February 27, 2015


Na Saleh Ally
KUNA wakati niliwahi kuandika kuhusiana na uamuzi wa Simba kusajili Waganda watano katika kikosi chake. Hakika sikuangalia suala la viwango na badala yake suala la wachezaji wote wa kigeni kuwa wanatokea taifa moja.


Sikuangalia viwango kwa kuwa lengo langu halikuwa hilo, niliangalia suala la nidhamu na umoja halafu sikuona sababu ya msingi kung’ang’ania kuwa na wachezaji watano kutoka Uganda.


Simba walijua mengi kutokana na rekodi walizokuwa nazo au hata kupitia timu jirani. Emmanuel Okwi amekuwa msumbufu sana hadi kufikia kuwa kero, lakini beki Joseph Owino naye aligeuka kuwa tatizo.

Wachezaji wa Uganda ndiyo wanaoongoza kwa kuomba ruhusa kurejea nyumbani kwao kwa sababu mbalimbali, hasa zile zinazohusiana na masuala ya kifamilia.

Kwa kiwango, unaweza kusema ni wachezaji wazuri, mfano Okwi, Owino ni wale ambao uwezo unaonekana wazi. Juuko Murshid pamoja na kuwa mgeni lakini kaonyesha uwezo.

Kwangu Dan Sserunkuma ni mtu anayejua mpira kutokana na uwezo wake lakini hadi sasa hajatumia uwezo wake wote kuona Simba inafanikiwa, hali kadhalika Simon Sserunkuma.

Binadamu ni wabinafsi, wakati mwingine hujipendelea hata bila ya kujua walichofanya si sahihi, hii ilikuwa moja ya hofu zangu, kwamba ni moja ya mambo ambayo yanaweza kutokea.

Waganda lazima wataunda “Kampala” ndani ya Simba. Hakuna ubishi watateteana na ikiwezekana kutengeneza kikundi cha Waganda.

Katika hali ya kawaida unaweza kulichukulia suala hilo kama ni la kawaida sana kama ambavyo niliwahi kumsikia kiongozi mmoja wa Simba akisisitiza wao walichoangalia ni kiwango.

Jiulize, Simba imewaacha wachezaji wangapi licha ya kuwa na viwango vizuri? Sasa vipi isiangalie athari za Waganda watano ambao akikosea mmoja, akiadhibiwa mmoja au vinginevyo wanaweza kuanzisha maandamano?

Juzi nimesikia, kundi la wachezaji hao wa Kiganda liliamua kuhama kutoka katika hoteli ya kisasa ya Saphire Court ya jijini Dar es Salaam na kwenda kuishi katika hoteli nyingine.

Vigumu sana kusema Saphire si hoteli isiyo na viwango. Inajulikana kwa ubora, lakini Waganda hao wote wameondoka na kupanga hoteli bila ya ruhusa ya uongozi. Vipi Waganda hao wanakuwa na uamuzi wowote bila ya kuwashirikisha viongozi? Jibu, wamefanya kwa kuwa wako wengi na wana uwezo wa kuteteana.

Kwa uongozi, walichofanya wachezaji hao ni sehemu kubwa ya dharau kwa kuwa wanajua wako wengi na wakifanya lolote si rahisi kuwaadhibu wote na wanajua hilo kwa kuwa wanawajua viongozi wao.

Mawazo yanaweza kufanana, utaifa unaweza kuwa sehemu ya ushawishi. Haya yote viongozi wanayajua na ndiyo maana hata wachezaji hao Waganda walipopewa nyumba, wote wakakataa kwa kuwa mmoja wao alianza kuikataa.

Kama hali hiyo itaendelea na uongozi ukaifumbia macho, basi bila shaka hakuna ubishi kwamba mbele itasumbua na kuleta mgawanyiko na kusababisha kutokuwa na maelewano kati ya Watanzania dhidi ya Waganda.

Ukiangalia hata viwango vya uchezaji, mimi bado naweza kutofautiana na wengi. Kwamba Okwi, Sserunkuma na ndugu yake, bado hawajaonyesha kiwango sahihi cha kuisaidia Simba hadi sasa na kama kweli wanalipwa vizuri na wanaamini wako kufanya kazi, lazima waongeze juhudi na kuongeza zaidi ya walipo sasa.

Kwa upande wa uongozi wa Simba ukubali umeshafanya kosa na usumbufu huu hata wakiuficha utaendelea kuwa tatizo. Hivyo wawe makini na suala la nidhamu na usawa, la sivyo watasababisha mgawanyiko au mpasuko.


Tunajua Simba kwa sasa inakwenda kwa mwendo wa kusua. Pamoja na hali mbaya, bado ina wachezaji wanaoweza kubadili mambo lakini lazima wabadili juhudi kwa kuwa sura zao hazitaweza kucheza!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic