MICHAEL AKIMKABA TAMBWE KATIKA MECHI YA LIGI KUU BARA... |
PICHA ya ukurasa wa mbele wa gazeti namba moja
la michezo nchini, Championi ilionyesha beki George Michael wa Ruvu Shooting
akimkaba mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara ilimalizika kwa
sare ya bila mabao huku Yanga ikishindwa kuendeleza ubabe dhidi ya timu hiyo ya
jeshi ambayo msimu uliopita ilikubali kipigo cha mabao saba.
Ingawa mashabiki wa Yanga walionyesha wazi
kukerwa na sare hiyo, lakini kabali ya Michael ‘iliyogunduliwa’ na Championi
ndiyo ilikuwa gumzo zaidi na kufanya hali ya hewa ibadilike kabisa.
Wapenda mpira waungwana, waliungana bila ya
kujadili ushabiki wa Yanga na Simba au timu nyingine na kukemea kitendo kile
cha kikatili ambacho muungwana yeyote, kamwe hawezi kuungana nacho.
Viko vyombo vya habari navyo vilisimama kidete
kukikemea kitendo hicho, vingine vikashindwa kusimama na kuonyesha hakikuwa
sahihi kwa hofu ya kushindwa au kuonekana havikuwa vya kwanza kukiibua kitendo
hicho na kukizungumzia zaidi, huenda Championi litapata sifa nyingi sana!
Ukweli unabaki palepale, picha hiyo
ilichapishwa kwenye Gazeti la Championi na ndiyo iliyozua gumzo. Haitabadilika
na jambo la msingi si kuangalia nani atapata sifa kubwa sana, badala yake
tusaidie vipi matendo ya kikatili kama hayo kutofanyika.
Ninachoshangazwa, wako wanaotetea na hasa
baadhi ya viongozi wa Ruvu Shooting. Wanaingiza mzaha au utani katika jambo
linalotaka kudhibitisha kuwa mchezo wa soka si wa kiungwana.
Wako wanaotaka kulikwepesha jambo hilo lionekane
kama linakuzwa au ni la kawaida sana. Huenda wanasahau kuwa kwa kiwango cha
Ligi Kuu Bara, basi huenda lililotokea ni kiwango cha soka la mchangani.
Wako wanaotaka Michael achukuliwe hatua kali.
Mimi naungana nao, lakini napendekeza achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na
kusiwe na jazba katika utekelezaji wake.
Ninashauri kwa kuwa nimeelezwa Michael ni
askari, kuna kila sababu ya afande huyo kujitokeza na kulizungumzia suala hilo
hadharani kama ambavyo Tambwe alizungumza na waandishi wa habari, juzi.
Afande Michael ajitokeze, azungumze kwa kuwa
sisi wote ni binadamu na tunakosea. Kila anayekosea pia ana nafasi ya
kurekebisha makosa yake hasa kama atakuwa ameanza kwa kuyakubali makosa
aliyotenda. Kama haukubali ulipojikwaa, basi kujikwaa yatakuwa ndiyo maisha
yako milele.
Michael ajitokeze na kueleza ilivyokuwa. Kama
anaamini amekosea basi aombe radhi na kama inawezekana hata kama atapewa adhabu
basi wako wanaopaswa kumsamehe.
Sidhani kama kila mmoja atamuadhibu kwa kuwa
waliokasirishwa ni wengi. Kama ataonyesha uungwana wa kujutia kosa, wadau wengi
watamsamehe wakiamini naye ni binadamu kama wao ndiyo maana amekubali kuhusiana
na kosa.
Pamoja hivyo, bado ninaweza kuweka msisitizo
kuhusiana na suala la kuangaliwa kuhusiana na uchezeshaji wa waamuzi na ukuzaji
wa viwango vyao.
Bado tunahitaji waamuzi imara ambao wanaweza
kufanya kazi yao kwa ufasaha kuliko kuwa ni wenye hofu ya lawama.
Anayeogopa lawama, kamwe hawezi kuifanya kazi
yake kwa ufasaha na kiwango cha juu. Naamini mwamuzi Mohamed Teofili wa
Morogoro au wasaidizi wake walikuwa wamejawa hofu muda mwingi na huenda kuna
matukio waliyashuhudia lakini wakashindwa kuchukua hatua kutokana na uoga.
Niikumbushe TFF kuwa, waamuzi ambao wamepigwa
kwenye michuano ya Ligi Daraja la Kwanza, wangependa kuona shirikisho hilo
linawachukulia hatua wahusika, tena mara moja.
Wakifanya hivyo, watasaidia kuwaondolea waamuzi
hao woga na pia kuwapa woga wale wenye tabia ya kupiga waamuzi kwamba wakifanya
upuuzi huo, haraka sheria itachukua mkono wake. Picha za mchezaji anamkimbiza
mwamuzi na wengine wakimpiga zipo na zinaweza kufanyiwa kazi ili kulisafisha
soka hapa nyumbani, ukweli sasa limechafuka!
0 COMMENTS:
Post a Comment