NGASSA AKISHANGILIA JANA BAADA YA KUFUNGA BAO PEKEE LA YANGA.... |
Bao la Mrisho Ngassa ndiyo lililoiondoa Yanga katika matatizo ambayo yangeweza kuiweka kwenye wakati mgumu nchini Botswana.
Yanga imefuzu katika hatua ya Kombe la Shirikisho dhidi ya BDF XI ya kwa jumla ya mabao 3-2.
Ilianza kwa kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Amissi Tambwe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar kabla ya kupoteza kwa mabao 2-1 katika mji wa Lobatse, Botswana.
Katika kipindi cha kwanza cha mechi hiyo ya pili, hakuna ubishi Yanga ilikuwa na nafasi ya kushinda hata mabao manne.
Ilipata nafasi tatu safi kabisa kupitia kwa Ngassa, Tambwe na Simon Msuva, kauli nzuri ya kutamba ni hivi, "wakazichezea".
Mwamuzi wa mechi hiyo, ukiondoa ushabiki utakubaliana nami hakuwa "mzuri" kwa Yanga hasa katika kipindi cha pili kutokana na kuibania kwa makusudi kwa mara kadhaa.
Kwa kuwa alilazimika kutoa kadi nyekundu kwa mchezaji wa BDF aliyemuumiza kwa makusudi Msuva, kipindi cha pili aliingia akiwa na kila njia ya kuhakikisha anatengeneza kadi nyekundu kwa Yanga.
Watu waliokuwa hatarini kupata kadi ni wale waliokuwa tayari wana njano, mmoja wao ni Danny Mrwanda, akaruka kupiga kichwa katika hali ya kawaida kabisa, mwamuzi akampa kadi ya pili ya njano na kuzaa nyekundu.
Haikuwa haki lakini hiyo ndiyo maana ya kucheza ugenini wakati mwingine hasa kwa mechi za bara la Afrika, Ulaya kunakuwa na ugumu kidogo katika hilo.
Tunajua Yanga hata katika Ligi Kuu Bara ndiyo timu inayoongoza kwa kutengeneza nafasi nyingi sana. Lakini inaongoza kwa kutozitumia.
Katika mechi ya kwanza jijini Dar, hali kadhalika, Yanga ilikuwa na uwezo wa kuibuka na ushindi wa bao nne au zaidi. Lakini mwisho wake ikaishia kwenye "aaah", "aaah" ambazo hazina faida kwa timu.
Kuna kila sababu ya wachezaji wa Yanga kuliangalia hilo kwa kuwa tena si kazi ya kocha wala hapaswi kuhojiwa.
Wazi wao hawataki kuzipoteza, lakini mtu makini ni yule mwenye makosa machache. Unapokuwa na makosa mengi unaitwa si makini. Hii Ndiyo tofauti.
Hivyo washambuliaji wa Yanga, bado hawajaingia kwenye makini kama utafanya tathmini ya nafasi wanazopata ukilinganisha na zile wanazozitumia.
0 COMMENTS:
Post a Comment