Ishu ya kipa
wa Yanga, Juma Kaseja na klabu yake limechukua sura mpya baada ya uongozi wa
Yanga kutoa kauli kali juu ya aliyejitambulisha kuwa ni meneja wa kipa huyo,
huku ikielezwa kuwa kipa huyo amepata ofa ya kucheza soka Uarabuni.
Meneja wa
Kaseja, mwanamichezo Abdulfatah Saleh ambaye amejitambulisha kuwa ni meneja wa
mchezaji huyo, amenukuliwa na vyombo vya habari likiwemo gazeti hili, akisema
kuwa Yanga imevunja mkataba na mteja wake kutokana na kukiuka masharti ya
mkataba.
Akijibu madai
hayo, Katibu Mkuu wa Yanga, Beno Njovu, amesema kuwa, kisheria wao hawamtambui
huyo anayejiita meneja wa Kaseja na hivyo hawawezi kutambua madai ya kuvunjwa
kwa mkataba kama inavyoelezwa.
Njovu alikataa
kujibu swali la mkataba huo kwa njia ya simu na kuomba atumiwe barua pepe,
alipoulizwa kupitia barua pepe, alijibu kwa kifupi kama ifuatavyo:
“Siwezi
kukujibu maana mchezaji Juma Kaseja hana meneja anayetambulika na taasisi
yoyote, iwe Yanga, TFF au hata Fifa.”
Kisha baada ya
hapo akaambatanisha na majina ya mawakala ambao wanatambulika Fifa, akiwataja
kuwa ni Ahmed Binkleb, John Ndumbaro, Mehdi Remtulla na Ally Saleh.
Wakati hayo
yakiendelea, Abdulfatah Saleh ameliambia gazeti hili kuwa Kaseja anaendelea
kupata ofa mbalimbali ikiwemo kutoka Dubai.
“Kaseja kubaki
Yanga baada ya mzunguko huu wa sasa ni mgumu kutokana na Yanga kukiuka masharti
ya mkataba kwa kushindwa kumalizia fedha za usajili zilizobaki, shilingi
milioni 20, ambazo zilitakiwa zilipwe kabla ya Januari 15, mwaka huu.
“Kuna klabu
mbili za Dubai lakini bado mazungumzo yanaendelea,” alisema Abdulfatah.
0 COMMENTS:
Post a Comment