May 28, 2014

DIEGO AKITOKA NJE DAKIKA YA 9.


Na Saleh Ally
MITAA mbalimbali katika miji tofauti nchini, gumzo ni namna Atletcio Madrid ilivyoshindwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku ikiwa imefanikiwa kumla ng’ombe mzima na mkia wake, ikabakiza manyoya tu ya mkia!
Wengi walionyesha kushangazwa na namna Atletico Madrid walivyoshindwa kuhimili sekunde 90 tu, wakamruhusu Sergio Ramos kusawazisha kwa Real Madrid na dakika za nyongeza wakafungwa mabao mengine matatu na matokeo ya mwisho kuwa 4-1.
SIMEONE AKIMLAUMU MWAMUZI

Gumzo hilo la Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Shinyanga, Mbeya na kwingineko ni la dunia nzima. Lakini kosa kubwa lilianzia kwa kocha Diego Simeone.
Lengo si kumlaumu, lakini uamuzi wa kumchezesha mshambuliaji wake nyota, Diego Costa huku akijua ni mgonjwa ulikuwa ni tatizo.
Huenda Simeone aliamini angewatisha Madrid, lakini akalazimika kumtoa Costa katika dakika ya tisa tu.Tatizo au makosa yalianzia hapo.
ENEO ALILOCHEZA MARCELO

Kosa 1:
Hauwezi ukamponda na kusema Simeone ni kocha asiyejua mambo, kama ni hivyo, swali litakuwa vipi alifika fainali au kutwaa ubingwa wa La Liga?
Lakini ukweli uko hivi; alifanya makosa makubwa katika suala la Diego Costa ambaye alimchezesha kwa dakika tisa maana yake kitendo cha kumtoa na kumuingiza Adrian, yalikuwa matumizi mabaya ya nafasi ambayo angeweza kuitumia katika dakika za mwisho wakati wanaongoza kwa bao 1-0.
Atletico ilishindwa kupambana kwa sekunde 90 ambazo ni asilimia 0.1 ya mchezo.
Lakini kama Atletico wangekuwa na nafasi hiyo, wangeingiza beki wakati wa dakika za nyongeza na ingewasaidia katika mambo mawili makuu.
Moja, ingesaidia kupoteza muda kwa kuwa mchezaji mmoja hadi kutoka ndani ya uwanja, anachukua hadi sekunde 45 kama atajua namna ya kuutumia muda vizuri.
Pili, ni suala la kushusha presha. Atletico Madrid walionekana kuzidiwa mwishoni lakini hakukuwa na mbinu ya kupoza presha ile na mabadiliko ya kutoa na kumuingiza mchezaji yangesaidia.
Kwa kawaida, wakati mchezaji anatoka kuna mambo mengi yanatokea uwanjani kwa watu profesheno. Kwanza ni mazungumzo kati ya wachezaji na kuelekezana wapi wanakosea.
Pili, mwalimu anapata nafasi ya kuzungumza na wachezaji wake kwa ufasaha kwa kuwa kama mechi inaendelea, kitaalamu mchezaji humsikiliza mwalimu kwa asilimia 35 na zilizobaki anazibakiza kwenye mchezo.
Tatu, wakati timu kama Madrid ikishambulia kwa kasi, kuanzishwa kwa zoezi la kumtoa na kumuingiza mchezaji, kawaida linaondoa ile kasi yao na wanalazimika kuanza mwanzo, kawaida lazima wanatoka mchezoni.
Halafu hata wakianza tena, hawawezi kuwa katika kasi waliyokuwanayo na wanalazimika kuanza kujipanga upya na kwa muda mchache uliokuwa umebaki, ingekula kwao.
Kosa 2:
Utaona kosa la pili linasisitiza kosa la kwanza lilivyokuwa hatari, kwa kuwa wakati Madrid wakishambulia kama nyuki kutoka kushoto, Simeone alitakiwa kumtoa Juanfran ambaye hakuwa ‘fresh’ kutokana na kuonekana akilalamika maumivu mara kadhaa na angeingia mtu mwingine mwenye nguvu kusaidia kuongeza ugumu kutoka upande huo.

Hilo halikuweza kufanyika kwa kuwa tayari Simeone hakuwa na nafasi ya kufanya mabadiliko, hivyo akampa nafasi Marcelo ambaye ndiye mtu aliyekuwa chachu kubwa ya mabadiliko kiuchezaji kwa Madrid.
Marcelo aliyeingia dakika ya 59, alibadilisha aina ya ukimbiaji wa timu, akaongeza kasi ya Di Maria aliyekuja kuwa nyota wa mchezo na Madrid ikarudi katika kiwango chake hasa dakika za mwisho.
Bado Simeone hakuwa na la kufanya zaidi ya kujaribu kutoa maelekezo kwa wachezaji wake kujaribu kutumia mbinu mbadala ambayo hata hivyo hakuwa nayo.

Vikosi na mabadiliko:
Real Madrid: Casillas; Carvajal; Varane; Sergio Ramos; Coentrao (Marcelo, 59); Khedira (Isco, 59); Modric; Di Maria; Ronaldo; Bale; Benzema (Morata, 79).
Atletico Madrid: Courtois; Juanfran; Godin; Miranda; Filipe Luis (Alderweireld, 83); Gabi; Tiago; Koke; Raul Garcia (Sosa, 66); David Villa; Diego Costa (Adrian, 9).


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic