September 29, 2014


Na Saleh Ally
INAPOTOKEA timu ikapoteza michezo au kupata sare mfululizo, huwa kuna mambo mengi sana yanayojitokeza.


Hali hiyo imeikamata Simba ambayo imetumia dakika zake 180 za mwanzo za Ligi Kuu Bara kuchuma pointi mbili tu.

Hali hiyo inaonyesha kuzichanganya pande tatu kuu za Simba, kwanza viongozi, pili benchi la ufundi na tatu ni wachezaji. Kwamba nini kinaendelea?

Kibaya zaidi, Simba imeanza kufunga katika mechi zake zote mbili za nyumbani, halafu wageni wakasawazisha na mwisho majibu ya dakika 90 yakawa ni sare.

Mechi ya kwanza dhidi ya Coastal Union, hadi mapumziko, Simba ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0. Kipindi cha pili, Wagosi wakasawazisha yote na kuanza kuwapa Simba wakati mgumu.

Mechi ya pili, Simba ikatangulia kufunga bao dhidi ya Polisi Morogoro, ikaenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao hilo. kipindi cha pili, wageni wakasawazisha na dakika 90 zikamalizika kwa 1-1.

Kuna michezo mingi ya kuangalia kama ishu itakuwa ni kwenda kitaalamu. Mtazamo wa wengi ni ushabiki zaidi, kitu ambacho si sahihi na hakiwezi kuwa msaada kwa Simba.

Huu ndiyo wakati ambao Simba wanatakiwa kutulia kuliko mwingine wowote na kujipanga. Huenda inaweza kuwa rahisi kwa mashabiki kuchanganyikiwa, lakini hali hiyo ikiingia kwa wachezaji na benchi la ufundi linaloongozwa na Patrick Phiri, maana yake wamejimaliza wenyewe.

Kikosi:
Hakuna ubishi kwa kiwango cha Ligi Kuu Bara, Simba ina kikosi kizuri tu ambacho kinahitaji mambo madogo kujiweka sawa.

Uwezo wa Phiri na wasaidizi wake, Selemani Matola, Iddi Pazi na meneja, Nico Nyagawa unajulikana na wala si kitu cha kubabaisha.

Wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza na benchi lake, si wachezaji wa kubahatisha lakini ni lazima wawe na malengo na kukubali kwamba wana kibarua cha kuipa Simba matokeo mazuri na wala si hadithi.

Lazima wajue Simba ina mashabiki wengi wanaoelewa mpira, lakini itafikia wakati watachoka na mambo yatabadilika.

Nafasi:
Hili ndilo tatizo namba moja la Simba katika mechi mbili walizocheza. Mechi ya kwanza dhidi ya Coastal, Simba walipata nafasi nane nzuri za kufunga, wakafunga mabao mawili.

Mechi dhidi ya Polisi Moro, Simba walipata nafasi sita za kufunga, wakaitumia moja peke yake, tena kwa uwezo binafsi wa Emmanuel Okwi.

Iwapo Simba ingekuwa inazitumia nafasi zake vizuri, hakika ingekuwa ndiyo timu inayoongoza kwa mabao mengi.

Si rahisi timu kufunga katika kila nafasi inayoipata lakini uwiano wa ubora wa safu bora ya ushambuliaji huanzia 50% ya utumiaji nafasi kupanda juu. Kwa sasa, Simba wako chini ya 40% ya matumizi mazuri ya nafasi za kufunga wanazozipata.

Kwenye hili Phiri lazima alitupie macho kwa ukaribu sana, la sivyo, vijana wake watamuangusha, mwisho itakuwa Simba ‘gonga-gonga’ pasi, bila mabao.


Kipindi cha pili:
Katika dakika 90 za kipindi cha pili (dakika 45 za Coastal na 45 za Polisi Moro), Simba haijafunga hata bao moja.

Phiri ana kila sababu ya kuitengeneza timu ambayo ina uwezo wa kufunga kwa vipindi viwili. Simba yake ni ile yenye nguvu kipindi cha kwanza tu, dakika 45 za pili, inapotea njia.

Mabeki:
Umakini wao uko juu sana kwa asilimia mia katika kipindi cha kwanza kwa kuwa kila dakika 45 katika mechi zote mbili hawajaruhusu bao.

Dakika 45 mara mbili katika mechi mbili, wameruhusu mabao matatu. Wakifungwa mawili na Coastal na moja dhidi ya Polisi.

Hakuna nidhamu ya kutosha kwenye safu ya ulinzi na hili litaendelea kuwaumiza Simba kama hawatalifanyia kazi mapema.

Kocha anaweza kuwa na la kulifanyia kazi, ila wachezaji wenye akili zao timamu wanapaswa kujitathmini.

Mfano, dakika hizo kuongeza umakini wa kuepusha faulo mbele ya lango kama walichokifanya Simba katika mechi ya Coastal, Rama Salim, akafunga bao la kusawazisha.

Kutengeneza ukuta wa uhakika, ambao unahakikisha mpira hauchezwi nyuma na mfano mzuri angalia ulinzi wa Polisi Moro katika mechi dhidi ya Simba, ulikuwa bora mara 200 kuzidi ule wa Simba.

Hakuna mchawi, si sahihi kusema Simba ina kikosi kibaya lakini makosa madogo kama hayo ndiyo yanayowaangusha na wakati mwingine vizuri mchezaji ayaone na kuyafanyia kazi na si kusubiri kocha aseme.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic