October 8, 2014


Wakati homa ya mechi ya Ligi Kuu Bara itakayozikutanisha klabu kongwe za soka hapa za Simba na Yanga ikizidi kupanda, uongozi wa Simba unadaiwa kumficha mshambuliaji wake wa kimataifa kutoka Burundi, Amissi Tambwe.


Taarifa zinasema kuwa, Simba wameanza kuhofia hujuma kutoka kwa wapinzani wao, hivyo wameamua kumhamishia hotelini.

Simba na Yanga zinatarajiwa kupambana Oktoba 18, mwaka huu katika mchezo wa ligi kuu utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba ambazo gazeti hili limezipata zimedai Simba hivi sasa imemficha Tambwe katika hoteli moja iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kumtoa katika nyumba aliyokuwa akiisha hapo awali maeneo ya Sinza Kwaremi.

Nyumba hiyo kwa sasa wanaishi wachezaji wa kikosi cha vijana cha timu hiyo.
Hatua hiyo ya uongozi huo kufanya hivyo ni kutokana na kuhofia kuwa Yanga ingeweza kutumia mwanya huo na kumrubuni.

“Pamoja na kuwa katika hoteli hiyo, pia yupo chini ya ulinzi mkali kutoka kwa viongozi wanamfuatilia kwa karibu muda wote.

“Unajua hapo awali Tambwe alikuwa akihusishwa kutaka kwenda Yanga, hivyo inawezekana hiyo ndiyo sababu kubwa inayowafanya viongozi hao kuwa na hofu hiyo,” kisema chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, kiliongeza: “Pamoja na Tambwe hivi sasa kuishi hotelini hapo bado viongozi wa Simba hawana imani ya kutosha.”

Katika hatua nyingine, chanzo hicho kilipoulizwa kama uongozi huo pia una mpango wa kumficha mshambuliaji mwingine wa timu hiyo, Emmanuel Okwi ili naye asirubuniwe na Yanga kilisema:

 “Suala hilo kwa Okwi halipo kwa sababu kila mtu anajua uhusiano wa sasa wa Yanga na mchezaji huyo ukoje, hivyo itakuwa ni vigumu kurubuniwa.”


Msimu uliopita, Tambwe ndiye aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufunga mabao 19 lakini msimu huu hadi sasa amepachika bao moja tu katika mechi tatu.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic