Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema
hawana nia ya kulumbana na Yanga kama inavyochukuliwa.
Hans Poppe amesema Simba ina nia ya kulinda kipaji cha mshambuliaji
Emmanuel Okwi na wala si malumbano dhidi ya Yanga, waeleweke.
“Yanga imeomba kuvunja mkataba na Okwi, naye amekubaliana na hilo,
lakini kila upande Yanga na Okwi wamefunguliana kesi, kila mmoja anamdai
mwenzake.
“Wakati hilo linaendelea, Okwi ameomba kucheza kwetu kwa ajili ya
kulinda kipaji chake. Sisi tumekubaliana na hilo na hatujampa hata fedha za
usajili.
“Kesi ya Yanga na Okwi si yetu, sisi tumemchukua Okwi kulinda kipaji
chake. Sasa kama Okwi atashindwa kwenye mashitaka waliyofungua Yanga wakitaka
kulipwa pamoja nay eye afungiwe, hilo ni suala jingine.
“Mfano mzuri ni pale wakati Simba inaidai Etoile du Sahel, Okwi akaja
Yanga na kuendelea kucheza. Sasa sioni sababu kubwa ya malumbano,” alisisitiza
Hans Poppe.
Okwi amejiunga na Simba wakati Yanga ikisistiza ni mchezaji wake na
haijavunja mkataba.
Imesisitiza ni mchezaji wake na ina matatizo naye hivyo imesisitiza TFF
kumpa adhabu yeye pamoja na Simba kwa kuingia mkataba juu ya mkataba ambao
haujavunjwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment