
bora na mwenye mipango, maana yake ushindani utaongezeka na kusaidia soka ya
Tanzania ambayo kila kukicha inajifunza kutembea.
Pili, kama Manji mwenyewe ataamua
kuondoka na kuachia wengine wagombee, bado litakuwa ni jambo zuri kwa maana ya
demokrasia, lakini Yanga hawatatakiwa kumuachia aende zake.
Achaneni na zile hisia, kwamba akienda
kwani yeye ni nani! Pongezi kwa wale walioona umuhimu wake, hawakujali maneno
ya watu wakapiga magoti na kumuomba aendelee kuongoza Yanga kwa kugombea mara
nyingine.
Kama ataendelea kushikilia msimamo
wake, basi safari hii aombwe kuwa kati ya walezi au ateuliwe kuwa Mjumbe wa
Bodi ya Wadhamini, halafu aendelee kusaidia kuendeleza alichokianzisha kwa
kushirikiana na viongozi walio madarakani.
Kawaida hatupendi kuelezana ukweli,
lakini hakuna anayeweza kukataa kwamba viongozi wenye njaa wanaoziongoza klabu
za soka, taasisi au vyama, wamekuwa ni tatizo kubwa kwa kuwa wanafanya juhudi za
kujishibisha wakiwa madarakani na kusahau kuzishibisha klabu wanazoziongoza.
Ukisema Manji anataka kujishibisha
kupitia Yanga, itakuwa ajabu! Fedha anayo, ukisema anataka kujulikana, bado
itakuwa ajabu. Sasa anataka nini Yanga? Jibu analo mwenyewe. Lakini kama ni
hali halisi, inaonyesha ni mapenzi yake mwenyewe.
Manji bado anahitajika Yanga, iwe kwa
kugombea au ateuliwe na kuendelea kusaidia gurudumu la maendeleo ya klabu hiyo.
Wekeni kando ushabiki, kuwa na watu watano kama Manji, basi tayari maendeleo
katika soka yanapiga hatua kwa kasi kubwa.
Kumpoteza Manji mmoja kabla ya kupata
mwingine ni sawa na kulazimisha kuendesha gari lisilokuwa na mafuta. Linaweza
kutembea kwenye mteremko tu, likifika kwenye mlima, mwisho wa safari umewadia.
Katika hili, Yanga bado wana nafasi ya
kuwa na uamuzi wa kufanya, wana haki ya kuona kipi ni sahihi kwao na wanataka
kufanya nini. Lakini haya ndiyo mawazo yangu kwao kutokana na hali halisi
ninavyoona. Wakiyakubali, itakuwa poa sana.
0 COMMENTS:
Post a Comment