KILA Ligi Kuu Bara inapoanza kupamba moto,
mashabiki wengi sana wa soka huelekeza masikio na macho yao upande huo, pia
inakuwa vigumu sana kuyabandua upande huo.
Siku zote Ligi Kuu Bara inakuwa na presha kubwa
kwa kuwa kila timu inataka ushindi na waliopoteza wanataka kuendeleza mambo
lakini kwa wale walioshinda wanataka kuendelea bila ya kufungwa.
Presha inakuwa kubwa zaidi kwa Yanga na Simba
kwa kuwa zina mashabiki wengi wanaoziunga mkono, mashabiki walalamishi na
wasiokuwa na subira. Hali hii inawafanya viongozi kuwa na presha kubwa.
Unapofikia wakati wa ligi hiyo, hakuna ubishi
kwamba uongozi unaelekeza nguvu zake nyingi upande huo ukitaka kupata mafanikio
na kuepukana na kelele hasi za mashabiki ambao wanataka kuona chanya kila
kukicha.
Si vibaya kuwa na uongozi unaotupia nguvu zake
katika moja ya mambo ya msingi na kuwafanya mashabiki kuona wako sahihi katika
uteuzi wao wakati wa uchaguzi. Pia si vibaya uongozi kukumbuka mashindano
lakini kutosahau umuhimu vitu vya maendeleo muhimu kwa klabu zao.
Si vibaya kuwasaidia makocha Marcio Maximo na
Patrick Phiri, lakini vitu muhimu kama uwanja, ni sahihi na muhimu zadi
kuhakikisha vinamilikiwa na klabu hizo kwa ajili ya maendeleo.
Utakumbuka klabu zote mbili za Yanga na Simba
zilianzisha mchakato wa viwanja vyao. Kila upande unamiliki uwanja, Yanga ukiwa
ni ule wa Kaunda ambao uko katikati ya jiji na Simba katika eneo la Boko, nje
kidogo ya Dar es Salaam.
Maandalizi ya kuhakikisha unafanyika ukarabati
au ujenzi tayari yalianza, lakini yamepotea ghafla na hakuna anayezungumzia
wala kulifanyia tena kazi jambo hilo ambalo ni muhimu sana kwa klabu hizo.
Simba na Yanga zinahitaji sana viwanja kwa kuwa
ndiyo pango la kazi zao. Kuuza bidhaa bila kuwa na sehemu ya kufanyia biashara
haiwezi kuwa sahihi na klabu hizo kongwe hazipaswi kwenda na mfumo wa biashara
za ‘kutembeza’.
Wenyeviti wanaoziongoza Yanga na Simba ni
vijana au kaka zetu wa enzi hizi. Yusuf Manji na Evans Aveva. Wote wametembea,
wafahamu wa mambo na hauwezi kusema kutakuwa na ugumu kwa wao kuleta
mabadiliko.
Kama Aveva na Manji itafikia siku wameondoka
Simba na Yanga, halafu wakaziacha klabu hizo kutokuwa hata na uwanja wa mazoezi
unaotambulika kwa ajili ya timu zao. Hakika litakuwa ni jambo la kushangaza na
linapaswa kuzungumzwa au kukemewa kwa miaka mingi.
Manji na Aveva lazima watupie nguvu zao kwenye
kuhakikisha hata kabla ya kuisha kwa msimu huu, basi Yanga na Simba zinakuwa na
viwanja vyao, angalau vya mazoezi tu.
Kuwa na viwanja ni kujikomboa, timu zote hizo
mbili zinauhitaji uwanja. Lakini timu zao za vijana pia zinahitaji viwanja. Si
kazi rahisi kukuza vijana bila ya kuwa na uwanja kwa ajili ya mazoezi.
Kama ni aibu ya kukosa uwanja imekuwa ni ya
muda mrefu sana. Kwa Simba ya Aveva na Yanga ya Manji, kuna kila sababu ya
klabu hizo kupata uwanja. Tayari zilianza mikakati na hakuna sababu ya
kuisimamisha na kubaki nguvu kwenye ligi.
Hata kuwa na kikosi bora, kupata uwanja ni
sehemu ya mikakati bora ya kuwa na kikosi imara kwenye ligi. Manji na Aveva
msiliweke kando suala la viwanja kwa kuwa umuhimu wake ni sawa na uti wa mgongo
wa klabu zenu.
Kitu kizuri zaidi ni suala linalowezekana na
klabu hizo zinazoongozwa na wenyeviti vijana zaidi ukilinganisha na wakati
mwingine uliopita, zina kila sababu ya kuwa Yanga na Simba mfano ukilinganisha
na zile zilizopita lakini changamoto kwa Yanga na Simba zinazokuja.
unajua nyinyi waandishi mnaboa sana, hivi kwenye uchaguzi wa Simba Aveva kama mgombea sela yake si mliipigia debe? Point tatu goli tatu, sasa huo uwanja unaouzungumzia ni upi alio ahidi Aveva? hapa kweli naamini njaa zinawasumbua waandishi wengi hapa Tanzania, hebu toa na lihabari lako linaboa
ReplyDelete