Uongozi wa Mbeya City umesema hauna sababu ya kuwalaumu wachezaji kwa
kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Nile Basin, kwa kile walichosema kuwa kwa
kiwango chao, kufika robo fainali ni hatua kubwa mno.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Mbeya City kushiriki michuano ya
kimataifa, tangu kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita.
Akizungumza kutoka Sudan, Msemaji wa
timu hiyo Freddy Jackson, alisema kuwa wanatarajia kuwasili nchini leo asubuhi
au alfajiri sana, lakini hii yote itategemeana na ratiba ya ndege.
Aidha Jackson, alisema licha ya kutupwa nje kocha Juma Mwambusi na jopo zima la timu hiyo,
halina cha kulaumu bali kujivunia kutokana na kupata changamoto na imewapa
uzoefu wa kutosha wachezaji wao.
“Sawa kila timu ina ndoto ya kutwaa ubingwa na sisi ndiyo ilikuwa
‘tageti’ yetu, lakini ndiyo hivyo tumetolewa. Hatuwezi kulaumu sana na lazima
tujivunie kufika robo fainali kwa timu kama Mbeya City ambayo ndiyo kwanza
ilinusa michuano hii.
“Kuna kitu tumejifunza, wachezaji wetu wamepata uzoefu fulani
ambao utatusaidia katika ligi kuu msimu unaoanza,” alisema Jackson.
Aliongeza kuwa, huenda wasivunje kambi baada ya kufika huku, au
wakatoa likizo ya wiki moja ya mapumziko kabla ya kuendelea ya kambi kwa ajili
ya maandalizi ya ligi kuu bara.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetanmgaza tarehe ya
kuanza kwa ligi kuu ambayo itaanza kurindima Agosti 24, mwaka huu.
Gud
ReplyDelete