February 13, 2015


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limekuwa likichukua hatua kutokana na matukio ya vurugu katika Ligi Daraja la Kwanza lakini inavyoonekana kazi bado ni ngumu kukomesha vurugu kutokana na matukio mengi ya ajabu yanayoendelea kutokea kwenye michezo ya ligi hiyo.


Vurugu zilizotokea kwenye mechi ya Toto Africans dhidi ya Geita Gold Sports kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Nyankumbu na ile ya Mwadui dhidi ya Polisi Tabora, zinatoa picha kuwa bado kuna vitu havipo sawa.


Geita vs Toto 
Awali, mashabiki wa Geita walionyesha chuki ya wazi kwa wenzao wa Toto kwa kuwaambia lazima wawapige.

Baada ya mchezaji wa Geita, Venance Joseph kuunawa mpira katika dakika ya 14 na mwamuzi kuamuru penalti, kilichotokea baada ya hapo ni vurugu kubwa, mashabiki kuvamia uwanja, polisi kupambana na mashabiki na mwamuzi kupigwa kichwa na mchezaji wa Geita.

Licha ya uwepo wa viongozi wa serikali katika mchezo huo, mazingira ya uwanja huo pia ni hatarishi kwa usalama wa wachezaji na wahusika kwa kuwa hauna sifa za kuchezewa mechi kubwa na yenye ushindani ambayo inaweza kuhudhuriwa na mashabiki wengi.


Kuna hatua mchezaji wa Toto, alipigwa na jiwe kubwa mgongoni kiasi cha kupoteza fahamu kwa dakika kadhaa.

Polisi nao wakaanza kukimbizana na mashabiki kama vile vitani, hakika ilikuwa hali ya kusikitisha na hofu kubwa.

Mwadui FC vs Polisi Tabora
Dalili za vurugu zilianza kuonekana kabla ya mchezo huo kutokana na kuonekana kwa dalili za kushutumiana katika imani za kishirikina, mfano ni kitendo cha Polisi Tabora kuzuiwa kuingia uwanjani kwa muda.
      
Wakati mchezo ukiendelea, kulitokea vurugu za mashabiki wa timu hizo mbili, huku mashabiki wenye umri mdogo nao wakiwemo uwanjani, wengine wakiwa wameshika vilevi vilivyomo ndani ya chupa.

Mchezo huu haukuwa na vurugu nyingi lakini bado mazingira ya kiusalama hayakuwa mazuri kwa wahusika wote waliofika kushuhudia mechi hiyo.

Mtazamo
Inavyoonekana bado kuna tatizo kubwa kwenye suala la uelewa wa mashabiki wa baadhi ya mikoa, mazingira ya rushwa hasa kwa waamuzi ni makubwa, mazingira ya viongozi wa mikoa kubeba timu zao yamekithiri, waamuzi kutokuwa salama pia ni suala kubwa.


TFF na wadau wote tunatakiwa kuwa kitu kimoja katika kukemea na kuondoa madudu yanayoendelea kwenye soka letu, kwani ukimya au kulea yote hayo, matokeo yake ni kuzalisha matatizo makubwa zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic