Na Saleh Ally
SIKU chache zilizopita,
mshambuliaji Mbwana Samatta wa TP Mazembe aliamua kuzungumzia namna ambavyo
anaona kikosi cha timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kimekuwa kikipata ugumu.
Kauli hiyo ya Samatta
unaweza kusema imechelewa kwa kweli Taifa Stars imekuwa ikiathirika kwa kiasi
kikubwa kutokana na kutegemea wachezaji wengi zaidi wanaocheza nyumbani.
Lakini hakuna ambaye amekuwa
tayari kusema hilo, huenda kwa kuwa wengi wanacheza nyumbani au wale wanaocheza
nje, wamekuwa wakiamini iwapo watasema hivyo wanaweza kuonekana wanawadharau
walio nyumbani.
Ukweli unajenga, ukweli
unabadilisha mambo na ndiyo dawa kila kunapokuwa na upungufu kwenye jambo.
Kukaa kimya ni kuendelea kukuza tatizo. Hivyo Samatta anaweza akawa shujaa wa
kipindi hiki kutokana na kuamua kuvunja ukimya kwa kuwa huo ndiyo ukweli.
Alichokisema Samatta ni
shule na huenda wachezaji wengi ambao wako hapa nyumbani wanaweza kujipima au
kutafakari alichosema mshambuliaji huyo wa TP Mazembe.
Ukweli kama Tanzania
ingekuwa ina wachezaji wengi wanaocheza katika nchi za jirani, Afrika
Magharibi, Kaskazini na hata Asia na Ulaya ingesaidia kuleta mabadiliko kuliko
kuwa na wengi wanaocheza nyumbani pekee.
Samatta mwenye anaweza kuwa
mfano mzuri sana katika hilo. hakuna anayeweza kukataa tena kuwa mshambuliaji
huyo na mwenzake Ulimwengu ndiyo tegemeo la ushambuliaji la Taifa Stars.
Leo kama Ulimwengu na
Samatta hawapo, kila mmoja atakwenda uwanjani na hofu kwamba nani ataleta
kashkash au kufunga mabao. Kweli Taifa Stars ni timu, lakini umahiri wa vijana
hao wawili, umetengenisha mafuta na maji na uwezo ndiyo unawafanya kila mmoja
awaamini.
Ukweli Samatta na Ulimwengu
hawajaujenga uwezo huo kupitia kwa waganga wa kienyeji, badala yake mambo
matatu makubwa. Kwanza kujiamini, pili kujaribu na tatu nia ya kuamini wanaweza
kufanya, wakaingia kwenye ushindani.
Samatta si mchezaji wa muda
mrefu, ukihesabu miaka aliyochipukia Mbagala Marketi iliyokuja kuwa Afrika
Lyon, muda mchache aliocheza Simba na sasa tegemeo la Taifa Stars na klabu
kubwa kama ya TP Mazembe utaona alijiamini, akajaribu kusonga mbele na sasa
yuko anapambana kwenye ushindani.
Ndiyo, yuko kwenye ushindani
kama Ulimwengu ambaye alikuzwa pale kwenye kituo cha vijana cha TFF.
Akajaribu
kwenda Sweden kabla ya kuuzwa TP Mazembe. Leo wawili hao wanafanikiwa kucheza
Mazembe yenye mafowadi saba kutoka nchi za Zambia, DR Congo na Ghana nab ado
wanapata nafasi.
Ushindani wanaoupata TP
Mazembe ndiyo unaowafanya Ulimwengu na Samatta waendelee kuimarika. Ukubwa wa
timu hiyo ya DR Congo, unawapa nafasi ya kushiriki michuano mikubwa ya kimataifa
mara kwa mara kuliko wachezaji wengine wa Tanzania.
Kauli ya Samatta, kama
kungekuwa na wengine watano wanaopata changamoto kama wanazopata wao wakiwa na
TP Mazembe, basi Stars ingekuwa imara zaidi kwa kuwa kungekuwa na wengi
walioimarika na wanaoweza kuisaidia zaidi.
Hakuna maana waliopo sasa
wanadharaulika, lakini hakuna ubishi kucheza ugenini kuna ushindani na majaribu
mengi ambayo kama mchezaji yuko tayari kuingia kwenye ushindani, basi
anaimarika zaidi.
Tabia ya kuridhika na
wanachopata hapa nyumbani, au kuona Yanga, Simba na Azam FC ndiyo mwisho wa
safari ni kujidumaza. Badala yake Samatta na Ulimwengu wanaweza kutumiwa kama
mfano mzuri wa hivi karibuni wa wachezaji wa hapa nyumbani kukubali changamoto.
Kama vipaji na uwezo wa juu,
wachezaji wengi wa hapa nyumbani ni bora hata kuliko wale wa Zambia, DR Congo,
Rwanda, Uganda, Kenya na kwingineko. Tatizo moja tu, hamko tayari kuukabili
ushindani, halafu ni waoga ile mbaya!
0 COMMENTS:
Post a Comment