KWA mara nyingine, Yanga
imeingia kuwa moja ya klabu inayochagiza katika masuala ya msisimko wa soka
nchini kwa kuamua kuajiri watu watatu kutoka nchini Brazil kwa ajili ya
kuitumikia.
Pamoja na makocha hao
wawili, Yanga wamejiri kiungo mchezaji anayeitwa Andrey Coutinho ambaye atakuwa
na kazi ya kurudisha kiungo cha Jangwani.
Yanga imewahi kuajiri makocha wawili kutoka Ulaya,
pia wachezaji wawili kutoka Ulaya wote wakiwa makipa kwa nyakati tofauti
wakaichezea timu hiyo.
Ilikuwa ni sehemu ya
kuonyesha kuwa timu ya Tanzania inaweza kuajiri wachezaji kutoka nchi tofauti
ingawa huko nyuma, Malindi ya Zanzibar iliwahi kuajiri mchezaji pia kutoka
Brazil.
Safari hii Yanga, imerudi
tena na kuweka rekodi nyingine ya kuajiri raia watatu wa Brazil ambao wanakuja kufanya
kazi kuhakikisha kikosi chake kinakuwa bora zaidi.
Jambo la wageni hao
limefanywa kitaalamu, kwanza Yanga wameanza kumnasa Maximo ambaye uwezo wa kazi
yake ulionekana wakati akiinoa Taifa Stars. Halafu yeye akapewa kazi ya
kutafuta msaidizi pamoja na kiungo.
Yanga haitalaumiwa kwa kuwa
Maximo ambaye amepewa kazi ya kuinoa Yanga kwa mafanikio ndiye ameachiwa
apendekeze wa kufanya nao kazi kutoka nchini kwao Brazil. Kila kitu kimekwenda
kitaalamu.
Vizuri kuupongeza uongozi wa
Yanga kwa hatua uliopiga ambayo itakuwa ni changamoto au funzo kwa aina yoyote
ile. Mfano Wabrazil hao wakifanya vema kutakuwa na somo, lakini wakifeli, bado
kutakuwa na jambo la kujifunza kwa wadau wa soka nchini.
Pamoja na hivyo, kuna kila
sababu ya kuamini Coutinho kama mchezaji hawezi kuwa malaika katika kikosi cha
Yanga kwa kuonekana ujio wake kama kila kitu kimemalizika.
Wala kusiwe na wanaoamini,
huenda Coutinho atakuwa na uwezo wa Ramirez wa Chelsea au Neymar wa Brazil kwa
kuwa tu wote ni wachezaji kutoka Brazil, hiyo haiwezi kuwa sawa.
Matarajio ni kuona Coutinho
anatoa mchango wake katika kikosi cha Yanga kama ambavyo mchezaji yoyote
‘profesheno’ anatakiwa kuifanya kazi yake anapotoka nchini kwao na kwenda
kucheza nchi nyingine.
Bila shaka atakuwa anajua
kwamba ana deni kutoka kwa uongozi na wanachama wa Yanga ambao wanatarajia
kuona makubwa kutoka kwake. Lakini makubwa hayo yasiwe ya kipimo cha umalaika,
watu kuamini huenda hakosei au akicheza katika kikosi Yanga haiwezi kufungwa.
Bado wachezai walio Yanga
wanapaswa kumchukulia mchezaji huyo kama changamoto, lakini suala la kugombea
naye namba linabaki palepale na lazima washindane naye na kushirikiana naye pia
ili kuifanya ofisi yao ambayo ni Yanga inapata mafanikio.
Kumvika umalaika, itakuwa ni
tatizo na huenda itawaingiza Yanga kwenye presha kubwa, mfano kama vile kuamini
akiwepo yeye, basi wao hawawezi kufungwa au lazima watafanya vizuri.
Coutinho atakuwa na uwezo wa
kufanya vizuri zaidi kama atapata naye atatoa ushirikiano ili kujenga kikosi
imara cha Yanga ambacho kinataka kufanya vizuri katika michuano ya nyumbani na
ugenini.
Hakuna ubishi lazima Mbrazil
huyo atapata shida mwanzoni, kuna suala la mazingira ambayo lazima yako tofauti
nay ale ya Brazil, hivyo atahitaji muda nab ado watu wanapaswa kulikubali hilo.
Lakini kama itagundulika
hana lolote, basi bado Yanga wana haki ya kukataa kuuziwa Ubrazil na badala
yake watake mchapakazi. Mara moja uongozi unaweza kuchukua hatua na kumrejesha
kwao.
Hivyo kumuunga mkono ni
jambo bora sana kwa maana ya kumsaidia afanye kazi yake vizuri. Lakini pia kuwa
wazi kama wakiona ameshindwa kazi, basi litakuwa jambo zuri ili kuonyesha
kwamba wako ‘siriaz’ na wasingependa kuona utani kwenye maendeleo ya klabu na
timu yao.
Tusubirini tuone.
0 COMMENTS:
Post a Comment