Imeelezwa kuwa kila kitu kipo tayari kwa ajili ya kocha Fred Felix
Minziro, kusaini mkataba kwa ajili ya kuinoa JKT Ruvu, msimu ujao, lakini wachezaji
wapya wa timu hiyo wakawa kikwazo katika kukamilika kwa zoezi hilo.
Minziro aliyeanza kuinoa JKT kwenye mzunguko wa pili wa ligi akitokea
Yanga, ameliambia Championi Jumatano kuwa, tayari ameshaafikiana na uongozi
lakini zoezi la kuchuja wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao limeingilia
kati ufanikishwaji wa kusaini mkataba wake huo.
Kwa sasa timu za JKT na Ruvu Shooting, zipo kwenye mchakato wa mchujo
na usaili wa wachezaji wenye vipaji na uwezo mzuri watakaoweza kuzitumikia timu
hizo msimu ujao.
Kocha huyo alisema kwamba kuhusu kusaini mkataba mpya JKT, hilo halina
shida kwa kuwa tayari ameshamalizana na uongozi kila kitu lakini mara baada ya
zoezi hilo la mchujo kukamilika basi atasaini mkataba wake huo.
“Kama ni mazungumzo tayari nimeshamalizana na uongozi, kilichobaki
sasa ni mimi kutia saini, lakini hili zoezi lilitakiwa kufanyika mapema kama si
muingiliano wa programu ya kutafuta wachezaji wapya.
“Zoezi hili likiisha basi mara moja tutakamilisha ishu ya mkataba na
kuhusu vijana ni kwamba bado tunaendelea kuwapokea na tutachagua kati ya nane
mpaka kumi, kwa watakaoonyesha uwezo mzuri, lakini kama wakikosekana hapa basi
tutaangalia njia nyingine ya kufanya usajili,” alisema Minziro.
0 COMMENTS:
Post a Comment