Na Saleh Ally
ENGLAND haikuwa imepoteza
mechi yake ya kwanza ya Kombe la Dunia tokea mwaka 1986, lakini usiku wa kuamkia
jana, haikuwa na ujanja dhidi ya Italia ‘Azzurri’.
Wakati England imepoteza
mechi hiyo kuna mengi yataibuka lakini chanzo, kivutio cha mchezo huo alikuwa
ni kiungo wa Italia Andrea Pirlo mwenye umri wa miaka 35.
Kiungo huyo wa mabingwa
wa Italia, Juventus ndiye alikuwa kila kitu aliyeichanganya England alivyotaka
yeye, akaipeleka mechi hiyo iende alivyopanga yeye.
Kuna mambo mengi
Waitaliano walifanya lakini la kwanza, kila walipopata mipira, kabla ya kwenda
mbele ilikabidhiwa kwa fundi huyo ili aanze kupanga anataka waende vipi na
alifanya hivyo.
Kila walipohisi kuna
presha kubwa ya kushambuliwa, basi ikitokea wamepokonya mpira kutoka kwa
wachezaji wa England, Pirlo alikabidhiwa mpira naye anaanza kazi ya kupanga
mipango ambayo ilikuwa ina madhara kwa England.
Kitakwimu, England ilimiliki
mpira kwa 25% na Italia 75%, kazi kubwa ikifanywa na Pirlo ambaye alikuwa
mchezaji aliyegusa mpira mara nyingi zaidi yaw engine wote katika mechi hiyo.
Ingawa mwisho wa mechi,
Mario Balotelli aliyefunga bao la pili na la ushindi kwa Italia alitangazwa
kuwa mchezaji nyota wa mechi, Pirlo alikuwa zaidi ya nyota.
Mashabiki wa Italia, muda
mwingi waliimba “olés, oles”, huku Pirlo akiendelea kuupoza mpira na kupanga
mechi nzima iende anavyotaka yeye.
Kabla ya mechi hiyo,
mmoja wa memba wa benchi la ufundi, Gary Neville alianzisha zoezi la kumdhibiti
babu huyo na kuliita “Operation Stop Pirlo”, Neville anaijua kazi yake. Lakini
mwisho amefeli.
Juhudi za kumtumia Jordan
Henderson, hazikuzaa matunda, mkongwe Steven Gerrard alijitahidi, lakini kazi
ilikuwa ngumu na hata alipopewa jukumu hilo Danny Welbeck, ili amvuruge, bado
kazi haikuwa lahisi.
Pamoja na kampeni, Pirlo alipiga
pasi 69 katika kipindi cha kwanza na zikafika kwa 96% ambayo ni ya juu kuliko ya wachezaji
wote.
Pia ndiye alikuwa
stesheni na anayewaagiza Marco Verratti na Daniele de Rossi, wafanye nini,
maagizo yake hayakuwa kwa maneno, badala yake basin a vitendo, kazi ikafanyika.
Awali Kocha wao, Cesare
Prandelli aliamua waanze na mfumo wa 4-3-2-1, haukufanya kazi vizuri, wakaingia
kwneye 4-1-4-1 na hapo ndipo England ilipofia.
Prandelli amembadika
Pirlo jina la “mchezaji wa wote”. Akimaanisha kocha yoyote anaweza kumtumia kwa
kuwa anaweza kucheza aina yoyote ya mfumo wa soka.
Yeye ameimuingiza kwenye
mfumo wa rejeta, hiki ni kifaa ambacho hutumika kupoza injini inayofanya kazi.
Ndiyo maana gari zinawekewa maji, kupitia rejeta.
Kila Italia walipokuwa
wanashambuliwa sana, mpira unapelekwa kwa Pirlo ili kupoza mambo kwa kuwa
katika historia yake ya soka, hajawahi ‘kupaniki’.
Pirlo amekuwa akisema
hivi: “Kupaniki ni kujimaliza zaidi, mchezo wa soka unatoa zaidi nafasi ya
kurekebisha makosa na ukipaniki, unaiua nafasi hiyo, ndiyo maana napenda
kutulia zaid.”
Pirlo bado ana uwezo wa
kuendelea kutoa somo kwa vijana katika mechi zijazo za Kombe la Dunia. Ukubwa
dawa, lakini kazi yake haina mwingine.
0 COMMENTS:
Post a Comment