MAGORI |
Na Saleh Ally
NILIWAHI
kuzungumzia kuhusiana na Coastal Union kuachana na malumbano yasiyokuwa na
sababu dhidi ya aliyekuwa mdhamini wao, Nassor Bin Slum ambaye ni mnazi mkubwa
wa timu hiyo.
Mwisho Bin
Slum ameondoka na kuamua kufanya mambo yake kibiashara zaidi, sasa kampuni yake
kupitia matairi na betri za magari, inadhamini timu tatu za Ligi Kuu Bara
ambazo ni Mbeya City, Stand United na Ndanda FC. Coastal wameanza kupitisha
harambee kuweka mambo yao sawa!
Simba kuna
Kundi la Friends of Simba (FOS), linaundwa na wanachama wengi wao wakiwa ni
wafanyabiashara wakubwa, ni watu wazima wenye uwezo wa kifedha.
Ndiyo kundi
linaloongoza kwa kujazwa kashfa karibu na kila anayekuwa madarakani au shabiki
wa waliopo madarakani. Simba ikishinda FOS hawahusiki, ikifungwa wanakuwa
wamehujumu wao.
Kumekuwa na
kashfa nyingi kuhusiana na watu wa kundi hilo, lakini hakuna aliyewahi kusimama
na kutoa ushahidi kuhusiana na wanaowatuhumu. Ikifika uchaguzi, hata kama
hakuna mgombea anayetokea FOS, basi lazima utasikia kundi hilo limetajwa na
lawama tele ambazo hazina uthibitisho.
Huenda wengi
wanahofia kuzungumzia walichokifanya FOS kwenye maisha ya Simba, wanahofia
kuonekana ‘wamenunuliwa’ kama ilivyozoeleka au kuwaudhi wale wasiowapenda FOS,
mimi siogopi.
FOS wanaweza
kuwa na mabaya yao, wao ni binadamu, lakini ni kundi lililofanya mazuri mengi
Simba na yako wazi. Vipi kila kitu kwao ni matusi na lawama tu?
Wakikosea
wakosolewe bila ya woga, huo ni msingi sahihi wa maendeleo, lakini walipopatia,
ukweli uwe wazi na wasifiwe.
Kuna watu
Simba ambao hawawapendi FOS lakini zitakuwa sababu binafsi na zaidi ni za
kimaslahi, lakini huenda hata baadhi ya wapinzani wa Simba na hasa watani wao,
Yanga, wasingependa kuwaona FOS wakiiongoza Simba, huenda wanakumbuka kile
kipindi cha miaka saba bila kukishinda kikosi hicho kutoka Msimbazi.
Kwa miaka
saba, Simba ikiwa na watu wengi wa FOS, iliinyanyasa Yanga ambayo ushindi wake
dhidi yao ulikuwa ni sare, zaidi ya hapo ni kipigo. Hivyo, Yanga watakuwa na
haki ya kutotaka kuwaona tena FOS wakirudi.
Mpira ni
fedha, Azam FC inafanya mabadiliko sasa kwa kuwa ina fedha. Yanga kuna Yusuf
Manji, uwezo wa mipango, uwezo wa kutoa mamilioni ya fedha, ndiyo maana
wanachama walitaka abaki.
Unapoambiwa
kuwa FOS wanainyonya Simba, halafu ukaangalia kundi hilo baadhi ya watu wake
kama Crescentius Magori, Zacharia Hans Pope, Kassim Dewji, Mussa Batenga, Azim
Dewji, Evans Aveva, Musley Al Rawah, Salim Try Again, Mohammed Nassor, Adam
Mgoyi, Swed Nkwabi na wengine wengi ni watu wenye uwezo kifedha.
Kama
wanaiibia Simba, jiulize Simba kwa mwaka inaingiza kiasi gani, inatumia kiasi
gani na watu kama hao ambao wengine ni mamilionea, wanagawana kiasi gani ili
wafaidike kama inavyoelezwa?
Simba
inapokuwa imebanwa, hasa wakati wa mechi dhidi ya Yanga, hurudi na kuwaangukia
ili waweke msaada wao, baada ya mafanikio hakuna kiongozi anayesema tena.
