Na
Saleh Ally
MSHAMBULIAJI
nyota wa TP Mazembe, Mbwana Samatta ameanza majaribio na Klabu ya CSKA Moscow
ya Urusi akiwania kupata nafasi ya kuitumikia.
CSKA
Moscow ni moja ya klabu kubwa kabisa barani Ulaya na duniani kote, si vibaya
kusema ni klabu ya kiwango cha akina Chelsea, Manchester United, Arsenal na
wengine.
Siku
chache kabla Samatta kwenda Urusi kwa ajili ya majaribio na baadaye kusafiri na
timu hiyo hadi Hispania kwa ajili ya kambi, meneja wake, Jamal Kisongo
aliliambia Championi kwamba juhudi kubwa zilifanyika kumshawishi mmiliki wa TP
Mazembe, Moise Katumbi akubali.
Bilionea
Katumbi alitaka Samatta aendelee kubaki TP Mazembe kwa kuwa ndiye mchezaji
tegemeo na kipenzi chake. Hakuona kama kuna sababu ya kumuachia huku akiwa
tayari kumuongezea dau zaidi ya dola 10,000 ambayo hulipwa sasa.
Kumuondoa
Samatta ndani ya Mazembe ndiyo ushindi namba moja na huenda hapo ndiyo pongezi
ndiyo zilikuwa zinahitajika. Si sasa.
Sitaki
kuingilia uhuru wa wale wanaompongeza Samatta sasa, lakini huu ni wakati
mwafaka wa kumpa moyo na ikiwezekana kumuombea dua afanikiwe kwa kuwa hatuna
sababu ya kuuliza juhudi kwa Samatta hadi alipofikia.
Tunampongeza
kwa kupata majaribio? Naona ni sawa na kumpongeza wakati akiwa vitani kwamba
hongera kwa kupigana. Tuwe naye, tumpe moyo, tumueleze Watanzania
wanavyomtegemea na akishinda tumpongeze. Akishindwa tumuambie kateleza, ainuke
asonge na tumuunge mkono hadi atakaposhinda na hapo ndiyo wakati wa pongezi.
Unakumbuka
alikuja baada ya Mussa Hassan Mgosi, Mrisho Ngassa, Shabani Nditi na wengine
wengi unaowajua. Juhudi na maarifa, uthubutu wa kukubali kwamba kufanya vema
nje ya Tanzania inawezekana.
Uthubutu
pia wa kukubali kubadilisha kwamba Simba na Yanga si mwisho wa mafanikio yote.
Samatta anajiamini na mfano mzuri wa utofauti wake na wachezaji wengine ulianza
kuonekana pale alipogoma kucheza Simba.
Aligoma
kwa kuwa waliahidi kumpa gari, lakini hawakufanya hivyo na badala yake wakaanza
kuuza maneno. Akakaa nyumbani hadi walipompa walichoahidi. Kama unakumbuka,
siku chache TP Mazembe wakamchukua.
Wachezaji
wangapi wa Tanzania wamekwenda nje ya nchi yetu wakafanya madudu. Wako
waliolipwa vizuri, walipewa nyumba za kuishi halafu siku chache wakarudi
nyumbani kisa wamekumbuka kuja kuungana na wenzao kucheza mechi za mchangani au
kuvuta pamoja sigara kubwa?
Wangapi
unawajua hawaamini kucheza nchi za jirani kama Kenya, Uganda, DR Congo, Rwanda
na kwingine ni njia ya kusonga kulikoendelea zaidi kisoka kama Uganda?
Unawajua
wangapi ambao wanaona kucheza Yanga au Simba ndiyo mwisho kabisa wa ndoto zao
na wala hawahitaji tena kwenda kwingine?
Samatta
ni ‘figa’ ya mabadiliko ya Tanzania, hivyo tumuombee na huenda akasaidia
kujenga kizazi kipya kinachojiamini, kilicholenga kwenda mbele zaidi ya Yanga
na Simba.
Ndani
ya CSKA Moscow kuna nyota kadhaa kutoka Afrika lakini hawa wawili, Ahmed Musa
kutoka Nigeria na Seydou Doumbia wa Ivory Coast ndiyo wanaofanya vizuri zaidi.
Kwa
msimu huu kila mmoja ana mabao saba. Ninaamini kama Samatta atapata nafasi,
basi hata wao watakuwa na hofu kubwa kwa kuwa uwezo wake uko juu zaidi.
Kama
atashindwa, timu nyingine tatu zinamsubiri ili zimpe nafasi ya kufanya
majaribio, moja wapo St Etienne ya Ufaransa ambayo si klabu ndogo.
Ndiyo
maana nikasema, huu si wakati wa pongezi kwa Samatta. Badala yake dua na kuwa
naye pamoja, wakati wa ushindi, pongezi zitafuatia na akifanikiwa basi safari
moja au hatua muhimu itakuwa imepigwa katika maendeleo ya soka nchini.
0 COMMENTS:
Post a Comment