KAMA kungekuwa na tuzo ya mdhamini bora wa Ligi Kuu Bara, basi
moja kwa moja ingekwenda kwa kampuni ya kuuza matairi na betri za magari ya Bin
Slum Tyres Limited ya jijini Dar es Salaam.
Sina uhakika kama Bin Slum ana matawi nje ya Jiji la Dar es
Salaam, lakini kampuni hiyo imefanya mambo ambayo sasa ndiyo inapaswa kuwa njia
sahihi kwa kampuni nyingine.
Nazungumzia kwenye soka, nasema Bin Slum ingeweza kupewa tuzo
kutokana na uamuzi wake wa kishujaa, uamuzi wa kijasiri ambao unaonyesha
ulilenga kusaidia hata kuliko faida.
Kampuni ipi ya kibiashara ambayo itafanya mchezo na suala
linaloitwa faida? Lakini Bin Slum Ltd ni kampuni ambayo imejaribu baada ya
kuamua kutoa udhamini kwa timu tatu za Ligi Kuu Bara.
Kwanza ni Mbeya City ambayo wameidhamini kupitia bidhaa za betri
zake bora za RB na kumwaga zaidi ya Sh milioni 300 katika kipindi cha miaka
mitatu, utakubaliana nami kwamba si jambo dogo.
Baada ya hapo, kampuni hiyo ikaamua kutoa udhamini mwingine kwa
kampuni ya Stand United ya Shinyanga. Hapa ndiyo ujasiri unapoianzia, kwamba
imekubali kuidhamini timu ambayo ndiyo imepanda tu daraja.
Kampuni ya Bin Slum haitokei Shinyanga, lakini imekubali kutoa
udhamini wa vifaa pamoja na Sh milioni 50, lakini imechangia kwenye manunuzi ya
basi la timu hiyo pia.
Kupitia matairi yake ya Double Star, Bin Slum imekuwa mdhamini wa
Stand United ambayo ndiyo imepanda tu daraja. Hili ni jambo jema kwenye soka
nchini.
Kama hiyo haitoshi, Bin Slum imeendelea kusambaa kwa kufunga
safari hadi mkoani Mtwara na kuidhamini Ndanda FC kupitia matairi yake ya Vee
Rubber. Hii ni timu pia iliyopanda daraja.
Utakumbuka timu chache za Ligi Kuu Bara zina wadhamini, lakini
utaona timu zenye udhamini ni kubwa zenye majina kama Yanga au Simba. Kidogo
Azam FC kwa kuwa msimu uliopita wamekuwa mabingwa.
Timu nyingine zimekuwa na mdhamini mmoja au hakuna kabisa. Jambo
ambalo linatokana na kampuni nyingi kuingia woga kutokana na mambo mawili
makubwa yanayojitokeza sana kwenye mchezo wa soka.
Kwanza, hofu ya kufanya kazi ya watu wasiokuwa na mpangilio wa
mambo. Pili, kuamini kwa timu za ligi kuu ukiacha Yanga, Simba na Azam FC,
nyingine ni vigumu sana kujitangaza.
Bin Slum hawakujali hilo, wameonyesha ujasiri na ndiyo maana
kampuni nyingine zimeanza kujitokeza kuzidhamini Ndanda na Stand United kwa
kuwa zinaona kumbe inawezekana kama ilivyofanya kampuni hiyo ya kuuza matairi.
Wapo wanaoweza kuona vibaya au haya kuipongeza kampuni hiyo ya Bin
Slum. Lakini ukweli ni kwamba wanastahili pongezi ya kuwa chachu ya wengine
kuona kuwa soka inaweza kuzitangaza bidhaa nyingi. Tumeona Benki ya Exim
imeanza kuiunga mkono Bin Slum kwa kuidhamini Stand, wengine wajitokeze pia.
Lakini bado, wakati Bin Slum inakuwa mfano, inaweza kuzishawishi
kampuni nyingine kuachana na kuamini Yanga na Simba tu, basi wanaodhaminiwa nao
wafanye mambo yao kwa mpangilio.
Mfano kuvaa nguo za wadhamini kwa wakati unaotakiwa na kutekeleza
mambo yaliyo kwenye mkataba ili kuondoa usumbufu kwa wadhamini ambao unaweza
kuwakatisha tamaa na mwisho kuamini soka si sehemu sahihi kuingiza fedha zao.
0 COMMENTS:
Post a Comment