Na Saleh Ally
ASIYEPENDA
kusikiliza maoni ya watu, akaamini anajua kuliko mtu yeyote, mara nyingi
huishia kufeli, kuna mifano ya watu wengi sana.
Lakini
katika kusikiliza, si lazima kila unaloambiwa ulifanyie kazi, kwa kuwa kuna
maoni ambayo yanaweza kuwa si sahihi, ukisikiliza kila uliloambiwa na
kuliamini, pia unaweza kufeli.
Ndiyo maana
Wanasimba wakamuamini Evans Elieza Aveva na kumpa urais kwa kuwa wanajua ana
uwezo wa kuikwamua klabu yao kutoka kwenye matatizo, migogoro, kashfa kibao za
uuzaji wachezaji bila ya kupata fedha na mengine mengi.
Pamoja na
malumbano kwa zaidi ya mwezi kuhusiana na uchaguzi mkuu, hatimaye wanachama wa
Simba, jana waliamua kumpa Aveva dhamana ya kuiongoza klabu yao hiyo ambayo
inahitaji mabadiliko ili kurudi kwenye maendeleo na sifa yake kwa kuwa Simba ni
klabu maarufu barani Afrika na yenye mafanikio katika nyanja za kimataifa kwa
hapa nyumbani.
Simba
imekuwa kwenye utulivu kwa miaka mingi, kabla ya uongozi wa ‘uncle’ Ismail Aden
Rage, haujaingia madarakani ambao katika miaka minne ni mwaka mmoja tu ulikuwa
una mafanikio, baada ya hapo ni migogoro, uadui na matatizo lukuki.
Matatizo
yaliyoondoa umoja ndiyo yaliyoifanya Simba kupoteza sifa yake ya sharubu imara na
badala yake karibu kila timu, zikiwemo hata Mbeya City iliyopanda daraja,
zikaanza kuisumbua, kuifunga na hata ukipenda unaweza kusema waliionea Simba.
Simba
haikuwa Simba tena, ndiyo maana wakati Wanasimba wanakupa kura, wengi wao
watakuwa wanataka mengi lakini mawili furaha ya moyo, yaani kuwa na timu
inayoshinda na maendeleo ya klabu, vitakuwa ni vitu vya kwanza kabisa.
Vipande:
Simba
imevunjika vipande, kipindi cha Rage kilikuwa cha hovyo, watu hawakuwa na
upendo, hawakuelewana na mwisho kila mmoja akaishi kwa kuangalia maslahi yake
na si yale ya Simba tena.
Ndiyo maana
uliona Simba ilivyoyumba, kwa kuwa kila mmoja aliigeuza chukua chako mapema,
hivyo una kazi ya kuzuia hilo na badala yake kila mmoja afanye kwa maslahi ya
klabu.
Siri:
Inawezekana
watakaosoma makala haya, wataelewa lakini siri itabaki kuwa ya kwako kwamba
siku zote msemakweli, anachukiwa.
Wala
usisimame, songa mbele kama utakuwa unafanya mambo kwa ajili ya maslahi ya
klabu. Pia ningekushauri hata kama utakuwa unajua mambo mengi ya klabu hiyo
kuliko mimi, usikubali kupendwa sana.
Nimeona
viongozi wengi wanaoingia madarakani wamekuwa wakipenda sana kuonekana watu
wazuri wanaotaka kumfurahisha kila mtu, ni kosa kubwa.
Kama kuna
mtu au kundi la watu linaharibu, basi waeleze ukweli kwa nia na njia nzuri na
mwisho lengo liwe umoja na kusaidia kuijenga Simba.
Umoja:
Kama
nilivyoeleza awali, Simba ya sasa iko katika vipande. Moja ya kazi kubwa ni
kuunganisha makundi makubwa ambayo chuki zao ni zile za kibinadamu na
zinaiumiza Simba.
Najua
hauwezi ukafanya mambo yote kwa wakati mmoja, lakini umoja ni kati ya mambo ya
mwanzo kabisa kuanza kuyafanya kwa kuwa bila ya kuwa pamoja hakuna kitu kimoja
kinaweza kuwa cha umoja na kushika namba moja.
Binadamu
wana kawaida ya kusahau, huenda wako waliokuwa na hasira kwa kuwa walitaka
kugombea wakaondolewa, wengine wana hasira kwa kugombea na kushindwa. Lakini
wote hao ni Simba na wana uwezo wa kuisaidia klabu yao.
Hivyo
Aveva, una kazi kubwa ya kuwaunganisha Wanasimba hata kama itakuwa ni taratibu
huku ukiendelea kufanya mambo mengine ya mafanikio.
Simba ni
kubwa, kwa hali iliyokuwa imefikia, haiwezi kubadilika ndani ya siku mbili na
kila kitu kikaenda tofauti. Lazima muda wa kutosha unatakiwa.
Lakini
hakuna mabadiliko yatakayopatikana kwa siku moja bila ya kuanza taratibu. Hivyo
ni vizuri kuanza taratibu kuwaunganisha Wanasimba kwa ajili ya kujenga Simba
moja imara kuliko ‘visimba’ vingi visivyokuwa na ushirikiano na mwisho ni kuiua
tu nguvu ya klabu hiyo.
Najua utakuwa
na kazi kubwa sana, karibu usaidie kuendeleza soka na kama kawaida, ukipatia
tutakumwagia sifa za kutosha, lakini siku ukikosea, basi ukweli ndiyo ada.
0 COMMENTS:
Post a Comment