Wapo
wanachama wanaosisitiza hivi: “Hata kama wanaiba, angalau wanatupa furaha ya
ushindi.” Lakini katika wanaosema ni wezi, hakuna aliyewahi kuthibitisha au
kutoa mfano zaidi ya mmoja kupokea maneno huku na kuyasambaza kule bila ya kuwa
na uhakika.
Usajili:
Inawezekana
kabisa kipindi hiki FOS watakuwa katika ushindani mkubwa katika suala la usajili,
lakini inajulikana wakati ule walivyoitesa Yanga hasa ile chini ya Francis
Kifukwe, walikuwa wakifanya wanavyotaka.
Simba ilikuwa
na wachezaji karibu wote waliokuwa bora, taratibu walianzisha mpango wa kupata
wachezaji bora na moja ya mifano mizuri ni pale mmoja wa wajumbe wao alipoamua
kuuza basi na kumsajili Mark Sirengo kutoka Kenya.
Aveva ndiye
alipewa kazi ya kusafiri hadi Nairobi kufanya mazungumzo na Sirengo,
akafanikiwa kumleta nchini na alikuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa na wenye
msaada mkubwa.
Kama
unakumbuka akina Selemani Matola, Said Sued ‘Panucci’, Juma Kaseja, Christopher
Alex, Boniface Pawasa, Ulimboka Mwakingwe, Victor Costa Nampoka na wengine ni
wachezaji walioonekana kama hawafai mwanzo lakini nguvu ya FOS iliwarudisha na
kuanza kujiamini, ubora wao ukaonekana.
Kukubalika:
Wapo
wanaoamini FOS ni wababaishaji, waliopo kwa ajili ya kuivuruga Simba lakini
kuna makocha wanasikia faraja na wanataka kufanya kazi na kundi hilo.
Mmoja wa
makocha hao ni Patrick Phiri, raia wa Zambia, ambaye kila akiitwa Simba, basi
lazima atauliza kama watu fulani wapo na wote ni memba wa FOS. Anaamini anaweza
kufanya nao kazi vizuri na mambo yakaenda sawa.
Kocha
mwingine ni Milovan Cirkovic raia wa Serbia, mmoja wa makocha vipenzi katika
Klabu ya Simba ambaye aliondolewa nchini si kwa uwezo, badala yake
kutokukubalika kwa baadhi ya viongozi wa Simba chini ya uongozi wa Ismail Rage,
lakini pia baadhi ya wajumbe wa FOS ambao hayakuwa matakwa ya kundi hilo.
Kuondoka kwa
Milovan ambaye aliiongoza Simba kutwaa ubingwa na kuitwanga Yanga kwa mabao
5-0, kipigo cha kihistoria, taratibu, kikosi kikaanza kuporomoka hadi kufikia
kuonekana ni cha kawaida kama timu nyingi za kawaida.
Makosa:
FOS si
malaika, kuna makosa mengi wamefanya kama binadamu na huenda mengine hatuyajui
ingawa mafanikio na chachu yao katika soka ni changamoto.
Wakati
mwingine wao kwa wao wamekuwa wakikinzana, wengine wanataka hili na wengine
lile, maana wako wengi na asilimia kubwa wana uwezo kifedha.
Hali hiyo
imekuwa ikisababisha katika vipindi fulani Simba kuyumba kwa kuwa wao kwa wao
hawaelewani. Hii imetokea mara kadhaa na hasa katika uamuzi wa masuala ya
usajili wa wachezaji au kuajiri kocha mpya.
Inawezekana
hata sasa kama Aveva ambaye ni mwenzao ataingia madarakani, basi makosa
yakawepo kama binadamu. Lakini kama kweli ni wazoefu, wamepita kwingi basi
wanapaswa kuwa watu waliojifunza na wasirudie makosa waliyopitia.
Badala yake
wafanye kila wanachoamua kwa ajili ya Simba, ingawa kupishana kimawazo ni jambo
la msingi sana. Kinachofikiwa katika uamuzi wa mwishoni vema kikaheshimiwa.
