Na
Saleh Ally
MAKOCHA
wawili wa Yanga na Simba, Marcio Maximo na Patrick Phiri, wote wametupiwa
virago na klabu hizo mbili.
Simba
na Yanga ndiyo klabu kongwe, kama zilivyo nyingine zenye hadhi yake zinachotaka
ni matokeo mazuri na ya kuridhisha, si hadithi.
Kocha
wa kariba ya Phiri na Maximo, hakuna ubishi ni wale waliopiga hatua,
wanaoaminika ni bora na uwezo wao ulikuwa unajulikana.
Hisia
kwamba hawana uwezo zilitanda, rekodi zikawa zinawahukumu lakini ukweli unabaki
kuna mambo pia yalikuwa matatizo na si matatizo yao.
Katika
Ligi Kuu Bara, rekodi ya Maximo raia wa Brazil ilikuwa ni kucheza mechi saba,
kushinda nne, sare moja na kupoteza mbili dhidi ya Mtibwa Sugar na Kagera
Sugar. Aliiacha timu ikiwa katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 13.
Phiri
alicheza mechi nane, alishinda moja, sare sita na kupoteza moja. Ameiacha Simba
ikiwa katika nafasi ya tisa ikiwa na pointi tisa, maana yake wastani wa kikosi
chake ni sare tisa.
Maximo
aliondoka baada ya kufungwa mabao 2-0 na watani wao, Simba katika mechi ya Nani
Mtani Jembe lakini bado rekodi hazikuwa zimefikia kiwango cha chini kusema
hawezi, lakini nitakubaliana na Yanga kwamba kiwango cha uchezaji cha kikosi
chao hakikuwa cha kuridhisha.
Kwa
upande wa Phiri, angalau timu ilikuwa inacheza lakini bado haikuweza kufunga
mabao na sare sita mfululizo, zinakera.
Sina
sababu ya kuingilia uamuzi wa Yanga na Simba ila napenda kuendelea kuwa muwazi
kwamba kufeli kwa vikosi vyao, sababu haiwezi kuwa makocha hao pekee.
Kuna
uwezekano wa asilimia nyingi sana kwamba hata makocha wapya, Goran Kuponovic
raia wa Serbia anayechukua nafasi ya Phiri na Hans van der Pluijm anayeziba ya
Maximo, nao wanaweza kuonekana hakuna kitu kama uongozi wa klabu hizo utaamua
kubadili fenicha sebuleni ili kuridhisha wageni watakaowatembelea, wakiwa
wamesahau kuziba matundu kwenye paa la nyumba huku wakijua ni kipindi cha
masika.
Mnajua
ndani ya klabu zenu kuna majungu, kuna watu wasio na kazi yao kupitisha majungu
kutoka kwa mchezaji huyu, kwenda kwa yule kwa lengo la kuonekana mtu mzuri,
baadaye apewe fedha ili aendeleze maisha yake.
Watu
hao wasingekuwa na uwezo wa kuingia ndani ya timu kama hawapati ruhusa ya
viongozi. Ni wapambe wa viongozi na wanaonekana ni muhimu, ndiyo maana wana
nafasi ya kuzivuruga timu hizo.
Kitu
cha pili, umoja na upendo. Ndani ya timu hizi mbili, bado hakuna upendo wa
kutosha. Kuna makundi hata ndani ya wachezaji na baadhi ya viongozi si watu
wenye busara, kazi yao ni kulaumu tu au kuwaumiza au kuwavunja nguvu wachezaji.
Wale
makocha mmewaondoa, mmeleta wapya. Mmesahau pia hawakuwa na vifaa vya kutosha
kufanya kazi zao kwa ufasaha.
Yanga
na Simba hadi leo zimeendelea kuishi kwa kuwa na viwanja vya kukodi. Wakati
mwingine makocha wanashindwa kufanya kazi zao vizuri.
Mfano
kocha anataka wafanye mazoezi mara mbili kwa siku, kwa kuwa klabu inalazimika
kulipa Sh 100,000 hadi 300,000 kwa siku, inamlazimisha kufanya mara moja.
Ernie Brandts aliomba Yanga apewe magoli
madogo kwa ajili ya kutoa mafunzo muhimu katika ufungaji, ilishindikana na
gharama yake ukiangalia ilikuwa haizidi hata Sh milioni moja!
Hivyo
hata Kopunovic na Pluijm hawatakuwa na muda mrefu kwa kuwa Maximo na Phiri
kuonekana tatizo pekee ni kujikaanga kwa mafuta yenu wenyewe.
Kingine
muhimu ni nidhamu. Nani kati yenu anaweza kukataa kuna tatizo hilo ndani ya
vikosi vyenu? Mnajua kuna wachezaji wanaojikweza, mnajua kuna wachezaji wa
kigeni wanataka kuwa na nguvu zaidi ya kocha.
Ujio
wa Pluijm na Kopunovic unaweza kubadili upepo kwa kuwa watashikilia suala la
nidhamu. Vyema muwaunge mkono na mkitaka kikosi bora, kusiwe na mchezaji bora
kuliko wengine.
Mfano
Emmanuel Okwi kwa Simba au Kpah Sherman kwa Yanga, wakitaka kuwa ‘special’
kuliko wenzao. Mbona Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Madrid
wako sawa na wenzao ndani ya klabu zao!
Hakuna
mmoja juu ya wengine. Pia vizuri mkaacha nguvu ya uendeshaji wa kikosi ikawa
kwa kocha ili akishindwa ashindwe kweli.
Muhimu
mrekebishe hayo ambayo huenda yalichangia kuwaangusha mliowafukuza ili
yasichangie tena kuwafukuza mlionao.
0 COMMENTS:
Post a Comment