July 9, 2014



Na Saleh Ally
MARCIO Maximo amerejea nchini kwa mara nyingine, safari hii akiwa kocha wa kikosi cha Yanga chini ya klabu hiyo kongwe.


Alikuwa kocha aliyefanikisha kuipeleka Taifa Stars kwenye michuano ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) nchini Ivory Coast, pia akachangia kuamsha hamasa ya kikosi hicho cha taifa.

Pamoja na mafanikio aliyopata, changamoto zilikuwa nyingi zikiwemo zile za kuingia kwenye bifu na baadhi ya wachezaji, kukosa washambuliaji wa kiwango alichotaka na mengi. Baada ya kutua Yanga, ametaka yote yasahaulike kwa kuwa sasa anaanza upya.

Ataiweza Yanga? Jibu ndiyo, kwa kuwa ni kocha ambaye pia amewahi kufundisha klabu mbalimbali kwao Brazil na hata barani Ulaya. Lakini sasa ndiyo wakati mwafaka kwake kuzijua vizuri changamoto za soka nchini.

Asipokuwa makini na imara, basi changamoto hizo anaweza kuziona kama adui kwani akizishinda, ataonekana amefanya vizuri na kuendelea kubaki Yanga. Lakini zikimshinda, basi ajue hakutakuwa na maswali mengi, safari itamkuta.

Inawezekana zikawa changamoto nyingi sana ambazo Maximo analazimika kupambana nazo ili kushinda vita ya mafanikio. Lakini hizi tano inabidi azitazame kama adui anayetaka kumshinda na lazima atakutana nazo.

Viwanja vibovu:
Kama utajumlisha siku zote za maandalizi ya Taifa Stars, ilikuwa haichezi zaidi ya mechi 15 kwa mwaka. Hivyo siku za maandalizi zilikuwa ni chache, pia mazoezi yake na mechi zote zilichezwa kwenye viwanja vyenye kiwango kizuri.

Sasa Maximo anakumbana na ubovu wa viwanja vya mazoezi na vile vya mikoani, kikosi chake kitapata changamoto ya namna ya uchezaji na si ile ya kutandaza mpira chini kwa kasi.

Waamuzi:
Waamuzi ni tatizo kubwa, mechi nyingi wamekuwa wakiboronga, ukiachana na wale wachache ambao hufanya vizuri. Lakini bado kuna upangaji wa kupendelea baadhi ya timu fulani.

Waamuzi waliokuwa wanachezesha mechi za Taifa Stars, walitokea nchi jirani, viwango vyao vilikuwa juu kwa kuwa wako chini ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) pia Fifa, hivyo viwango vyao ni juu zaidi ya wale wa nyumbani ambao wengi wamekuwa wakifanya madudu.

Mechi nyingi:
Wakati akiwa Taifa Stars alikuwa anajiandaa kwa mechi sita au saba tu kwa msimu mzima. Sasa mambo ni tofauti, Ligi Kuu Bara ni mechi 26, lakini kuna zaidi ya mechi tano za kirafiki, pia zile za kimataifa.

Presha ni kubwa, hatakuwa na muda wa kupumzika na Yanga wanachotaka ni kushinda hata kama ni mechi ya kirafiki, analazimika kufanya kazi mfululizo na lazima apunguze jazba ili kuliweka jeshi lake safi mechi baada ya mechi.

Hujuma:
Inaonekana ni siri, lakini rekodi zipo nyingi kwamba watu wa timu moja, hata kama hawachezi nayo basi watataka kuihujumu. Wanaficha sana lakini hayo yanafanyika sana katika ligi hiyo.

Kuna baadhi ya timu zimewahi kuelezwa kuwa hadi na vitengo vya watu maalum ambao kazi yao ni kuzivuruga timu nyingine. Presha hiyo haikumkuta akiwa Taifa Stars, lakini hawezi kumaliza mechi 26 bila kuonja uchungu wa mambo hayo.

Wakati mwingine hujuma zinaweza kutokea hadi ndani ya kikosi cha Yanga yenyewe kwa wale ambao wangefurahi kuona inapoteza na uongozi uonekane haujafanya jambo!

Simba:
Hapa ndiyo kuna presha kubwa, ikiwezekana hata ile ya kukosa kombe la Ligi Kuu Bara. Maximo ana dakika 180 dhidi ya Simba, yaani mechi ya mzunguko wa kwanza na wa pili, kama haitatokea mechi nyingine hapo katikati kama ile ya Nani Mtani Jembe.

Kwake tayari ni presha kubwa ambayo hajaizoea na anatakiwa kupambana nayo kweli, Wanayanga furaha yao ni kuifunga Simba na huenda wanaweza kuvumilia kupoteza mechi moja lakini si zote.

Wakati akiwa Taifa Stars, presha ilikuwa ni kushinda dhidi ya wageni ambao lazima wataondoka baada ya mechi. Lakini Simba ni wenyeji kama Yanga, wakikufunga wanabaki hapa nchini na majigambo na majivuno yanaendelea, presha kubwa.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic