Na Saleh Ally
Yanga ilizaliwa mwezi huu, mashabiki wa Yanga wanajua
kuwa wapo katika mwezi muhimu kwa kuwa ndiyo kipindi ambacho klabu yao pendwa
ilianza kuhesabika.
Februari 12, 1935, Yanga ikawa hewani. Ndiyo maana ni
sahihi kusema tayari klabu hiyo imetimiza miaka 80.
Hakuna ubishi tena kwamba Yanga iliyoanza kwa jina la
New Youngs, ndiyo klabu kongwe nchini na huenda ndiyo jambo kubwa zaidi
wanachama na mashabiki wake wanaweza kujivunia. Simba imetokea ubavuni mwake,
hali kadhalika Pan African na zote zinajulikana kama klabu kongwe.
Katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mashabiki na
wanachama wa Yanga kutoka sehemu mbalimbali nchini na nje ya mipaka ya Tanzania,
wamekuwa wakisherehekea klabu yao kufikisha umri huo mkubwa.
Nilisikia baadhi ya wanachama na mashabiki hao walikuwa
katika maandalizi kwa ajili ya kufanya sherehe za miaka hiyo ya kuzaliwa kwa
klabu yao.
Wana haki ya kufurahia umri mkubwa lakini najaribu
kujiuliza, kwa miaka au umri wa Yanga na ilichonacho sasa ni sawa kushangilia
au ni bora kuweka ‘msiba’?
Yanga inategemea mapato yake, inategemea kujiendesha
kupitia soka, unaweza kusema uhai wa klabu hiyo ni soka? Lakini katika umri wa
miaka 80, haina hata uwanja wa mazoezi!
Yanga yenye miaka 80, yaani 40 mbili au 20 mara nne,
haina timu ya vijana ya kueleweka. Haina chumba kwa ajili ya kuweka kumbukumbu
zake, Wazungu wanasema museum. Ungeweza kuona makombe na picha za wakongwe,
viongozi waliopita na mambo mengine.
Hata makao makuu ya klabu, mazingira ni mabaya, ya hovyo
kabisa na huenda viongozi wakasikia vibaya kuambiwa kwa kuwa kweli panatia
aibu!
Ukiachana na mpira, pamoja na ukubwa wa Yanga, klabu
hiyo haina biashara nyingine yoyote iwe ya kuuza jezi, vibeba ufunguo, kofia,
mipira, bendera na vitu vingine, ipo tu ili mradi.
Yanga kama klabu, ingeweza kujivunia migogoro,
kutopendana, watu kufanyiana majungu, kusengenyana, unafiki na mengine ambayo
si ya maendeleo.
Ukiwa muungwana tulia, tafakari uone kama kweli Yanga
ina kitu kikubwa cha kujivunia zaidi ya rangi zake mbili, kijani na njano na
ndiyo kitu namba moja mashabiki wake wanaweza kukitanguliza mbele yao kwa
mafanikio makubwa.
Yanga haijafanya vizuri michuano ya Caf, hauwezi
kuifananisha na TP Mazembe, Enyimba, El Merreikh, Al Ahly, Zamalek na timu
nyingine kongwe za Afrika.
Yanga ilipata maendeleo makubwa katika miaka ya 1970 na
1980 baada ya hapo, mafanikio yake ni ya hadithi zaidi kuliko vitu
vinavyoonekana.
Angalia majengo yake mawili, lile la makao makuu, makutano
ya mitaa ya Jangwani na Twiga na lile la Mtaa wa Mafia jijini Dar es Salaam,
yalijengwa na kina babu.
Tangu waliopo ambao unawaita vijana waanze kuongoza
klabu hiyo mwishoni mwa miaka ya 1990 na sasa ya 2000, hawana jengo au kitega
uchumi chochote kilichoongezeka na hata yale majengo waliyoachiwa, mfano Uwanja
wa Kaunda, yamechakaa.
Waliopo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2000, ni wale
wanaoweza kutunza rekodi nyingi katika makaratasi na si utendaji. Walio na
mipango mingi isiyotekelezeka.
Hivyo kuliko Yanga kukutana na kufanya sherehe ya
kufurahia kutimiza miaka 80, vema wangekutana na kufanya ‘msiba’ wa kutathmini
kuwa pamoja na kufikisha umri huo, wana nini cha kujivunia?
Hadi wanafikisha miaka hiyo, tangu waliokuwa wakijulikana
kama vijana waanze kuchukua klabu, wamefanya nini, kipi wanacho cha kujivunia,
wapi wameteleza, nini cha kufanya, wapi wabadili gia? Kama wakiona sherehe
ndiyo sahihi, maana yake wameridhika kusherehekea miaka 100 wakiwa hapo walipo.







Sawa Saleh sasa tutafanya bethidei ya simba hapo mwakani,tutakualika mwanachama wetu ila TFF hatuwataki kwani wamezidi kutuwekea ngumu wanalunyasi!
ReplyDelete