UAMUZI
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusimamisha uchaguzi wa Simba uliopangwa
kufanyika Juni 29, mwaka huu umenishitua na bado sijaelewa vizuri!
Nilikuwa
kati ya waandishi waliohudhuria kikao chake wakati akitangaza kuhusiana na
uamuzi huo uliojaa kila aina ya mikanganyiko ambayo inayonyesha Simba haitakuwa
tena na matumaini ya kufanya vizuri msimu ujao, nitaeleza.
Kabla
ya kulizungumzia suala la kutofanya vizuri, turudi kwenye hili la kusimamisha
uchaguzi na kuutaka uongozi wa Simba kuunda kamati ya maadili ni la kukurupuka
na linaonyesha lina jambo ndani yake.
Angalia
mambo haya, baada ya kamati ya uchaguzi kufanya kazi yake na kumuengua Michael
Wambura, alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa chini ya TFF. Kamati hiyo
ikachukua uamuzi wa kumrudisha.
Lakini
bado kuna wanachama waliendelea kukata rufaa wakijumuisha masuala kadhaa ambayo
mengine yalipelekwa na kamati ya uchaguzi kwenye kamati ya maadili ya TFF.
Sasa
TFF inalirudisha suala hilo Simba, hali ambayo ingelazimisha kufuta kwanza kwa
uamuzi uliotolewa na kamati ya rufaa ya TFF. Maana jambo hilo liliishatoka
kwenye mikono ya Simba na kuingia TFF, sasa limerudishwa tena kwenye klabu hiyo
wakati vyombo vya shirikisho hilo viliishatoa maamuzi!
Tayari
huu ni mkanganyiko mkubwa! Pili, TFF imeagiza kuwa hadi Juni 30, siku moja
baada ya tarehe ya uchaguzi waliokuwa wamepanga Simba, ndiyo uundaji wa kamati
hiyo ya maadili iwe imekamilika.
MALINZI |
Itakayofanya
kazi ya kuunda kamati hiyo ni kamati ya utendaji. Sasa hicho ndiyo kichekesho
cha kuvunja mbavu na hata magoti, kama Wambura amerudishwa kugombea, maana yake
bado ni mjumbe wa kamati ya utendaji.
Maana
yake naye atashiriki kuunda kamati ya maadili ambayo itafanya kazi ya kujadili
masuala yanayompinga yatakayowasilishwa kwenye kamati hiyo. Ingekuwa kabla ya
mchakato wa uchaguzi kama ilivyofanyika kwa kamati ya uchaguzi sawa, si sasa
uchaguzi umeanza na fitna kibao.
Inajulikana
uongozi uliopita chini ya Ismail Aden Rage umegawanyika akiwemo Rage mwenyewe.
Wengine wanaunga mkono huku, wengine kule, hivyo suala la kamati hiyo ni vurugu
mpya ndani ya Simba, TFF na Malinzi wanalijua hilo.
Nikirudi
kwenye hoja ya kwanza kabisa, kwamba Simba itaendelea kuteseka, kwa kuwa
haitakuwa na muda tena wa maandalizi, nasherehesha na suala hilo la uundaji wa
kamati ambalo mwisho wake ni Juni 30.
Halafu
zitapangwa siku za kukaa kwa kamati hiyo mpya, ndani yake kutakuwa na muda wa
wale watakaokata rufaa kwenye kamati ya maadili ya TFF kama hawataridhika na
uamuzi wa kamati ya maadili ya Simba.
Kimahesabu,
inaonekana uchaguzi wa Simba unaweza kufanyika mwishoni mwa Juni. Mwezi mmoja
kabla ya ligi kuanza, itakuwa Agosti 24, sasa jiulize lini uongozi mpya
utaingia madarakani na kuanza kufanya usajili, maandalizi ya timu kwa uhakika?
TFF
wanalijua hilo, hata kama watasema hawahusiki wanajua namna Simba imekuwa na
machungu mambo kwenda hovyo kwa ajili ya kutaka kufanya kitu Fulani. Awali,
nilianza kupata hisia huenda ni kwa lengo la kumlinda mtu Fulani ndiyo maana
mambo yanakwenda shaghalabaghala bila ya kujali maslahi ya Simba.
Lakini
Malinzi akajibu swali la kwamba kuna taarifa anambeba Wambura kwa vile alikuwa
ni kampeni meneja wake. Yeye akasema hakuwahi kutangaza hilo na watu
wanamzushia.
Kwa
kuwa limetoka mdomoni mwake, si vibaya kumuamini. Lakini hili la uchaguzi
kusimamishwa, kusubiri kuundwa kwa kamati ya maadili katikati ya uchaguzi wa
Simba ni kuiangamiza Simba. Nasisitiza TFF inalijua hilo.
0 COMMENTS:
Post a Comment