Na Saleh Ally
MIAKA 15 iliyopita, Ambwene Allen Yessayah
aliamua kutoka chumbani alipokuwa baada ya kukata shauri kwamba anafanya muziki
na kumfuata mama yake alipokuwa.
Yessayah sasa maarufu kama AY, alimfuata mama
yake mzazi ambaye alikuwa mmoja wa walimu maarufu mkoani Morogoro na kumueleza
nia yake ya kutaka kufanya muziki.
Safari hii alikuwa ‘siriaz’, alichoka mambo ya
kuimba chumbani na alitaka kurekodi wimbo utakaosikika redioni, lakini fedha
ndiyo lilikuwa tatizo kubwa.
“Niliamua kuwa wazi, nilimuomba mama shilingi
elfu ishirini kwa ajili ya kurekodi wimbo. Mwisho alikubali kwa kuwa niliamini
nikirekodi lazima utafanya vizuri, tutasikika na baada ya hapo tutaanza kupata
fedha,” anasema AY katika mahojiano na gazeti hili.
“Hatukuwa na uwezo nyumbani, elfu ishirini ilikuwa
nyingi lakini mama ni mama. Ingawa baba hakupenda mambo ya muziki. Kwa fedha
hizo nikafunga safari hadi Dar es Salaam kwenye studio za Master J, kwa
kushirikiana na wenzangu wa Kundi la OSG, tukarekodi wimbo wetu wa kwanza kwa
shilingi elfu kumi.”
Wimbo wa kwanza wa kundi hilo lililokuwa
linaundwa na marafiki watatu, AY, Buff G na Snare unajulikana kama ‘Kipi
Kikusikitishacho’.
“Siku chache baada ya kuanza kupigwa redioni,
ulifika Top Ten. Nakumbuka nikiwa Morogoro niliambiwa natafutwa na watangazaji
wa East Africa kutaka kufanyiwa mahojiano, nikapanda basi kutoka Morogoro hadi
Dar kumfuata Steve B.”
Hiyo ndiyo safari ya msanii maarufu wa muziki
wa kizazi kipya, AY ambaye amekuwa akifanya vizuri kila kukicha.
Msanii ambaye Nasibu Abdul maarufu kama Diamond’
aliandika kwenye Mtandao wa Kijamii wa Instagram kuwa ndiye amewapa moyo
wasanii kupambana hadi nje ya Tanzania.
Siku moja baadaye, akatupia ujumbe kwenye
Instagram akisema anaamini Diamond atashinda tuzo mbili Channel O.
Siku chache, Diamond amefanikiwa kuchota tuzo
tatu za Channel O, vipi AY alijua mapema?
“Niliamka asubuhi, moyo ukaniambia Diamond
atashinda zaidi ya tuzo moja. Niliangalia vipengele anavyogombea, nikaona
itakuwa ni zaidi ya tuzo moja atakayoshinda, ndiyo nikaandika.
“Najivunia Diamond, tumeshauriana mara kadhaa.
Ukiona umemhamasisha mtu, halafu anafanikiwa, unasikia raha sana.
“Najua wapo waliochukia, lakini sasa ni wakati
wa kumuunga mkono. Mwakani Tanzania ipeleke hata wanamuziki kumi kwenye Channel
O. Nakumbuka nimekuwa nikienda peke yangu kutoka Tanzania, Kenya wanaleta
wanamuziki kumi, kwa nini?
“Tena kabla tulikuwa tunashinda tuzo ya Afrika
Mashariki tu, sasa Diamond ameshinda hadi msanii anayechipukia waliyokuwa
wakishinda Wanigeria na Wasauz. Huu ndiyo wakati mwafaka, mwakani tuzo hiyo ije
nyumbani tena.
“Tusione ni rahisi kwa Diamond au nilipofikia
mimi ilikuwa rahisi tu. Lazima tujiamini, tujitume, tujikubali na kushirikiana
maana hauwezi kuinuka peke yako.”
Team Diamond Vs Team Kiba:
“Nimekuwa nikisikia, kwamba wanashindana
kupitia hizo timu. Sidhani kama huu ni wakati mwafaka, naona kama kuna watu
wanataka kuwatumia kusingizia wanashindana.
“Waamke, waone mbele. Kiba na Diamond washikane
mikono, wasonge mbele na kazi zao ni nzuri, hakuna haja ya hizo timu, mimi
sioni kama ni sahihi.
“Nataka kuwaunga mkono Diamond na Kiba wakati
wowote kwa kuwa mimi ni kati ya waliopigania muziki huu kufika hapa. Roho
inauma nikiona mtu anafanya utani, nimesumbuka sana.
“Mfano wakati huo nilisafiri hadi Uganda kwa
saa 24, lengo ni kwenda kufanya shoo ya bure tu. Kisa, nilitaka kufahamika!
Imenisaidia kujitangaza, kuitangaza nchi yangu ndiyo maana leo kwa wengine
inakuwa rahisi.
“Nakumbuka nilitembea kwa miguu usiku saa tisa
kutoka Masaki hadi Morocco, lengo ni kupunguza nauli. Sikuwa nayo, nilishinda
njaa mara kibao. Siwezi kufurahi nikiona msanii anatokea anaharibu tu, kama
anaona hawezi kuwa msanii, aachane na kuimba, afanye kitu kingine.
“Hata ukisema watoto, enzi zetu tulikuwa
tunapambana kuwaonyesha wazazi na jamii muziki ni sanaa na itakuwa ajira. Leo
wazazi wako tayari kuwasapoti watoto wao, utaona ni mabadiliko makubwa sana,
ndiyo maana nasisitiza umoja.”
Songi jipya:
“Kwa kweli niwashukuru sana Watanzania, Wimbo
wa Touch Me niliowashikirisha Shawn Kingston na Ms Triniti umepokelewa vizuri
na unapendwa. Una kiwango cha juu, achana tu na niliowashirikisha, lakini hata
maprodyuza (Reily Urick na Zaire Koalo wa Studio za Network Showbizz), wako
vizuri. Hawa jamaa wako California, Marekani na wana uzoefu.
“Watanzania wanielewe, lengo si kujulikana
Marekani au kufanya vizuri huko. Nataka kufanya vizuri hapa nyumbani kwa
kushirikiana na watu wa ‘levo’ za juu.
“Hata soka ina ‘levo’ zake, mfano ligi kuu,
ligi ya mabingwa. Mchezaji anajipima kutokana na kucheza mashindano makubwa,
ndiyo ninachofanya.
“Sasa niko katika hatua za mwisho, inafuatia
video ambayo pia imetengenezwa kwa kiwango cha juu kabisa,” anasema AY.
0 COMMENTS:
Post a Comment