September 24, 2014

OMOG (KULIA) AKIWA NA MSAIDIZI WAKE, KALLY ONGALA RAIA WA UINGEREZA.

Kocha Mkuu wa Azam, Mcameroon, Joseph Omog, ameibuka na kuweka bayana sababu tatu ambazo zinaweza kuwagharimu katika harakati za kutetea ubingwa wao huku wakiushuhudia ukienda Jangwani au Msimbazi.


Pamoja na Azam kuanza ligi kwa kishindo cha mabao 3-1 dhidi ya Polisi Moro, lakini Omog amesema hakuridhishwa na kiwango chao, huku akibainisha makosa matatu ya msingi ambayo yanaweza kuwagharimu baadaye iwapo hayatafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

Mcameroon huyo alitaja makosa hayo kuwa ni ukosefu wa umakini katika safu ya ushambuliaji, mawasiliano hafifu kwenye safu ya ulinzi pamoja na wachezaji kuridhika mapema na matokeo ama kiwango chao. 
Alikwenda mbali na kusema kasoro hizo ndizo ziliwagharimu kwenye mchezo na Yanga, ambao walilala kwa mabao 3-0 kabla ya kujirudia kwenye mchezo na Polisi, japo walipata ushindi huo.

“Nashukuru tumeanza vizuri msimu, lakini siwezi kukisifia sana kikosi maana kilikuwa na udhaifu mkubwa, ambao unaweza kutusababishia matatizo mbeleni.
“Kuna tatizo la wachezaji ‘ku-relax’ kwa kuridhika na matokeo hasa dakika za mwisho, wanasahau mpira unaweza kubadilika muda wowote. Safu za nyuma na mbele kuna upungufu mkubwa, hakuna mawasiliano mazuri katika safu ya ulinzi, wamekuwa wakiruhusu mashambulizi yasiyo ya msingi kama ilivyo safu ya mbele ambayo bado haina umakini katika umaliziaji.

“Kama wangekuwa makini tungepata mabao mengi sana. Kiukweli bado tuna kazi kubwa ya kuondoa kasoro hizi, vinginevyo ubingwa utakwenda Simba au Yanga, ingawa tunapambana sana kuubakiza,” alifunguka Mcameroon huyo.
Azam inajipanga kukutana na maafande wengine wa Ruvu Shooting katika mchezo utakaopigwa Jumamosi wiki hii.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic