NAAMINI
utakuwa umepata taarifa kuhusiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutaka
kupewa asilimia 5 kutoka kwenye fedha ambazo klabu 14 za Ligi Kuu Bara zinapata
kutoka kwa wadhamini!
Nilizipata taarifa hizi
wiki iliyopita, lakini ilikuwa ni vigumu sana kwangu kuamini kama kweli TFF
inaweza ikafanya uamuzi huo.
Nikafanya kazi ya ziata
kupata uhakika, ushahidi kuhusiana na suala hilo kama kweli TFF inaweza
ikafanya kitendo hicho ambacho kinaweza kuwa sawa na dhuluma.
Uhakika niliupata siku tatu
zilizopita kuwa kweli TFF inataka klabu zikatwe asilimia tano kutoka fedha
wanazipata kutoka Azam TV na asilimia tano tena kutoka fedha za Vodacom.
Halafu fedha hizo zipelekwe
kwenye fungu la maendeleo ya michezo ambalo linatumiwa nashirikisho hilo!
Hili kwangu ni geni, lakini
sitaki kusita wala kupindisha mambo, naliita ni dhuluma na kama viongozi wa
klabu watakaa kimya, itakuwa ni maajabu ya karne.
TFF wanataka fedha za
klabu, kwamba zichukuliwe na kuingizwa kwenye maendeleo ya soka. Bado usisahau
klabu zinakatwa mapato kwenye kila mechi na kuna fedha hizo zinakwenda kwenye
mfuko huo.
Kama zitakatwa fedha, maana
yake ni mara mbili na kwanini TFF iamua kufanya hivyo huku ikijua klabu sasa
ndiyo zimeanza kupata ahueni.
TFF inataka izikate klabu
fedha ziende kwenye maendeleo ya soka na zaidi kwake huzitumia katika timu za
taifa.
Kama utazungumzia udhamini,
Taifa Stars ina wadhamini wakubwa tu Kilimanjaro ambao wamekuwa wakitoa kila
kitu kwa timu hiyo.
Wakati mwingine nilianza
kufikiria huenda TFF imeishiwa fedha kutokana na ile kambi ya Taifa Stars
maboresho ambayo sasa haijulikani ilipo wala faida yake ni ipi!
Au pia najiuliza, huenda
hao ndiyo wale washauri wa Rais wa TFF, Jamal Malinzi wako kazini na wameibuka
na wazo jipya na kuisaidia TFF kujipatia fedha.
Klabu ndiyo zikatwe fedha
ziende kwenye shirikisho, badala ya shirikisho ambalo linachuma fedha kutoka
kwenye klabu lizisaidie kupata ahueni ya uendeshaji.
Lazima kuwe na uungwana au
huruma, kwamba klabu zinahitaji lundo la fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi
26 kwa msimu.
Kambi, kulipa mishahara na
uendeshaji wa timu kwa ujumla si jambo dogo. Kuna timu zinatumia hadi zaidi ya
Sh milioni 80 kwa mwezi.
Mfano kwa timu za Yanga na
Simba ambazo hazina viwanja vyake, ukiweka gharama ya viwanja kwa mwezi,
mishahara, posho na uendeshaji, kufikia Sh milioni 100 wala si ishu kubwa.
Hapo ndiyo uungwana wa TFF
kama mzazi au kiongozi wa mpira nchini unatakiwa kufanya kazi na si wao tena
kuzidi kuzinyonya klabu.
Tayari suala hilo limetoka
TFF na kufikishwa kwenye uongozi wa juu wa bodi ya ligi. Nafikiri TFF inapaswa
kulipitia hilo upya na kuahirisha inachotaka kukifanya.
Wadhamini wanafaidika
kujitangaza kupitia hizo klabu na wala hawajitangazi kupitia TFF wala timu za
taifa. Hivyo ziacheni klabu zifaidike na udhamini huo ‘mduchu’ si kuanza
kuzipunguzia tena na kutaka kuzinyonya.
Fedha za Fifa ambazo mnapewa kila mwaka dola 250,000,
ukijumlisha zile za udhamini na zile wanazokatwa klabu kupitia mfuko huo wa
maendeleo zinawatosha.
Sasa mfanye juhudi za
kutafuta wadhamini wa timu za wanawake na zile ambazo hazina udhamini. Tumieni
nguvu yenu kubwa kwenye ubunifu wa nini cha kufanya na si kulahisisha tu mambo
na kutaka kutumia nguvu kuzinyonya klabu.
Saleh Chatu huyoooo,mkimbie!
ReplyDelete