August 2, 2014



MANCHESTER, England
MAZUNGUMZO mengi mwishoni mwa Fainali za Kombe la Dunia yalikuwa ni juu ya kocha mpya wa Manchester United, Louis van Gaal, kwamba ni mchezaji yupi hatamtumia au atamtumia katika kukijenga kikosi chake kwenye msimu wake wa kwanza klabuni hapo.


Tayari van Gaal ameshatua Man United na michezo ya kwanza tu ya maandalizi imeonyesha Manchester United itakuwa ya namna gani msimu ujao.

Van Gaal ameanza kutumia mfumo wa 3-5-2, ambao unasimamisha mabeki watatu tu nyuma, ambao pia aliutumia alipokuwa na Uholanzi kwenye Kombe la Dunia.

Ni dhahiri kwamba kutakuwa na ushindani mkubwa wa namba Manchester United, hasa kwa upande wa viungo washambuliaji, lakini mfumo wa 3-5-2 ambao van Gaal atautumia, utampa nafasi Mhispania, Juan Mata kuonyesha thamani yake na kuwa mchezaji muhimu kwa Mashetani Wekundu.
Mfumo na majukumu
Kwenye mfumo wa 3-5-2 ambao van Gaal amekuwa akiutumia, Mata atakuwa fiti kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kati mbele ya viungo wawili wakabaji na nyuma ya washambuliaji wawili.

Atakuwa mchezaji muunganishaji wa timu ambaye atakuwa anaweza kufanya kazi ya kuchezesha na kukata mistari, kuivuta timu kutoka katikati na kuisogeza mbele hadi maeneo hatari, aidha kwa pasi au kwa chenga.

Shinji Kagawa, Adnan Januzaj na wengine kadhaa watakuwa wanashindania namba na Mata katika nafasi hiyo, lakini Mata ana uwezo na uzoefu wa Ligi Kuu England unaomwezesha kupata nafasi hiyo.

Kucheza katikati hakumzuii kukimbia pembeni na kutafuta nafasi na spidi yake itamruhusu kukimbia haraka kwenye eneo la ushambuliaji katika muda mwafaka.

Mizunguko ya mchezaji bila mpira na uwezo wa kuuona mchezo wote ni muhimu na Mata ana uwezo huo katika soka lake.

Rooney na Mata
Inavyoelekea, van Gaal atakuwa akiwachezesha Wayne Rooney na Robin van Persie mbele zaidi, lakini Rooney ndiye atakayekuwa na kazi ya kuzunguka zaidi kama Mata ambaye atakuwa nyuma yake kidogo, lakini van Persie mwenyewe anaweza akawa na jukumu la kufunga tu.

Muunganiko huu na kazi ya kuzunguka itakayofanywa na Rooney pamoja na Mata, utakuwa ni wa kuvutia, hasa mmoja atakapokuwa akishuka chini zaidi, iwe kwa nafasi au kwa kumvuta beki, hilo litaifanya Man United kuonekana hatari sana mbele na hatari zaidi ikifika kwenye eneo la penalti.

Inaweza pia kuifanya United ionekane ikitumia mfumo wa 3-4-2-1, kuliko wa 3-4-1-2 katika mchezo wa wazi, kwa kuwa mbele kutakuwa na wanaume wenye uwezo wa kuwachangaya wapinzani kwa kukimbia huku na kule wakibadilishana nafasi huku namba zao zikiwa ni zilezile. Ukiwa na namba 10 mmoja na ukitumia mabeki wanaopanda badala ya mawinga, msisitizo mkubwa unaangukia kwenye ubunifu na uwezo wa mchezaji ambaye atapata mpira katika eneo la mbele.

Kama Mata peke yake hatoshi, Man United ina wachezaji wengi wanaoweza kuwasababishia wapinzani maumivu kutokana na uwezo wa kukimbia na kubadilishana nafasi.
Mchango unaotarajiwa
Akiwa siyo mmaliziaji wa mwisho, Mata atakuwa pengine akitarajia mabao 15 msimu ujao, wakati Manchester United itakapokuwa ikitumia mbinu mpya ya van Gaal.
Mata alikuwa chanzo kikubwa cha kutengeneza nafasi katika kikosi cha Chelsea kabla kocha Jose Mourinho hajaamua kumuweka nje ya timu. Kama akicheza mbele na watu wengi wakimzunguka ili kufanya kazi ya kuzuia, Mata anaweza akatengeneza kati ya nafasi za mabao 90 au 100 kwa msimu mmoja.
Bila shaka, hilo linategemea na yeye mwenyewe jinsi atakavyoamua kuwa kwenye ubora wake wote ambao hadi sasa bado hajauonyesha katika kikosi cha Manchester United.
Lakini msisitizo ni kwamba, mfumo ambao unatarajiwa kutumiwa na van Gaal msimu ujao, unatarajiwa kutengeneza ubora kwa wachezaji muhimu, ambao mmojawao ni Juan Mata.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic