February 9, 2015


Muziki wa kuchekesha wa viongozi Coastal…

Na Saleh Ally
NILIMSIKIA kiongozi mmoja wa Coastal Union akisema wamechukua uamuzi wa kuhamia kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kwa kuwa wamekuwa wakihujumiwa nyumbani kwao Mkwakwani.


Kiongozi huyo alisema maneno hayo wakati akihojiwa kwenye redio, eti uamuzi wao wa kuhama Mkwakwani ni kukwepa hujuma na wameona nje ya nyumbani kwao wamekuwa hawana matokeo mazuri ukilinganisha na nje.

Maneno ya kiongozi huyo wa Coastal Union ilikuwa ni picha halisi ya kuonyesha kiasi gani soka yetu imejaza viongozi wengi wenye vipaji vya kubabaisha mambo.

Maelezo yake ni kwamba Coastal Union Tanga inahujumiwa, ajabu! Maana hata hata data kwamba hujuma hizo ni za namna gani? Pia hajui nyumbani wamcheza mechi ngani na kushinda au kupoteza ngapi?

Anatolea mfano wa ugenini kwamba ndiyo wamekuwa wakifanya vizuri, lakini inaonyesha pia hana data huko wamepoteza mechi ngapi?

Hata wale viongozi wa Kagera Sugar waliosema wanahama CCM Kirumba, Mwanza kwa madai wanahujumiwa, hawakuweka wazi wanahujumiwa vipi kwa kuwa wachezaji ni 11 kwa 11 na waamuzi ni walewale.

Hata kama wamehamia Kambarage Shinyanga, basi hawatakwenda kitu. Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo unaweza kufanya waamini wako sahihi!

Ukiwasikiliza Kagera Sugar pamoja hali kadhalika Coastal Union utagundua ni hisia potofu za kishirikina kwa kuwa data zinawakana na hasa Coastal Union na Mkwakwani ambako ni nyumbani.

Jaribu kuwaza kama unaweza kusikia kauli ya kizembe kama hii: “Manchester United wameamua kuhama Old Trafford na sasa watatumia Uwanja wa zamani wa Arsenal wa Anfield kwa kuwa wanahujumiwa!”

Sasa Coastal ina viongozi wenye ndoto za kutaka kukimbia nyumbani, kwa hujuma wanazoshindwa kuzianisha hadharani.

Viongozi waoga, wasiojua data za kile wanachozungumza, ili mradi wameamua kwa kuwa ukienda kwa hesabu, Coastal Union imecheza mechi 14. Kati ya hizo, imeshinda tatu tu, sare 6 na imepoteza tano.

Katika mechi 14, nyumbani imecheza mechi  ya hizo, mechi 8 na ugenini mechi 6. Takwimu zinaonyesha Coastal imeshinda nyumbani mechi 2 na ugenini mechi moja.

Ikiwa nyumbani imetoka sare 3 kama ilivyo kwa ugenini.  Mkwakwani imepoteza mechi 2 na idadi hiyohiyo imepoteza ugenini.

Coastal imepoteza mechi nne, 2 ugenini na 2 nyumbani. Sasa hawa viongozi wa Coastal wanakimbilia nini ugenini? Kama wanahujumiwa nyumbani, mbona hakuna tofauti ya kupoteza na wanakokwenda? Au yule kiongozi alikuwa ana maanisha nini hasa?

Maana yake Coastal Union hawana lolote la kujitetea kwa wanachama na mashabiki wao kutokana na timu inavyofanya. Wanatafuta pa kushika na kama ilivyo ada, viongozi wa soka nchini hawapendi kukubali matokeo zaidi ya kutafuta wa kuwaangushia mzigo.

Kwangu naona kama ni muziki unaochekesha tu, maana inaonekana hata data za mechi ngapi wamcheza, ngapi wamepoteza au kupata sare basi angalau waseme wazi kuwa wanahujumiwa vipi na namna gani kuliko kuzungumza mambo kwa kubahatisha.

Tabia ya viongozi kama wa Coastal ni wale wasiopenda kukosolewa, maana lawama ni sehemu ya silaha ya kujilinda kwao na watu wa namna hiyo hawawezi kuusaidia mchezo wa soka maana hawazikubali changamoto, badala yake wanazigeuza kuwa lawama.

Kama kweli tunataka maendeleo, lazima tuwe na viongozi imara, wanaoangalia maendeleo badala ya kugeuza lawama zisizokuwa na msingi ni silaha ya kuepusha matatizo.

Wanachopaswa kuangalia ni wanapungukiwa nini, wachezaji wamepewa fedha zao za usajili, mishahara yao inalipwa kwa wakati?

Lakini waangalie wana uwanja mzuri wa mazoezi na vinapatikana? Matunzo ya wachezaji wao yakoje na kadhalika lakini kusemasema tu ilimradi halafu hata kinachozungumzwa hawana uhakika nacho!


MATOKEO:

Sept 21:
Simba 2-2 Coastal 

Sept 27:
Mbeya 1-0 Coastal

Okt 4:
Coastal 2-1 Ndanda

Okt 18:
Coastal 2-0 Mgambo

Okt 25:
Kagera 1-1 Coastal

Nov 1:
Coastal 1-0 Ruvu

Nov 8:
Azam 2-1 Coastal


Dec 27:
Prison 0-0 Coastal

Jan 3:
Coastal 0-1 JKT

Jan 18:
Coastal 0-0 Polisi Moro

Jan 25:
Stand 0-1 Coastal

Jan 31:
Coastal 0-0 Mtibwa

Feb 4:
Coastal 0-1 Yanga

Feb 7:
Coastal 0-0 Simba


TAKWIMU:
Zote: 14
SHINDA: 3
SARE: 6
POTEZA: 5

Nyumbani: 8
SHINDA: 3
SARE: 3
POTEZA: 2

Ugenini: 6
SHINDA: 1
SARE: 3
POTEZA: 2






0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic