WAKATI unaanza mwaka 2014, matumaini ya
Watanzania wapenda michezo yalikuwa yako juu sana kutokana na mambo mengi
yaliyojitokeza.
Wapenda michezo iwe katika ridha, ngumi za
kulipwa, soka, netiboli na michezo mingine waliamini maendeleo yanafuatia.
Matumaini yao yalijengwa kutokana na viongozi wengi kuwa na maneno matamu.
Wapo waliowaamini kwa maneno yao matamu, wapo
waliwaamini viongozi wa michezo fulani kama vile riadha kwa kuwa waliwahi kuwa
wanariadha bora, lakini hadi jana tumeumaliza mwaka 2014, hakuna cha maana
kilichofanywa ambacho wanaweza kujisifia hadi sasa.
Inaonekana hivi; michezo yetu haina mwenyewe,
fedha za michezo hazina mwenyewe na mtu anaweza kuchukua chochote na hakuna
atakayembugudhi, inaonekana ni kama jambo la kawaida tu na ambaye anapiga
kelele kuhoji, anaonekana anapoteza muda tu.
Kuna mambo mengi yamepita katika kipindi cha
mwaka 2014, lakini jibu la mwisho katika kilichotokea ni hivi; hakuna maendeleo
wala jambo lolote lililojitokeza katika maendeleo ya michezo nchini.
Utakubaliana na mimi kwamba michezo ni biashara
kubwa sana, soka unaweza kuwa mfano mzuri. Fedha zake hazisaidii kuleta
maendeleo kwenye mchezo wenyewe kwa kuwa zinaingia kwenye mifuko ya wajanja
wachache ambao wanageuka kuwa maadui wakubwa kwa watu kama akina Saleh Ally
wanaojaribu kuhoji.
2015 ndiyo hii, baada ya ujinga mwingi kupita
mwaka 2014, huenda michezo ikaendelea kuwa moja ya mambo ya kijinga wanayofanya
Watanzania kwa kuwa faida zinazopatikana ni kwa ajili ya wabadhirifu wachache.
Inaonekana ni ujinga kwa kuwa wakati mwingine
michezo badala ya kuwa faida kwa taifa letu, imegeuka kuwa furaha kwa wachache,
kero kwa wengi. Faida kwa wachache na hasara kwa Watanzania wengi ambao
hawawezi kuinua mdomo na kujisemea.
Hatuna ujanja, lazima tubadilike na kuondoa
magugu ya ujinga kwenye michezo kwa mwaka 2015 na kujitathmini kama kweli kuna
jambo kubwa la maana tulilifanya na kama hakuna, tufanye nini ili kuepuka
kuumaliza mwaka huu kama tulivyoumaliza 2014.
Magugu haya pia yanapaswa kufanyiwa kazi,
yaondolewe mara moja.
Wizi:
Katika michezo, wizi umekuwa wa waziwazi na
watu wanachukua fedha wanavyotaka, hawataki waulizwe na wanawashangaa wanaohoji.
Ukweli fedha zinazopatikana kwenye michezo na
hasa soka, kama zikitumika vizuri, maendeleo yatakua kwa kasi kubwa. Wanaokula
wamekuwa ni mchwa wabinafsi wanaotaka kujishibisha wao tu. Waache fedha hizo
ziingie kwenye mishipa ya maendeleo ya mchezo wa soka.
Majungu:
Huu ndiyo umekuwa mtaji wa watu wengi wapenda
michezo, ndiyo maana kila kukicha kuna makundi kwenye ngumi, netiboli, soka,
riadha ndiyo usiseme. Vipi mtaendelea wakati hampendani, kazi yenu ni
kusengenyana na kuchekeana machoni? Lazima tuache na kuamini ukweli na
kusameheana ndiyo njia sahihi ya kusonga mbele.
Ujeuri:
Viongozi wanaoingia madarakani, mfano mchezo wa
soka na ule wa riadha wamekuwa wababe mno, wasiotaka kumsikiliza yeyote kwa
kuwa wanajua sana na wao ndiyo kila kitu.
Viongozi hao wamekuwa kama vile madikteta,
wanataka kuendesha mambo kibabe, wanataka kutoulizwa au kuelezwa. Wamesahau
vyama si mali yao, klabu ni za wananchi au makampuni au mashirika ya umma. Sasa
kwa nini wasiambiwe au wasihojiwe?
Visasi:
Hiki ndiyo kitu kibaya zaidi. Viongozi wa
michezo hawapendani na kila mmoja angefurahi kuona mwingine anaharibu na
wamekuwa wakifanyiana visasi vya chinichini, kila mmoja akitaka kumuona
mwenzake anaharibu.
Kama utakuwa na watu wanaotaka kuwaona wengine
wanaharibu, maendeleo yatapatikana vipi katika kitu kinaoongozwa na watu hao
waliogawanyika kwa makundi? Huu ni ujinga, vizuri tukauacha ukaenda na mwaka
2014, ili angalau mwaka 2015 nao usiwe wa ujinga. Kama hatutaki, basi na 2015
tutauendeleza ujinga wetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment