Akiwa na uso wa huzuni, aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, jana
alifika kwenye mazoezi ya timu hiyo asubuhi na kuwaaga wachezaji wake.
Hiyo
ni baada ya kupewa taarifa za kutimuliwa na uongozi wa timu hiyo kufuatia
kipigo cha mabao 2-0 walichokipata dhidi ya Simba katika mechi ya Nani Mtani
Jembe iliyochezwa wikiendi iliyopita.
Maximo
alifika mazoezini hapo saa 2:35 akiwa na msaidizi wake, Leonardo Neiva, kiungo
mkabaji wa timu hiyo raia wa Brazili, Emerson De Oliviera, ambao wote wamesitishiwa
mikataba yao kwa ajili ya kuwaaga na Andrey Coutinho ambaye aliachwa kuendelea
na mazoezi huku hao wengine wakiondoka.
Mbrazili
huyo, aliwaaga wachezaji hao, zoezi lililotumia dakika kumi kwenye Uwanja wa
Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam kabla ya kuondoka na gari ndogo aina ya
Toyota Hiace kuelekea hotelini alipokwenda kufanya mazungumzo na viongozi wa
timu hiyo.
Kwa
mujibu wa mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, kocha huyo mara baada ya kufika
uwanjani hapo, aliwaita wachezaji hao na kuzungumza nao mambo mbalimbali
kuhusiana na timu.
Chanzo
hicho kilisema, katika mazungumzo yake aliwatakia kila la kheri wachezaji na
viongozi aliowaacha, Shadrack Nsajigwa na Salvatory Edward katika kuipa
mafanikio ya mataji ya ubingwa kwa kuanzia na Ligi Kuu Bara.
“Inasikitisha
kiukweli kocha wetu kufukuzwa ghafla, wamemshtukiza, ilitakiwa wampe muda
kidogo wa kuiandaa timu na siyo kumfukuza baada ya kufungwa na Simba katika
Nani Mtani Jembe.
“Alifika
leo asubuhi akiwa na msaidizi wake, Neiva, Emerson na Coutinho kwa ajili ya
kutuaga wachezaji, baada ya kufika tukazungumza naye kama dakika kumi na
baadaye akaingia kwenye gari na kuondoka na kumuacha Coutinho akiendelea na
mazoezi.
“Aliongea
maneno mengi, lakini kikubwa alitutia moyo wa kuendelea kufanya vizuri katika
mechi za ligi kuu na kututaka kumpa ushirikiano kocha mpya atakayekuja
kutufundisha,” alisema mchezaji huyo huku akionekana kuwa na majonzi.
Maximo
ambaye ameiacha Yanga ikiwa katika nafasi ya pili kwenye ligi akiwa kwenye gari
wakati anatoka kwenye lango la Loyola, alionekana kuwa na huzuni kubwa, huku
akikuna kichwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment