Na Saleh Ally
NCHI hii raha sana, watu wengi sana wanaishi
kwa ujanjaujanja na bado wanapata heshima mbele ya jamii na kuonekana ni watu
wenye mchango kwenye jamii.
Bila kupindisha nazungumzia wale wanaojiita
wasaidizi na washauri wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi, kwamba ni watu ambao hawana msaada wowote.
Inawezekana kabisa, TFF inayoongozwa na
Malinzi ipo katika hatua za mwisho kuzama na kuweka historia mpya ya kuwa na
uongozi uliokuwa ukitumainiwa na wengi kwamba unaleta mabadiliko ya soka
nchini, kumbe hauwezi hata kujua ofisi sahihi kwao ni ipi.
Kama mtu hajui hata ofisi yake inapaswa kuwa
wapi ambapo ni sahihi kutokana na kipato anachoingiza, ataweza vipi kuleta
mabadiliko kwenye kitu husika?
Nani anategemea maendeleo yapatikane kwa TFF
hii ya Malinzi iliyojaa wasaidizi kibao ambao hawana tija na si wataalamu
sahihi wa sehemu husika walizowekwa?
Yupi anaweza kusema kuna mafanikio ya soka
yanakuja huku mamilioni ya fedha yakitumika kwa ushauri usio sahihi na watu hao
bahati mbaya hawataki kukosolewa?
Kuna msaidizi mmoja wa Malinzi amenitumia
salamu kupitia kiongozi mmoja wa soka, kwamba anataka kunitumia chatu. Hii
inaonyesha kiasi gani watu bado wanaishi na mawazo ya zamani, ingawa pumzi
wanayovuta ni ya sasa.
Huyo anayetaka kunitumia chatu ni kwa kuwa tu
nilihoji uhalali wake wa kuwa TFF. Namsubiri huyo chatu na leo ninaendelea
kuhoji Malinzi kuwa na rundo la wasaidizi au washauri ambao hawana msaada.
Wanalipwa fedha na nani, kwa nini fedha hizo
zisitumike kwa ajili ya maendeleo ya mpira badala ya kuwapa watu hao ambao
wanafanya mambo yao kiujanja?
Kuna ule msemo; “dunia siyo mbaya, walimwengu
ndiyo wabaya.” Inawezekana Malinzi pia anaweza asiwe mbaya, lakini ‘wapambe’
anaowajaza TFF kwa ajili ya ‘ushkaji’, kuridhishana kwa kuwa walimsaidia kwenye
uchaguzi, ndiyo watakaomuangusha na kuuangusha mpira wetu.
Wakimuangusha Malinzi, haitakuwa biashara ya
Watanzania kwa kuwa amepita kwingi kuanzia akiwa promota wa ngumi. Akaanguka na
kuinuka na maisha yakaendelea, hilo litamhusu yeye na hao ‘washikaji’ zake.
Lakini kuuangusha mpira wa Tanzania kwa ajili
ya kuwafurahisha ‘wapambe’ au ‘washkaji’ kitakuwa si kitu rahisi kukubalika,
hasa kwa Watanzania ambao hawapo tayari kuona wanaendelea kudidimizwa na watu
wanaotaka kujifaidisha badala ya kuufaidisha mchezo wa soka.
Mfano ambao unaonyesha TFF chini ya Malinzi
haijui njia sahihi ya kupita, ni suala la Shirikisho la Soka la Kimataifa
(Fifa) kuingilia hadi wapi shirikisho hilo linapaswa kuweka ofisi.
TFF iliamua kuhamia mjini kwenye ghorofa la
PPF Tower ambako lilikuwa likilipa hadi Sh milioni 15 kwa mwezi. Likaacha ofisi
zake kwa madai pale kuna mpango wa uendelezaji wa eneo hilo, kukawa na taarifa
NSSF ndiyo wameingia mkataba na TFF kwa ajili ya ujenzi.
Sasa ni zaidi ya miezi minne, TFF hakuna
inalolifanya katika eneo la Karume huku mamilioni ya fedha ambayo yangetumika
kwenye soka la vijana na lile la wanawake, yakitumika kulipia hilo jengo la PPF.
Washauri au wasaidizi wa Malinzi wako wapi?
Vipi hawakuona kwamba hilo ni tatizo na kumshauri? Hadi imefikia Fifa wamekuja
nchini na kugundua hilo ni tatizo na kuitaka TFF irejee Karume ambako haitalipa
hata senti, kweli Malinzi na ‘vijana’ wake wamerejea Ilala!
Hili jambo linasikitisha, linaumiza na
inaonekana mwendo wa TFF hii ya Malinzi ni majanga katika soka nchini na kama
mtawaachia waende hivi, tutakwisha.
Maana yake Fifa wasipoona kuna jambo baya, wao
hawawezi kuliona. Hatukaki kurejea katika enzi za utumwa, kuwa watu tunaoagizwa
au kuamrishwa tu kama watwana au nyampara anayewaeleza nini cha kufanya
wafungwa wenzake.
Kikubwa ni kujitambua, kusimama kama
Watanzania ambao tunataka kuleta maendeleo kwenye mpira wetu. Malinzi lazima
akubali kupokea changamoto na kupambana kwa maendeleo ya soka kwa manufaa ya
Watanzania.
Malinzi, mliondoka Karume mkisema kuna suala
la kuboresha, vipi, liko wapi? Wakati Fifa wanawaambia mrejee mbona hamjasema
kuna programu ya uendelezaji? Hasara ilikuwa kiasi gani?
Fedha mlizopanga PPF Tower zilikuwa kiasi gani
na zingesaidia soka yetu kwa kiasi gani? Kuna hatari ya Tanzania kuzidi
kuporomoka na yale mabadiliko yaliyojitokeza wakati wa uongozi wa Leodegar
Tenga nayo yakayeyuka halafu tukarudi kule enzi za Fat.
Kuna kila sababu Malinzi aone kuna tatizo,
abadilike na aachane na hao watu wanaotaka kuwatumia watu chatu au majini, kisa
wamewakosoa.
Aachane na watu wanaotaka nchi ijaze watu
waoga, wanaohofia kusema ukweli, kisa wataumizwa au kutumiwa chatu! Hapa kwa
lengo la kujenga na si kuwaacha kina fulani waendelee kuharibu. Acha wengine
wakae kimya, lakini Tanzania hii si ile ya wale akina nanihii waliokuwa
wanafanya wanavyotaka.
Tunahitaji maendeleo, mkumbuke kama chatu wenu
akimla Saleh Ally, kuna Watanzania wengi wanajua, wanaelewa nao watapambana
kuhakikisha maendeleo yanapatikana na si ujanjaujanja tu. Nasisitiza,
hatuhitaji hadithi, tunahitaji maendeleo, ikishindikana, kaka Malinzi kaa
kando!








hapo umeongea kaka
ReplyDelete