October 10, 2014

NKONGO (WA TATU KULIA) NDIYE ATAZICHEZESHA YANGA NA SIMBA. HAPA ILIKUWA MOJA YA MECHI ZA WATANI ALIZOZICHEZESHA.
Bodi ya Ligi (TPLB)imemtangaza mwamuzi wa mechi gumzo zaidi nchini ya watani Simba na Yanga, inatarajiwa kupigwa Oktoba 18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.


Mwamuzi atakayekaa pale kati siku hiyo ni Israel Mujuni Nkongo ambaye kitaaluma ni mwalimu.

Nkongo ambaye aliwahi kufanyiwa fujo na wachezaji wa Yanga mwaka 2012 walipokuwa wakicheza dhidi ya Azam, alisababisha baadhi ya wachezaji wa Yanga kufungiwa na kutozwa faini kutokana na vurugu hizo, ambazo zilianza baada ya kupa kadi ya njano Haruna Niyonzima.


Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga, alimtaja mwamuzi huyo na watakaosimama pembeni siku ya mechi.

“Mwamuzi wa kati ni Nkongo, waamuzi wa pembeni watakuwa ni John Kanyenye wa Mbeya ambaye atakuwa ‘line one’ na katika ‘line two’ atakuwa Ferdinand Chacha wa Mwanza.

“Mwamuzi wa mezani atakuwa Hashimu Abdallah kutoka Dar na mechi kamishna atakuwa Salum Kikwamba akitokea Moshi, kuhusu masuala mengine tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa,” alisema.
Kuhusu mwamuzi huyo, Simba kupitia kwa katibu mkuu wake, Steven Ally, alisema wao hawana la kuzungumza kwa sasa juu ya mwamuzi huyo, huku Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto akisema:

“Sisi tulikuwa tunajua tu, wala hatuna hofu naye kwa kuwa tunaiamini timu yetu, tutaingia uwanjani kucheza soka na wala siyo mambo mengine, tupo tayari kwa mapambano dhidi ya wapinzani wetu wote.”

Katika mechi hiyo ya vurugu, Nkongo alipigwa ngumi na aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Stephano Mwasika ambapo matokeo ya mechi hiyo yalikuwa ni Yanga kufungwa mabao 3-1.




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic