MAFANIKIO kwa mchezaji yeyote ni kutokana na
anachokifanya duniani kwa maana ya kazi yake nzuri, lakini anafanya nini kwa
maana ya kuvuna makombe.
Ukizungumzia Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Yanga, unaweza
kusema ana mafanikio akiwa na Yanga kwa kuwa imebeba makombe kadhaa ya Ligi Kuu
Bara akiwa ndani ya kikosi.
Kwa kipimo cha uwezo wa kisoka kwa Afrika, basi
Cannavaro wa Yanga anaweza kuwa mmoja wa mabeki vipimo kwa kuwa huenda
anaongoza kwa kupambana au kuwakaba washambuliaji nyota kama Samuel Eto’o,
Didier Drogba, Godfrey Bonny, Mohammed Aboutrika na wengine wengi waliowahi
kukutana na Yanga au Taifa Stars.
Utaona namna gani thamani ya Cannavaro inavyoweza
kupambana hata kwa kuonyesha umahiri wa kuwadhibiti wachezaji nyota kutoka
sehemu mbalimbali duniani. Hakuna ubishi anaweza kuwa ndiye beki bora wa kati
kwa Tanzania kipindi hiki.
Unapozungumzia beki bora duniani katika wote wanaocheza
kwa kipindi hiki, utapindua vipi kwa beki wa kati wa Real Madrid na Hispania,
Sergio Ramos Garcia!
‘Brother Man’ mwenye sura ya kupendeza, lakini unaweza
kumuita mtukutu anayeijua kazi yake na amefanikiwa kuliko beki mwingine yeyote
katika kipindi hiki.
Huenda unaweza kusema amepita njia ya Cares Puyol au ‘ndugu’
yake Gerard Pique waliocheza katika kikosi cha Barcelona kilichokuwa fomu ya
juu miaka mitatu, minne iliyopita.
Kwa sasa, Ramos ndiyo mfalme wa mabeki, lakini
inawezekana amekwenda juu zaidi hata kutikisa kwenye ‘levo’ ya wachezaji nyota
kama akina Cristiano Ronaldo.
Wakati wa fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa
Klabu, wakati Madrid inabeba ubingwa huo mbele ya San Lorenzo kwa kuichapa
mabao 3-0, Ramos aliibuka ndiye mchezaji bora wa mchezo huo na kubeba mpira wa
dhahabu mbele ya Ronaldo aliyeshika nafasi ya pili.
Pamoja na kucheza vizuri na kuhakikisha Madrid haipotezi
siku hiyo, Ramos alifunga bao moja. Alionyesha kiwango cha juu hadi kufikia
kumpita Ronaldo.
Ramos ndiye beki aliyebeba makombe yote makubwa, bora na
yanayotambulika akiwa na Real Madrid ambayo ni nahodha msaidizi pia Hispania.
La Liga, Copa del Rey, Super Cup Hispania na Ulaya, Ligi
ya Mabingwa Ulaya, yote amechukua kwa upande wa klabu. Kwa upande wa timu ya
taifa, amechukua Kombe la Ulaya mara mbili, pia Kombe la Dunia.
Ubora wa kazi yake ndiyo unaofuta sifa ya utukutu
aliyonao kwa kuwa Ramos ni mmoja wa mabeki wanaoongoza kwa kulambwa kadi
nyekundu.
Ramos amewahi kuadhibiwa zaidi ya mara mbili baada ya
mechi kuchezwa, akituhumiwa kwa faulo za ‘chinichini’. Yumo katika kumi bora ya
mabeki wababe au wenye tabia mbaya.
Pia yumo kwenye kundi la mabeki 10 duniani wanaoogopewa na
mshambuliaji yeyote mkali duniani bora ya kujali anacheza dhidi yake nyumbani
au ugenini.
Beki huyo aliyeanzia kuchipukia kisoka akiwa na Sevilla,
tayari ameichezea Madrid mechi 300 za La Liga na moja kwa moja ameingia katika
rekodi ya mmoja wa wachezaji waliofanikiwa zaidi duniani.
Ukijumlisha na michuano mingine, Ramos ameichezea Madrid
mechi 425 na kwa umri wa miaka 28 alionao sasa, maana yake ana uwezo wa kucheza
mechi nyingi zaidi ya 200, hali inayomuweka kuingia kwenye rekodi nyingine ya
wachezaji waliocheza mechi nyingi zaidi.
Ramos ambaye amebatizwa na mashabiki wa Real Madrid jina
la Chuma, anaingia kwenye tano bora ya wachezaji wanaofanya zaidi mazoezi
kuhakikisha wanakuwa fiti.
Katika kikosi cha Madrid, wakati wa mazoezi magumu,
Ramos yuko kwenye tatu bora ya wale wanaokimbia sana, wanaokimbia kwa muda
mrefu bila ya kuchoka.
Maana yake, mafanikio yake hayakupatikana kwa urahisi na
bado anaendelea kujituma. Utukutu wake, unaweza kuwa sehemu ya mafunzo kwamba
anajua anachokifanya na ndiyo maana leo ni rahisi kuhesabu makombe, kuliko
utukutu wake kwa kuwa anapata mafanikio.
MAKOMBE:
Real Madrid
La Liga: 2006–07, 2007–08, 2011–12
Copa del Rey: 2010–11, 2013–14
Super Cup (Hispania): 2008, 2012
Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2013–14
UEFA Super Cup: 2014
Kombe la Dunia (klabu): 2014
Hispania:
Kombe la Dunia: 2010
Ubingwa wa Ulaya: 2008, 2012
0 COMMENTS:
Post a Comment