Uongozi wa klabu ya Stand United nao umeibuka na
kudai kuwa unashindwa kujua ni wapi ukashitaki kutokana na hujuma walizofanyiwa
na kusababisha mapato kuwa madogo.
Stand ambayo ilicheza na Simba, wikiendi iliyopita imelalama kuwa
kuna watu ambao wamo kwenye mamlaka za soka nchini ndiyo ambao wamekuwa
wakihusika katika hujuma mbalimbali.
Klabu hiyo inadai kuwa kuna watu ambao wamo ndani au wamekuwa
wakifanya kazi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamekuwa wakizinyonya
klabu na mfano halisi ni juu ya mapato ya mechi yao dhidi ya Simba kwenye
Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Katika mchezo huo, mapato yaliyotangazwa na TFF ni shilingi milioni
31, Stand ikaambulia milioni 6.5 huku Simba ikipata milioni 4.6.
Katibu Msaidizi wa Stand, Kennedy Nyagi, amesema walitafuta njia
mbadala ya kudhibiti mapato katika mechi hiyo lakini wakapigwa vita na watu
ambao alidai wanawategemea katika kuziendeleza klabu.
“Inaumiza sana, watu ambao tunawategemea ndiyo wanatuangusha, mapato
tuliyopata mchezo wetu na Simba hayafanani. Wameuza mpaka vishina vyote, maana
tiketi zimeuzwa mara tatu. Viongozi wanaodaiwa ni wa TFF na Bodi ya Ligi
walikuwepo pale, tulitoa mawazo yetu ili kuweza kunusuru ubadhilifu lakini wao
wakawa wanapinga.
“Inakuwa ngumu kwenda kulalamika hasa kwa vyombo husika wakati wao
ndiyo wanakuwa chanzo cha matatizo,” alisema Nyagi.
0 COMMENTS:
Post a Comment