NIANZE na
kuwapongeza Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu kwa kuonyesha uzalendo kutokana
na kuwahi kuichezea timu ya taifa, Taifa Stars ikiwa ni siku moja tu baada ya
kumaliza kuitumikia TP Mazembe.
TP Mazembe
ilikuwa ina kibarua cha mechi ya kimataifa nchini Sudan dhidi ya Al Hilal, mara
tu baada ya mechi hiyo, Samata na Ulimwengu walifunga safari haraka kuja nchini
kuitumikia Stars na siku iliyofuata, yaani jana, wakaingia uwanjani kupambana.
Waliofika
uwanjani au waliofanikiwa kuiona mechi hiyo waliona walivyopambana,
hawakuonyesha uchovu au kutegea na badala yake wote wawili walicheza dakika 90.
Ni kitu chema na mfano wa kuigwa.
Nikirejea
katika kikosi cha Taifa Stars, pongezi kwao kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya
wageni Zimbabwe ambao baada ya siku chache, kikosi chetu kitakuwa ugenini na
wenyewe kuwa wenyeji wetu.
Stars
inatakiwa sare au ushindi tena ili kupata nafasi ya kuingia kwenye makundi ya
kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika mwakani nchini Morocco.
Pamoja na
ushindi wa Stars, hakika sikuvutiwa na namna timu ilivyocheza kwa maana ya
kupambana na kuhakikisha tunashinda. Inawezekana wengine wameona sahihi, mimi
pamoja na ushindi, niliondoka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam nikiwa na
hofu.
Kwamba kwa
namna tulivyocheza, tutaweza vipi kuwatoa
Zimbabwe kwao. Jana tulikuwa
nyumbani, lakini idadi ya mashambulizi, aina ya uchezaji, Wazimbabwe
walionekana utafikiri wako Harare.
Uhodari wa
kipa na walinzi na viungo wa ukabaji ulichangia Stars kutoka na ushindi huo
mwembamba wa bao 1-0, la sivyo ingekuwa sare au ingewezekana kupoteza kabisa,
kitu ambacho kingekuwa kibaya.
Kocha mpya, Mart
Nooij huenda asiwe anajua hamu au kiu kuu ya Watanzania katika michuano ya
kimataifa. Inaonekana Kombe la Dunia haliko jirani yetu, inakuwa kazi ngumu.
Basi si vibaya tukianzia angalau kwenye Kombe la Mataifa Afrika na
tunalihitaji.
Hongera
Nooij kwa kuanza mechi yako ya mashindano kwa ushindi wa bao 1-0 lakini timu
haikucheza na Tanzania ina wachezaji waliokamilika hasa uliokuwa nao katika
kikosi cha jana.
Mashambulizi
waliyopanga Stars, mengi yaliishia njiani au washambuliaji kulazimisha kupiga
mashuti ya mbali kwa kushindwa kuutegua mtego wa Wazimbabwe ambao walitukosa
zaidi ya mara tano katika kipindi cha pili tu, tena kwa mashabulizi ya
kuwafanya Watanzania waingie katika hofu.
Stars
ilikuwa na wachezaji wanaocheza hapa nyumbani, lakini wako wanaocheza kwenye
nchi mbalimbali kama Qatar, DR Congo na waliowahi kucheza Ufaransa. Lakini
katika mechi ya jana, timu haikuwa imeunganika, haikuwa na ushirikiano sahihi
na hakukuwa na mapambano sahihi.
Upangaji wa
mashabulizi haukuwa ni ule unaoonekana kuunganika kuanzia katika safu ya ulinzi
yakienda yanapanda kwa mpango na mwisho kuwa imara au mashambulizi bora.
Tukienda hivyo Harare, tutarejea na aibu.
Pia tatizo
jingine lilikuwa ni kiungo, licha ya kuundwa na wachezaji wengi nyota lakini
Stars haikuwa imeunganika, walishindwa kuwa mhimili wa mawasiliano na kuifanya
timu ipande ikiwa imejikusanya sahihi
kufanya ‘mabaya’ kwa Wazimbabwe.
Hii si
dalili nzuri, inaashiria kazi ya Harare itakuwa ni kubwa maradufu na Stars
lazima wajipange vilivyo. Nooij lifanyie kazi kwa kuwa Watanzania wamechoka
kubahatisha au kusikia ilibaki kidogo tu. Safari hii tunataka kuona timu
inafanikiwa, la sivyo kutakuwa hakuna maana ya kufanya mabadiliko kwenye benchi
la ufundi.
Muda wa
maandalizi utakuwa unatosha kabisa na Nooij na benchi zima la ufundi la Stars
litakuwa na muda pia kuangalia nini cha kufanya lakini hata leo mkalale huku
mkitambua Watanzania hawataki hadithi tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment