Saa zaidi ya 24 baada ya Yanga kutishia kugomea
kuingiza timu uwanjani, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema endapo
klabu hiyo itathubutu kufanya hivyo, basi itakutana na rungu la sheria kali za
Ligi Kuu Bara.
Yanga ilitoa tamko hilo, ikishinikisha TFF
iwachukulie hatua kali waamuzi wa mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting, wachezaji
wa Ruvu waliomchezea ‘kibabe’ straika wao, Amissi Tambwe.
Selestine Mwesigwa ambaye ni Katibu wa TFF,
ameliambia gazeti hili kuwa, wao wanasubiri taarifa ya maandishi na hawawezi
kufanya kazi kwa shinikizo.
“Kuhusu suala la kugoma, nafikiri Yanga
wanaelewa kila kitu kuhusu sheria, kanuni na taratibu za ligi, kama kuna
malalamiko, wao wanajua waende wapi.
“Kuhusu kutoa maamuzi ya mchezo wa Yanga na
Ruvu, hatuwezi kuzungumza lolote kwa kuwa hatujapata ripoti husika ya mchezo.
“Kuhusu ripoti ya kamishaa kuwekwa wazi hilo
halitawezekana kwa kuwa hiyo siyo taratibu, kama hii ikiwekwa wazi ina maana
basi kila ripoti itabidi iwekwe wazi,” alisema Mwesigwa.
Tambwe alikutana na shuruba hiyo katika mechi
ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa ambapo
alikuwa na wakati mgumu katika kumpita beki wa Ruvu, George Michael.
0 COMMENTS:
Post a Comment