Na Saleh Ally
MRISHO Ngassa huenda amekuwa kati ya wachezaji wachache sana
wanaoweza kuweka hadharani kitu ambacho walifanya na wanaamini hakikuwa sawa
kwa ajili ya maendeleo yao kimaisha.
Ngassa amesema anajutia uamuzi wake wa kukubali ushawishi wa kubaki
Tanzania na kuacha kwenda kujiunga na El Merreikh ya Sudan, moja ya timu tajiri
barani Afrika.
Naijua ishu ya El Merreikh, walikubali kutoa dola 50,000 (Sh Sh
milioni 87.5) kwa Azam FC, halafu kiwango kama hicho kwa Simba ambayo Ngassa
alikuwa anaichezea kwa mkopo wakati huo na dola 50,000 kwa Ngassa mwenyewe.
Ushawishi wa Yanga uliwashinda El Merreikh, Simba na Azam FC. Ngassa
akakubali kubaki Tanzania kuichezea Yanga kwa dau la Sh milioni 60 kwa mkataba
wa miaka miwili.
Inawezekana kabisa kilichosababisha Ngassa abaki nchini ni mambo
mawili tu na hakuna ubishi. Kwanza mapenzi yake kwa Yanga, pili ni mazoezi,
kukubali kuondoka nyumbani lazima uwe jasiri, si rahisi.
Wakati anaingia mkataba wa miaka miwili na Yanga, usisahau alikuwa
na kesi na Simba iliyokuwa inamdai Sh milioni 30. Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF) likaendesha kesi, ikafikia Sh milioni 45 baada ya kupigwa penalti ya Sh
milioni 15.
Wakati Yanga inamsajili, ilishamlipa fedha yake Sh milioni 30 ya
mwaka wa kwanza. Maana yake likaingia suala la deni na ndiyo chanzo cha
kuzaliwa kwa ule mkopo wa Benki ya CRDB, hilo tuachane nalo.
Ishu ninayotaka kuizungumzia ni uamuzi wa Ngassa kuamua kubaki
nyumbani wakati akijua kwenda El Merreikh kulikuwa na faida kubwa zaidi kwa
maana ya maslahi, pia kuweza kujitangaza zaidi kwa kuwa timu ile ni kubwa, ina
mafanikio makubwa zaidi na tajiri zaidi ya Yanga, wote tunalijua hilo.
Akabaki nyumbani, Ngassa hakuweza hata kuinua mguu. Nimesema mapenzi
na mazoea, ndiyo maana leo nimemuita muungwana kuwa mkweli kwa alichokosea,
huenda litakuwa funzo kwa wengi sana.
Unakumbuka wachezaji wangapi wao waliinua kabisa miguu yao, wakapata
timu barani Ulaya, halafu mapenzi yakawarudisha nyumbani na mwisho wake wao ndiyo
wakapoteza.
Mfano wa zamani kidogo ni ule wa Edibily Lunyamila aliyekuwa
Ujerumani. Viongozi wa Yanga wakafanya kila juhudi kumshawishi arejee nyumbani
ili kuisaidia Yanga kuimaliza Simba na ahadi kibao, baada ya kufanikiwa
walichotaka wakamsahau.
Haruna Moshi ‘Boban’ alipata nafasi katika timu ya Gefle IF
iliyokuwa Ligi Daraja la Kwanza Sweden. Wakati anafanya vizuri, kuna kiongozi
mmoja wa Simba akawa anafanya kila juhudi kuhakikisha anarejea nchini.
Kiongozi huyo alimsisitizia Boban kuwa maslahi ya nyumbani yangekuwa
bora. Ikaelezwa alimshawishi hadi kuanza vituko, ilimradi tu arudi nchini.
Jerry Tegete pia alipata timu ya daraja la kwanza nchini Sweden.
Akapewa mshahara wa dola 2,500 (Sh milioni 4.4) na nyumba nzuri ya kuishi. Lengo
walitaka wamuone, kipindi hicho Ligi Kuu Bara ilikuwa imebakiza mechi tatu,
Simba walishakuwa mabingwa.
Mechi ya mwisho ilikuwa kati ya Simba dhidi ya Yanga. Tegete
akaondoka Sweden baada ya kushawishiwa na viongozi, akarudi kuichezea Yanga
iliyofungwa mabao 4-3, Hilary Echesa akihitimisha ushindi wa Simba.
Tegete alikubali kuacha bahati ya kuonekana zaidi, kuwashawishi
Waswidi wamlipe mshahara mzuri zaidi na kumpa mkataba akarudi nchini kuichezea
mechi iliyokuwa sawa na ya kirafiki tu!
Wengi wamepita kwenye njia hiyo ya kushawishiwa na viongozi kwa
kisingizio cha mapenzi. Kwa kuwa nao wanayaamini mapenzi, basi wanajikuta
wanapoteza vitu vikubwa na kujuta baadaye kabisa.
Hakuna ubishi Boban aliwahi kusikia ishu ya Lunyamila, hali
kadhalika Ngassa alisikia ishu ya Tegete. Vipi sasa hakuna kati yao hakuna
aliyejifunza? Au inawezekana wahusika wamekuwa wakiihadithia kwa kuficha mambo
kwa ajili ya kutetea upande wao ili waonekane hawakukosea!
Lengo si kumlaumu mtu, lakini kueleza namna ambavyo ukweli wa Ngassa
unavyoweza kuwa funzo pia kwa kukumbuka mifano hiyo iliyopita ya kina
Lunyamila, Boban na wengine basi wachezaji wajifunze kuliko kusubiri nao
waharibu halafu wajute!
Mapenzi ni jambo jema, kuitumikia kampuni au kitu unachokipenda ni
bora lakini mara nyingi mtu hutakiwa kutafakari ushawishi ili kuepuka kuingia
kwenye majuto kama ambayo aliyoyaanika Ngassa leo.
Inawezekana wengi wameshindwa kwenda nje ya Tanzania kutokana na
ushawishi huo wa viongozi ambao wanakuwa wanaangalia zaidi maslahi yao kwa wakati
huo maana ndiyo wanakuwa viongozi.
Kwa kuwa viongozi wanakuwa wanaangalia maslahi yao. Basi wachezaji
amkeni, wakati mwingine wekeni mapenzi kando na muangalie maslahi yenu ili
kuepuka kukumbuka shuka kukiwa kumekucha.








0 COMMENTS:
Post a Comment