UKITUA katika Mkoa wa
Shinyanga, hususan maeneo ya stendi ya zamani ya mabasi ya mikoani na wilayani,
utakutana na shamrashamra za makonda, madereva na wapiga debe ambao wanaendelea
na shughuli zao za kujipatia riziki.
Lakini hao makonda, wapiga
debe, mawakala na madereva, ndiyo chachu na mafanikio ya Stand United, kwani
wao ndiyo waanzilishi na wamechangia kwa kiasi kikubwa kuifanya timu hiyo ifike
hapo ilipo tangu ilipoanzishwa mwaka 2012.
Stand inaongozwa na viongozi wenye uchungu na mpira na uchu
wa mafanikio katika soka, ndiyo maana wamefanikiwa kwa kiasi fulani.
Wanaendesha timu huku
wakiendelea na majukumu yao ya kila siku na kazi zao, ingawa wanahakikisha kila
kitu kinakuwa kinaenda sawa kabisa bila tatizo katika mabasi wengine maduka
yanayozunguka eneo hilo la stendi.
Unapofika Stand, unakutana
na makamu mwenyekiti wa timu hiyo, Masumbuko Charles ambaye ni mmoja wa mawakala
wa basi la Loquman ambalo linafanya kazi ya kusafirisha abiria kutoka wilaya za
Meatu na Bariadi hadi mkoani Dodoma.
Licha ya Masumbuko kuwa na
majukumu mengi, timu inapofanya mazoezi huwezi kumkosa.
“Uwepo wangu katika timu
hii ni furaha kwa sababu ilikuwa ndoto yetu hapa tangu muda na imefanikiwa
kutimia kwa kiasi mpaka hapa tulipofika, tutapigana kwa sababu mwanzo tulikuwa
tunasumbuliwa na ukata lakini tumetimiza ndoto kwa kiasi,” anaeleza Masumbuko.
Rashid Daghesh ambaye ni kocha
wa kwanza wa Stand kwa sasa ni mjumbe wa kamati kuu ya timu hiyo huku aliyekuwa
msaidizi wake Aman Vincent akiwa ndiye mwenyekiti wa timu kwa sasa.
Rashid, pamoja na majukumu
ya timu aliyonayo, pia ni wakala wa mabasi ya Ruska ambayo yanafanya shughuli
zake mkoani humohumo.
“Kitu ambacho naweza
kujivunia Stand United ni pamoja na kuifanya timu kuwa hapa ilipofika sasa, kwa
sababu zamani wakati nacheza timu yangu haikuwa na bahati ya kufika ligi kuu,
sasa imepiga hatua, ni jambo la kheri,” anasema Rashid.
Mohamed Ally Hemed ‘Dulla’ yeye ni mmoja wa wadau walioanza
kuisapoti timu tangu inaanza, akiwa ni mfanyakazi wa hapo na anamiliki basi la Bedui
Ruska ambalo ameamua kuweka jina kubwa la timu katika basi hilo.
“Naipenda sana timu hii
popote iendapo huwa naisapoti kwa kiasi kikubwa tangu tumeanza kuichangia Sh 500
kipindi hicho,” anaeleza.
Araf Nassor akiwa ni Mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Stand United naye ni wakala wa mabasi ya Ruska lakini
akiwa pia ni mmoja wa waasisi wa timu.
“Timu imepiga hatua kwa
kiasi kikubwa lakini napenda kuwaambia Watanzania kuwa, Stand United si timu ya
wahuni, wala wafanya fujo, sisi ni watu wa malengo, ndiyo maana tumefika hapa,
japo ukata kwa sana lakini tunapigana kuendesha timu,” anasema Nassor.
Je, mashabiki wanaisapoti vipi
timu?
“Timu ilipokuwa ikienda
mikoani, kipindi hicho walikuwa wanagharamiwa na timu kwa kupitisha mabakuli na
kuchangisha na hawa mashabiki wetu wapo katika makundi mawili, Full Shangwe
ambao muda wote wanaishangilia timu pamoja na Babu Kubwa, wote hawa ni mashabiki
wa timu yetu.
“Pia kwa sasa baada ya
kupanda, mtashuhudia Bendi ya Stand ikitoa burudani katika michezo yake tofauti
wakati ligi kuu itakapokuwa ikiendelea,” anafafanua Nassor.
Hao ni baadhi ya wadau na
viongozi wa Stand United ambao wamekuwa na timu tangu inaanza mpaka hapo
ilipofikia, ingawa haikuwa kazi rahisi kufika hapo walipofika.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment