Na Saleh Ally
SASA ni uhakika kwamba Barcelona itamtumia Luis
Suarez katika safu yake ya mashambulizi kuhakikisha inarejesha makombe
yaliyopukutika.
Mataji ya Copa del Rey, La Liga na Ligi ya
Mabingwa Ulaya yalikuwa ni mambo ya kawaida kabisa katika kikosi hicho ambacho
msimu uliopita kilitoka kapa.
Kutoka katika chuo chake cha soka cha La Masia,
aina ya uchezaji wa Barcelona umekuwa kivutio kikubwa, lakini ndani ya misimu
miwili mambo yameonekana kwenda sivyo.
Baada ya kuondoka Pep Guardiola na nafasi yake
kupewa Tito Vilanova ambaye sasa ni marehemu, taratibu kasi ya kikosi hicho cha
Balaugrana ilianza kuporomoka.
Hata baada ya kupewa Kocha Tata Martino, bado
mambo hayakuwa na mabadiliko makubwa, naye baada ya msimu mmoja, akaondoka
kurejea kwao Argentina.
Kikosi kimerudishwa kwa mmoja wa magwiji wa
Barcelona, Luis Enrique aliyekuwa mmoja wa viungo wa pembeni wenye kasi kubwa.
Kurudi kwa Enrique ni jambo bora, lakini
usisahau kuongezeka kwa fowadi mpya Luis Suarez sasa kumekamilika.
Kukamilika kwake ni baada ya juhudi za kumtetea
apunguziwe adhabu baada ya kufungiwa miezi minne kutokana na kumng’ata beki wa
Italia, Giorgio Chiellini, wakati wa Kombe la Dunia nchini Brazil. Sasa
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limemruhusu afanye mazoezi na Barcelona
na kucheza mechi za kirafiki.
Ujio wa Suarez unaifanya fowadi ya Barcelona
kuundwa na watu watatu hatari zaidi lakini wote wanatokea Amerika ya Kusini.
Unaonekana umekuwa ni utamaduni, kwamba
Barcelona inaamini zaidi washambuliaji nyota kutoka Amerika Kusini kama
ilivyokuwa kwa Ronaldo Lima, Romario, Ronaldinho na baadaye Lionel Messi.
Sasa ina Neymar na Suarez na usisahau msimu
uliopita, mmoja wa tegemeo alikuwa ni Alexis Sanchez aliyetua Arsenal.
Barcelona wanategemea zaidi fowadi kutoka
kusini mwa Amerika na swali linaweza kupata majibu pale Suarez atakapoanza
kuichezea mwishoni mwa Oktoba katika mechi ya El Classico dhidi ya Real Madrid.
Suarez alifunga mabao 31 na kuwa mfungaji bora
wa Ligi Kuu England ambayo ina mikiki na ngumu kwelikweli. Neymar akiwa mgeni
alipiga mashuti 68 katika La Liga na kufunga mabao 11.
Messi akiwa amepiga mashuti 160 na pasi 11 za
mabao, hiyo ni msimu uliopita. Amekuwa mfungaji bora zaidi ya mara mbili, msimu
uliopita pamoja na kuwa majeruhi, alifunga mabao 28.
Wote watatu, jumla walifunga mabao 70, wana
nafasi ya kufunga zaidi ya hayo na kama kweli wakiwa na Barcelona halafu
wakafunga kwa idadi hiyo, hakuna shaka kikosi hicho
kitakuwa na nafasi ya
kutwaa kombe au makombe.








0 COMMENTS:
Post a Comment