Na Saleh Ally
GUMZO kubwa ndani ya siku hizi mbili ilikuwa ni ile ishu ya Rais Jakaya Kikwete kukabidhiwa rasimu ya katiba baada ya Bunge Maalum la Katiba kumaliza kazi yake.
GUMZO kubwa ndani ya siku hizi mbili ilikuwa ni ile ishu ya Rais Jakaya Kikwete kukabidhiwa rasimu ya katiba baada ya Bunge Maalum la Katiba kumaliza kazi yake.
Uliona shamrashamra za kila aina huku watu mbalimbali
wakipewa nafasi kuzungumza kwenye mkutano huo. Kitu kizuri zaidi, hadi wasanii
walipewa nafasi ya kuzungumza na kutumbuiza, safi.
Inawezekana sikuona, lakini wanamichezo walionekana
hawana maana, hii ni tokea mwanzo wa bunge hilo. watu wameishasahau mashujaa wa
michezo katika nchi na namna michezo ilivyo ajira au chanzo cha kuisaidia
serikali kupambana na tatizo kubwa la ajira!
Hakukuwa na nafasi kubwa ya michezo au ilionekana ni
kitu cha kawaida sana, kosa ambalo limeendelea miaka nenda rudi kama wakati huo
watu walipoona michezo ni uhuni au upotezaji muda.
Katika hilo nilikuwa ninapita tu, lakini niliona si vibaya
kwa pamoja kama tunaweza kuijadili ndoto niliyoota, ikanishangaza lakini
nikafikiri kwani hilo lingefanyika tatizo lingekuwa nini vipi halijawahi
kufanyika, au tuendelee kusubiri.
Wanamichezo kupewa nafasi za kuongoza nchi hii,
simaanishi urais, ninamaanisha kuangalia uwezo wa wanamichezo wengi katika
utendaji na kuwapa nafasi za kusaidia mafanikio katika nchi yetu katika mambo
kadhaa.
Nimeota Rais Kikwete akiwa amewateua Juma Ikangaa kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Manyara na Kanali Iddi Kipingu ambaye ni mstaafu kuwa Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, ndoto bana!
Ingawa nilishangaa lakini kuota kuna faida, kumenipa
nafasi ya kujiuliza maswali na leo nashirikiana na wewe msomaji, lengo si
kumkosoa Rais Kikwete katika uteuzi wake, lakini nataka kusisitiza kuna wanamichezo
wanaweza lakini hawapewi nafasi.
Wakipewa, wanaweza kuwa msaada kwa taifa hili, ninaona
Kipingu na Ikangaa wanaweza kuwa mfano wa wanamichezo wenye nafasi ya kuwa
msaada kwa taifa hili kwa kuwa wana kila sifa ikiwemo ile ya “uchungu wa taifa”
au “mapenzi ya dhati.”
Hakuna asiyejua ushujaa wa Ikangaa ambaye ameshinda
mashindano kibao ya kimataifa ya riadha yakiwemo yale ya Boston ambayo yana
heshima kubwa. Usisahau mashindano ya Japan na China, Ikangaa aliwaburuza
Wazungu na watu wa mataifa mengine wakiwemo Wakenya hata wale wa Ethiopia, hadi
sasa, ndiye Mtanzania mwenye rekodi nyingi za juu kwenye riadha.
Bado ni mwanajeshi, nidhamu yake ya kazi inajulikana
lakini aliwahi kuwa mkuu wa masuala ya michezo, kipindi ambacho michezo
iliibuka na kuanza kufanya vizuri kwenye majeshi, ninamaanisha pamoja na Polisi
na hata Magereza, yeye akiwa ndiye mratibu.
Kanali Kipingu, nani hajui? Wachezaji kibao, wametokea
sehemu mbalimbali na kuibukia Shule ya Sekondari ya Makongo wakati akiwa mkuu
wa shule. Hasheem Thabeet, Juma Kaseja, Boniface Pawasa, Ephraim Makoye, Jerry
Tegete na wengine wengi ambao sasa wanaitwa wakongwe.
Mafanikio ya Makongo yanajulikana na amelitumikia jeshi hadi anastaafu,
tunajua nidhamu ya jeshi, huyu ni mtu sahihi.
Nikirudi kwenye ile ndoto yangu, Ikangaa akiwa Mkuu wa
Mkoa wa Manyara, hakika kwa nidhamu ya jeshi angekuwa na uwezo wa kufanya mambo
mengi ya maendeleo kwa ufasaha, haya ni nje ya michezo.
Lakini kwenye michezo, angeweza kuuinua mkoa huo na hasa
kwa wanariadha kwa kuwa anajua ni nini cha kufanya na bado angeweza kuunganisha
mkoa huo na mashirika au watu wanaohusika na michezo kwenda kusaidia. Ninaamini
kuna vipaji vingi vya riadha, vinateketea katika ukanda huo, lakini hakuna
ubunifu.
Halikadhalika kwa Kanali Kipingu, aliwahi kuzunguka
karibu nchi nzima akisaka vipaji. Akiwa Dodoma angeweza kuusaidia mkoa huo
kuamka kimichezo na hata kwa maendeleo ya kawaida kwa kuwa ameonyesha mfano
kwenye mengi na pia ana sifa ya kuipenda nchi yake kama ilivyo kwa Ikangaa.
Asili ya wanamichezo ni kuwa wepesi, watendaji wazuri na
wenye muono wa mbali. Hapa ninazungumzia watu kariba ya Kipingu na Ikangaa, si
wale wanamichezo ambao kuipenda kwao michezo ni kwa kuwa itawaingizia fedha tu!
Ikangaa na Kipingu, au wanamichezo wengine wa kariba yao
wanaweza kuwa mfano, ni lulu, wasitupwe, wasisahauliwe na serikali iamini
michezo ni mhimili mkubwa wa maendeleo. Ndoto bana, aaah!
0 COMMENTS:
Post a Comment