Kocha Mkuu wa Simba, Mcroatia, Zdravko
Logarusic, amemkaribisha nyota mpya wa timu hiyo, Mrundi, Pierre Kwizera na
kumkabidhi kazi tatu maalum kikosini.
Baada ya kutua nchini, moja kwa moja
nyota huyo jioni alitinga mazoezini katika Uwanja wa Ununio Boko ambapo
alikutana na Logarusic na kumpatia kazi hizo.
Loga alimtaka Kwizera kufanya mambo
matatu makuu; moja, kuhakikisha anakuwa miongoni mwa wachezaji tegemeo katika
kikosi cha Simba msimu ujao kama mchezaji wa kimataifa. Pili, kuhakikisha Simba
inatwaa mataji mbalimbali likiwemo lile la Ligi Kuu Bara na tatu ni kuhakikisha
anaisaidia klabu kujiingizia kipato kikubwa kupitia miguu yake.
Kuhusiana na hilo, Logarusic maarufu
kama Loga, alisema kuwa kufanya vema kwa Kwizera kutatoa hamasa kwa mashabiki
kujitokeza kwa wingi viwanjani kuishuhudia timu yao, lakini pia mauzo ya jezi
na vifaa mbalimbai vya jina la Kwizera na Simba kwa jumla vitanunuliwa kwa
wingi.
“Karibu Simba, licha ya kukaribia
lakini kuna mambo muhimu ya kuzingatia kama kweli umekuja kwa nia ya kuitumikia
timu hii. Hakikisha unafanya kazi kama mchezaji wa kimataifa, uwe kioo kwa wachezaji
uliowakuta hapa.
“Hujaja hapa kwa maslahi ya hela, bali
wewe ndiye unategemewa kuhakikisha Simba inapata hela, maana timu yetu haina
hela. Kwa hiyo hilo ni miongoni mwa majukumu yako unapokaribishwa Msimbazi,”
alisema Loga.
0 COMMENTS:
Post a Comment