MWAIKIMBA AKIWA NA KIPRE TCHETCHE |
Straika mkongwe wa Azam, Gaudence Mwaikimba,
amemwambia straika mpya wa timu hiyo, Didier Kavumbagu kuwa anakwenda kujifunza
kutoka kwake.
Kavumbagu alijiunga na mabingwa hao katika
dirisha hili la usajili akitokea Yanga sambamba na Frank Domayo, ambapo
ameifanya safu ya ushambuliaji kuwa na hofu kubwa ya namba kwa sasa.
Mwaikimba
alikiri kuwa Kavumbagu ameongeza ushindani wa namba, lakini kwake si lolote
kwani ni kama amekuja kujifunza mengi kutoka kwa mkongwe huyo kuliko mchezaji
yeyote.
Mwaikimba, ambaye amedumu kwenye ligi kuu kwa zaidi ya miaka kumi,
amekuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Azam, hususan katika mechi za mikoani
ambapo mastraika wengi wa Simba, Yanga na Azam pamoja na maprofesheno wengine,
wamekuwa wakichemka.
“Kwanza Kavumbagu ana bahati kubwa kuja kipindi hiki, maana ana
nafasi ya kujifunza mengi kutoka kwangu. Mimi ni mkongwe na kuna vitu vingi
ambavyo atajifunza kutoka kwangu, ingawa na mimi vipo ambavyo nitajifunza
kutoka kwake.
“Kweli ameleta changamoto katika suala la namba, lakini pia ni
faida kwa wote kwani ni kipindi cha kila mchezaji kujituma mara mbili ili
kupata namba kikosi cha kwanza,” alisema Mwaikimba.
Ujio wa Kavumbagu, pamoja na Mhaiti, Leonel Saint Preux, umeifanya
safu ya ushambuliaji ya Azam kuwa na watu saba, wakiungana na Kipre Tchetche,
John Bocco pamoja na makinda Joseph Kimwaga na Kelvin Friday.
0 COMMENTS:
Post a Comment