WIKI ILIYOPITA, mashabiki kadhaa wa Coastal
Union walishikiliwa katika kituo kimoja cha polisi mjini kwa madai walikuwa
wanauza jezi za Coastal Union za msimu uliopita ambazo zilikuwa zina nembo ya
mdhamini ajulikanaye kama Sound.
Sound ni nembo iliyokuwa inatumika wakati
kampuni ya Bin Slum Tyres Ltd ikiidhamini Costal Union msimu uliopita. Msimu
huu Wagosi wa Kaya wanadhaminiwa na bidhaa ya Pembe.
Pamoja na kukamatwa, ikaelezwa uongozi wa
Coastal Union ndiyo ulishitaki, mashabiki hao walikana kuuza jezi hizo. Lakini
kukazuka hali ya kutoelewana kati ya mashabiki hao na uongozi baada ya viongozi
kuwataka kutoingia uwanjani kuishangilia Coastal Union wakiwa wamevaa jezi
hizo.
Vijana hao wakaweka msisitizo kwamba hawakuona
kama kuna tatizo lolote kuhusiana na wao kuvaa jezi za Coastal Union bila ya
kujali zina nembo ya mdhamini yupi.
Walisema zina nembo ya Coastal Union, hivyo
wakakataa kutekeleza agizo hilo na kuingia uwanjani wakiwa wamezivaa,
wakaishangilia Coastal Union kwa nguvu na mwisho ikashinda kwa mabao 2-1 dhidi
ya Ndanda FC.
Uongozi wa Coastal Union haukutoa ushirikiano
mzuri kwa gazeti hili, lakini baadaye lilifanikiwa kumpata Nassor Bin Slum,
mmiliki wa Kampuni ya Bin Slum Tyres Ltd ambaye alikiri kuzisikia taarifa hizo
za mashabiki wa Coastal Union kupelekwa kituoni, kisa walivaa jezi hizo na
kusema anaamini haikuwa sahihi na si haki kuwafanyia hivyo mashabiki hao.
“Mimi nahoji kuna tatizo gani mashabiki wa
Coastal Union kuvaa jezi za mdhamini wao wa zamani, tena wanaingia uwanjani
kwenda kuishangilia timu yao, kuipa nguvu ishinde?” alihoji Bin Slum.
“Nauliza mfano, mwakani kama Coastal Union
itapata mdhamini mwingine, halafu mashabiki wakavaa jezi zenye nembo ya Pembe
ambaye ni mdhamini wa msimu huu, watakamatwa?”
“Kuna kitu cha kulifanyia kazi suala hili ili
liende kiungwana, pia kuangalia umuhimu wa kuwa na Coastal Union moja badala ya
kugombana na kutengana kwa sababu ya matakwa ya mtu au watu wachache.
“Coastal Union ni timu ya watu, tena watu
wengi. Hivyo ni vizuri watu kuangalia nini watu wanataka na si mtu mmoja au
wawili wanataka nini,” alisisitiza Bin Slum.
“Viongozi si weledi pia, ndiyo maana mimi
niliwakimbia, utaona hapa kuna tatizo. Nilifikiri ilikuwa ni vizuri kupambana
na wale wanaouza jezi feki mitaani.
“Vipi unampangia shabiki avae nini, angalia
hata wale wa Manchester United wanavaa jezi za wadhamini waliopita kama AIG au
za wadhamini wa zamani zaidi.
“Kama kweli wanataka watu wavae jezi nyingi za
mdhamini wa sasa kumfurahisha kuna vitu vya kufanya.
“Waandae utaratibu mzuri wa kupatikana jezi
hizo, zipatikane kwa wingi na ikiwezekana kwa bei rahisi watu wengi wavae wakiingia
uwanjani.
“Mimi nasikia jezi mia mbili tu ndiyo
zimeletwa, sasa uwanjani pale wanaingia mashabiki wangapi? Halafu unakasirika
watu wasivae jezi za Sound!
“Hii inashangaza kidogo, kingine lazima wajue
jezi wanazovaa ni za Coastal, si Sound au Bin Slum. Jezi wanazovaa ni za
Coastal Union, ndiyo maana zina nembo ya klabu.
“Ingekuwa ni jezi ya Bin Slum pekee,
isingekuwa na nembo ya Coastal Union, ungeweza kusema jambo, lakini bado
utamzuia vipi mtu kuingia uwanjani na nguo au jezi anayoitaka? Vipi hawazuii
jezi za Arsenal, Manchester United na nyingine kuvaliwa uwanjani, halafu
wanazuia jezi yenye nembo ya klabu yao? Hakika wanapaswa kuipa heshima nembo ya
klabu yao.
“Wakati wa jezi zenye nembo ya Sound, kulikuwa
na utaratibu mzuri wa upatikanaji, bei ilikuwa chini. Sasa wanaweza kuiga
utaratibu huo mzuri na wakati mwingine wakiweza wagawe bure angalau jezi
kadhaa,” alisema.
Pamoja na Bin Slum, shabiki mwingine wa
Coastal Union aliyejitambulisha kwa jina la Abdulatif Famau, alipiga simu
kwenye ofisi za gazeti hili na kueleza kuwa analaani kitendo hicho cha uongozi.
“Mwisho polisi walilazimika kuwaachia wenzetu
waliowashikilia na kusema hakuna kesi. Jiulize nani anaweza kushitakiwa kwa
kuchagua avae jezi ipi?
“Halafu ile si jezi ya Sound au Bin Slum, ni
jezi ya Coastal Union, ina nembo na inatambulika kabisa kwa kuwa imetumika
msimu uliopita tu.
“Ajabu hata tukitaka jezi ya msimu huu, leo
hii hazitapatikana. Sasa tatizo ni lipi? waulize viongozi wadhamini wameingia
mkataba na klabu au sisi mashabiki. Nafikiri vizuri tufanye mambo ya kuisaidia
klabu na timu yetu na si kuangalia maslahi binafsi,” anasema Famau, akionyesha
kujiamini.








0 COMMENTS:
Post a Comment