Katika kundi
kubwa kama lao halikosi vikundi vingine vidogovidogo hata kama vitakuwa
vimejificha ndani yake. Hivyo vinaweza kuwa hatari kwa FOS kwa kuchangia kufeli
au hata kuivuruga Simba kabisa!
Faida:
Mmoja wa
viongozi wa Friends of Simba, Kassim Dewji, ndiye aliyejenga jengo la pili la
Simba ambalo linaiingizia klabu hiyo Sh milioni 180 kila mwezi, hakuna ambaye
ameweza kusema ahsante.
Wengi
wamekuwa wakisema msingi wake ulitakiwa kuwa wa ghorofa nane lakini
umechakachuliwa, maana yake wanalaumiwa, lakini kila fedha zikiingia,
zinatumika kuisaidia klabu na kuna uhakika wa nyingi tu zimekuwa zikiingia
kwenye mifuko ya wajanja.
Mafanikio:
Simba wakati
inafikia fainali ya Kombe la Caf mwaka 1993, Azim Dewji ambaye sasa ni Friends
of Simba, ndiye alikuwa mfadhili, Kassim Dewji alikuwa katibu mwenezi.
Mwaka 2003,
Simba ikafanya jambo kubwa katika historia ya soka Afrika. Kwanza ikaifunga
Zamalek kwa Cairo na kuivua ubingwa wa Afrika, hakuna timu ya Tanzania
iliyowahi kufanya hivyo.
Pili,
iliifunga na kuitoa mashindano timu bora kuliko zote barani Afrika katika
kipindi hicho na kwa mara ya kwanza ikacheza hatua ya nane bora ya Ligi ya
Mabingwa Afrika.
Wakati
ikifanya mambo hayo, Simba ilikuwa chini ya uongozi wa katibu mkuu, Dewji
ambaye ndiye aliongoza kila kitu kwa kushirikiana na FOS.
FOS ndiyo
waliingia mifukoni na kuchangisha fedha ili kuongezea chache zilizokuwa
zimepatikana kwa ajili ya kuweka kambi Oman.
Baadhi ya
wajumbe wa FOS walitoa mamilioni kuhakikisha wanampata kocha Talib Hilal ambaye
alikubali kupunguza bei na kusaidiana na kocha James Aggrey Siang’a, raia wa
Kenya, kuinoa Simba ikiwa Oman kwa ajili ya mechi ya marudiano jijini Cairo.
Simba
ilishinda na hadi leo imeweka rekodi nyingine ya kuwa timu iliyopokewa na watu
wengi zaidi kuliko nyingine yoyote. Hiyo ilitokea wakati wakirejea kutoka Cairo
na zaidi ya watu watatu walifariki dunia siku hiyo.
Zengwe:
FOS
wanasifika kwa fitna za kisoka, wako wanaosema huwahonga marefa au wachezaji wa
timu pinzani, lakini hakuna ambaye amewahi kuthibitisha.
Inabaki
katika zile kauli zinazoelea za kwenye kahawa kama Manji kahonga au Azam FC
imechukua ubingwa kwa kuwa ilihonga, vitu ambavyo vinakuwa havina ushahidi na
vinalenga kuchafua tu.
Ingekuwa
vizuri kama kuna mtu ana ushahidi na hilo na lengo lake ni zuri, basi
angejitokeza na kuisaidia jamii yetu ya soka kuhusiana na kitu na ukweli uwe
wazi kuhusu FOS badala ya taarifa za gizani, sawa na aliyefungua macho kwenye
giza akijaribu kutembea huku anapapasa!
Inawezekana
ndani ya FOS kuna watu wabaya, lakini haiwezekani wote wakawa wabaya. Vizuri
kukawa na kipande cha kuwapa moyo kwa kuwa hali halisi inaonyesha wanajitolea.
Sawa Saleh, makala NZURI lakini watakuja hapa kukuambia kuwa umehongwa, ni vizuri umeshaandika kuwa HUWAOGOPI... Hao jamaa wanaokwenda mahakamani nahisi watakuwa wametumwa, sio bure. Ni aina ya watu wanaofurahi wakiona SSC imekwama.
ReplyDelete