Na Mwandishi Wetu
MECHI ya Agosti 23, yaani Jumamosi ijayo
imekuwa ikizidi kupata umaarufu zaidi hasa baada ya waratibu wa ziara hiyo
kuamua kuteua kikosi cha wachezaji nyota wakongwe wa Tanzania.
Kikosi cha nyota wakongwe wa Tanzania kitakuwa
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kuwavaa nyota wakongwe wa Real
Madrid.
Awali kulikuwa na taarifa kwamba waliamua
kutumia kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kuwavaa wakongwe hao wa Real
Madrid, lakini taarifa zilibadilika na sasa ni zamu ya wakongwe wa Tanzania.
Kampuni ya Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN),
ambao ni waratibu, imepongezwa zaidi kwa wazo hilo la pili la kuwatumia
wakongwe wa Tanzania.
Baadhi ya wakongwe waliotajwa kuunda kikosi hicho
ni Mohammed Mwameja, Manyika Peter, Salum Sued, Shadrack Nsajigwa, Boniface
Pawasa, George Masatu, Shabani Ramadhani, John Mwansasu, Salvatory Edward,
Sabri Ramadhani ‘China’, Mao Mkami na Abubakar Kombo.
Wengine ni Malota Soma, Abubakari Kombo, Clement
Kahabuka, Habib Kondo, Mtwa Kihwelo, Steven Nyenge, Dua Said na Edibily Jonas
Lunyamila.
Wazo la kuteua wakongwe wenzao limekuwa
kivutio zaidi na huenda ikawa ni kipimo cha wachezaji wetu, soka yetu na soka
lao ambao wamecheza katika kiwango cha juu.
Katika listi iliyotolewa inaonyesha kuwa kuna
wachezaji wenye rekodi za juu kabisa ikiwa ni pamoja na kubeba mataji ya Ulaya
kwa ngazi za klabu na taifa lakini wako waliocheza kwenye Kombe la Dunia na
wengine kulitwaa kama ilivyo kwa Zinedine Zidane.
Waliotajwa kuwa watakuja nchini ni Ruben de
Lared, Michael Salgado, Luis Figo, Cristian Karembeu, Michael Owen, Steve
McManamann, Zinedine Zidane na wengine ambao Watanzania wangependa kuwaona
wakionyeshana kazi na nyota wa Tanzania.
Kwa kikosi hicho cha wakongwe dhidi ya
wakongwe wa Madrid, kutakuwa na mambo mengi ya kuvutia, mfano Luis Figo, mmoja
wa mawinga wenye kasi raia wa Ureno atakapokuwa akionyeshana kazi na Shadrack
Nsajigwa au Abubakari Kombo.
Au winga mwenye kasi wa Tanzania, Akida
Makunda ambaye pamoja na kuwa na umri mkubwa lakini bado ameendelea kuwa na
kasi ya juu, atakuwa akipambana na Michel Salgado.
Burudani zitakuwa nyingi na kama Zidane
atakuwa miongoni mwao, katikati pale upande wa nyota wa Tanzania kuna watu kama
Sabri Ramadhani ‘China’, Mao Mkami ‘Ball Dancer’.
Katikati mtu kama Mwansasu na Pawasa wanaweza
kazi, ingawa mashabiki wamekuwa wakiomba kuongezwa kwa beki ngangari, Bakari
Malima ‘Jembe Ulaya’.
Mbele Tanzania itakuwa inasukuma mashambulizi
na watu kama Malota Soma ‘Ball Juggler’, Dua Said na Clement Kahabuka ambaye
uwezo wake wa kufunga bado uko juu sana.
Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa waandaaji ni
kuwaandaa wakongwe hao wa Tanzania kwa kuwapa maandalizi mazuri na ya kiwango
cha juu.
Lakini wakongwe hao pia wanapaswa kujituma na
kujiweka sawa kwa ajili ya mechi hiyo kwa kuwa hawapaswi kuamini mechi itakuwa
rahisi hata kidogo.
Mechi itakuwa ngumu kwa kuwa kwa utaratibu,
timu hiyo ya wakongwe wa Real Madrid inatambulika na uongozi wa klabu hiyo.
Inatunzwa na iko kwenye hesabu za klabu,
wamekuwa wakifanya mazoezi mara mbili kwa wiki, tena kwenye vifaa vinavyotumiwa
na ile timu kubwa iliyo na akina Cristiano Ronaldo, Gareth Bale na wengine.
Kama unakumbuka, Championi ndiyo lilikuwa
gazeti la kwanza kuandika kuhusiana na ujio wa Real Madrid, huenda watu
wakadhani ni utani au ‘changa’ kama ambavyo wamekuwa wakiona kwingine.
Lakini sasa yanatimia na aliyelihakikishia
Championi mapema kwamba kweli timu hiyo inakuja alikuwa ni Rayco Garcia,
mchezaji wa zamani wa timu ya vijana ya Barcelona na baadaye Real Madrid.
Garcia alilihakikishia Championi kuwa wakongwe
hao wa Madrid wako fiti na wanacheza soka katika kiwango cha uhakika kwa kuwa
wana programu ya uhakika kabisa ya mazoezi.
Alionya soka la vurugu, kwamba kama ni soka
sawa, lakini si ‘kurukiana’. Lakini akasisitiza kwamba soka watakaloonyesha
litakuwa funzo kwa timu yoyote, ndiyo maana walikuwa tayari hata kucheza na
Taifa Stars.
Hivyo wakongwe wa Tanzania wajiandae kweli, la
sivyo wataangukia kwenye aibu ya kufungwa mabao matano, sita au saba, kitu
ambacho kitaharibu burudani wanayotaka kuiona Watanzania.
lini itakuwa live hiyo mechi
ReplyDelete