Kutokana na wachezaji wake saba kuteuliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars inayoivaa Benin, kesho, Kocha Mkuu wa
Yanga, Marcio Maximo ameonekana kushindwa kuendelea na programu nzima kama alivyokuwa akitaka.
Yanga inatarajiwa kukipiga dhidi ya Simba
kwenye Uwanja wa Taifa, Oktoba 18, mwaka huu, ambapo kocha huyo raia wa Brazil,
jana alionekana kuwa katika wakati mgumu kwenye mazoezi ya timu yake na
kujikuta muda mwingi akiwa nje ya uwanja.
Inakumbuka kuwa, Yanga ilitaka kuwazuia wachezaji wake hao
kujiunga na Stars, lakini Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) likaweka ngumu,
hivyo Wanajangwani hao kuamua kuwa wadogo.
Katika mazoezi ya Yanga yanayofanyika Uwanja wa
Shule ya Loyola jijini, Maximo alijikuta akiwa na wachezaji wachache ambao
amekuwa akiwatumia kwenye kikosi cha kwanza na hivyo kutumia muda mwingi katika
mazoezi ya viungo kisha baadaye kuwapanga kucheza ‘full game’.
Maximo amekuwa na kawaida ya kutoa mbinu
mbalimbali katika mazoezi yake, lakini jana hali ilikuwa tofauti na kumfanya
aonekane mpole kwa muda mwingi.
Wachezaji wa Yanga waliojiunga Stars ni;
Deogratius Munish ‘Dida’, Oscar Joshua, Edward Charles, Kelvin Yondani, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa ‘Uncle’ na Simon Msuva.
Wakati huohuo, Maximo ameonyesha kuwashtukia
Simba na kutamka kuwa hataki mchezaji wake yeyote kuidharau timu hiyo ambayo
imepata sare katika mechi tatu mfululizo.
“Nimeshawatahadharisha wachezaji wangu mapema
kuelekea kwenye mechi ya Simba kuwa wanatakiwa kuwa makini na hawatakiwi
kuidharau Simba kutokana na matokeo yao,” alisema Maximo.
0 COMMENTS:
Post a Comment