Na
Saleh Ally
UKITAJA
moja ya makocha bora kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, kamwe
hauwezi kumuacha Patrick Phiri, raia wa Zambia.
Ana
rekodi nzuri kwa upande wa klabu lakini timu ya taifa pia, amewahi kuivusha
Zambia kwenye Kombe la Mataifa Afrika ingawa hakufika mbali.
Kila
timu anayoifundisha hucheza soka la kuvutia na tayari hali hiyo imeanza
kujionyesha kwa Simba ingawa muda unatakiwa ili aweze kufanya mabadiliko
anayoyataka.
Wakati
ameanza mabadiliko, kuna jambo amekuwa akilifanya ambalo inawezekana ni hisia
za kibinadamu, kuamini au ushawishi lakini msingi wa hakuna binadamu
aliyekamilika unaweza kuwa mwongozo kwamba hata yeye anakosea pia.
Phiri
ameonekana kutomuamini kabisa mshambuliaji Amissi Tambwe raia wa Burundi na
kuamua kumuweka benchi. Mwenyewe amekuwa akisema atampa nafasi lakini anajaribu
kutengeneza mfumo tofauti.
Watu
wa karibu na Phiri wamekuwa wakisema Tambwe hawezi kuendana na kasi ya Phiri
katika kikosi chake, ndiyo maana sasa ameamua kumuweka benchi na kutumia vijana
wengine kama Elius Maguli.
Inawezekana
kabisa kuwa Phiri hamjui Tambwe na huenda amekuwa na haraka katika suala la
kuamua kuhusiana naye kwani Tambwe ana vigezo vyote vya kupata nafasi ya kwanza
kwenye timu yoyote ya Tanzania Bara.
Tambwe
ndiye mfungaji bora msimu uliopita akiwa amepachika mabao 19 katika mechi 24 za
ligi alizocheza, hali inayoonyesha ni mshambuliaji hatari anapokuwa mbele ya
lango la wapinzani.
Kusema
hawezi kuendana na mfumo, bado linakuwa ni jambo linalokosa uthibitisho kwa
kuwa katika mechi tatu za kirafiki alizoichezea Simba ikiwa kambini Zanzibar,
Tambwe alifunga bao moja.
Aliporejea
kwenye ligi, mechi tatu za mwanzo ambazo zote Simba ilitoka sare, Tambwe
alifunga bao moja akipiga kichwa krosi nzuri ya Okwi. Wastani wa bao moja kwa
mechi tatu, bado si mbaya.
Sasa
hapo ndiyo unaweza kujiuliza ni mfumo upi ambao unamshinda Tambwe kama amecheza
mechi sita za ligi na kirafiki na kufunga mabao mawili? Nani anauweza huo mfumo
na amefunga mabao mengi zaidi yake?
Kama
ni kweli Phiri ameona Tambwe hauwezi mfumo wake basi hakutulia na kumfuatilia
vizuri kwa kuwa Simba haichezi kasi ya kutisha kiasi kwamba Tambwe hataweza
kucheza.
Angalia
msimu uliopita, Tambwe alikuwa katika kikosi cha Simba kilichochoka, wachezaji
walikuwa wakidai mishahara na fedha zao za usajili, hali za kambi zao hazikuwa
nzuri na hakukuwa na watupia krosi safi kama Okwi, halafu akafunga mabao 19.
Jiulize
sasa ana watu kama Haruna Chanongo na Ramadhani Singano ‘Messi’ aliokuwa nao
msimu uliopita, ameongezewa Okwi na pia Paul Kiongera ingawa sasa ni majeruhi.
Kwa wachezaji hao wenye kasi na furuku, unafikiri Tambwe atashindwa kufunga
zaidi?
Ukisema
Tambwe ni mviziaji, kazi yake ni kufunga tu, eti hawezi kwenda na mabeki wawili
akaingia na kufunga, hilo ni tatizo la kutokuwa mchunguzi. Picha lukuki
zinaonyesha akikabwa na mabeki wawili au akikimbia nao ndani ya 18 kabla ya
kufunga.
Suala
la Tambwe lisiamuliwe kishabiki, inawezejana ni matakwa ya kocha au baadhi ya
viongozi wanaona Mrundi huyo si mzuri au hawafurahishi kwa aina yake ya
uchezaji kwa kuwa haina chenga na mbio nyingi. Wanachopaswa kujua kazi ya
Tambwe ni kufunga na wampe nafasi aifanye kazi yake.
Maguli
ni mchezaji mzuri, anaweza kuja kuwa bora zaidi ya alivyo sasa. Lakini kuwa
naye, isiwe sababu ya kumuona Tambwe hafai kabisa au hana lolote. Wote tunajua
Mrundi huyo ana kipaji cha upachikaji mabao, analijua vema lango kuliko
Watanzania lukuki.
Bado
Tambwe hastahili kukaa benchi kutokana na takwimu za msimu uliopita na hata
baada ya Phiri kutua Simba. Usisahau ni mwenye juhudi, anajitolea kwa ajili ya
Simba na nidhamu yake iko juu.
Maana
yake, kama mchezaji amekamilika. Phiri anapaswa kumpa nafasi zaidi na huenda
anaweza kubadili uamuzi na kuona alichokifanya kilikuwa na haraka au walioamini
hivyo pia waliharakisha mambo.
Kweli
Tambwe hana kasi kama ya Chanongo, Messi, Msuva au Ngassa. Lakini ukweli
linapofikia suala la kumalizia mpira ukaguse nyavu, Mrundi huyo anajua zaidi ya
wote hao. Hivyo Phiri ampe nafasi tena ili akishindwa, basi kusiwe na mwanya wa
kuamini alifanya haraka.
0 COMMENTS:
Post a Comment