Kikosi cha Taifa Stars ambacho jana (Juni 1 mwaka huu) kiliitupa
Zimbabwe (Mighty Warriors) nje ya michuano ya Afrika baada ya kutoka sare ya
mabao 2-2 kinarejea nchini leo (Juni 2 mwaka huu) kutoka Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itatua
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa
12.30 jioni kwa ndege ya Kenya Airways ikitokea Harare kupitia Nairobi.
Stars imefuzu kucheza raundi inayofuata kwa ushindi wa jumla ya
mabao 3-2, kwani awali (Mei 18 mwaka huu) iliifunga Zimbabwe bao 1-0 katika
mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika raundi ya pili, Taifa Stars itacheza na Msumbiji ambapo
itaanzia nyumbani kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano
itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taifa Stars imeendelea kupokea salamu za pongezi
kutoka kwa wadau mbalimbali baada ya kufanikiwa kuvuka kikwazo hicho cha kwanza
katika harakati zake za kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani
nchini Morocco.
Salamu hizo
zimetoka kwa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Manyara (MARFA), mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza
(MZFA), John Kadutu, na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd Mgoyi.
0 COMMENTS:
Post a Comment